Mwanzilishi wa kampuni ya simu ya Huawei asema Marekani hawawezi kuiangusha kampuni yake

Ren Zhengfei

Chanzo cha picha, Alamy

Mwanzilishi wa kampuni ya simu ya Huawei amesema hakuna "njia yeyote ambayo Marekani inaweza kuivunja" kampuni hiyo.

Katika mahojiano maalumu na BBC, bwana Ren Zhengfei ameelezea kukamatwa kwa binti yake Meng Wanzhou mwezi Disemba, ambaye ndiye mhasibu mkuu wa kampuni hiyo ni hatua ya kisiasa zaidi.

Marekani imeazimia kumfungulia mashtaka bi Meng na kampuni ya Huawei kwa tuhuma za kutakatisha fedha, ubadhirifu wa kibenki na kuiba siri za kibiashara.

Kampuni ya Huawei hata hivyo inakanusha madai hayo.

"Hakuna namna Marekani inaweza kutuvunja," amesema kwa mara ya kwanza toka mzozo huo uanze. "Dunia haiwezi kututupa kwa sababu tumepiga hatua kubwa. Hata kama watawashawishi baadhi ya mataifa kuwa wasitutumie kwa muda, pia tunaweza kupunguza uzalishaji kidogo."

Hata hivyo ameonesha wasi wasi wake kuwa endapo hatua hiyo itatokea basi itakuwa na athari.

Je Huawei ni kibaraka wa China?

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Meng Wanzhou alikamatwa Canada na kupelekwa Marekani

Huawei, ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya binafsi China imekuwa ikihusishwa na kutumika na serikali ya China.

Marekani na baadhi ya washirika wake wamekuwa wakidai kuwa teknolojia ya Huawei inatumika na mashirika ya ulinzi ya China kuwapeleleza.

Kwa mujibu wa sheria ya China, makampuni ya nchi hiyo yanalazimika "kuisaidia serikali katika shughuli za upelelezi wa Taiafa."

Hata hivyo Ren amesema kukubali kufanya upelelezi ni hatari ambayo asingeweza kuifanya.

"Serikali ya China imeliweka wazi suala hili kuwa haiwezi kufanya jambo hilo. Hatuwezi kufanya kuwakera wateja wetu duniani kote kwa ajili ya kitu kama hiki. Kampuni yetu haiwezi kufanya shuguli za kiupelelezi."

Kutengwa na Dunia

Wiki iliyopita, waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo ameonya kuwa washirika wake kutumia teknolojia ya kampuni ya Huawei na kudai kuwa itafanya kuwe na shida kwa Marekani kushirikiana nao.

Australia, New Zealand na Marekani tayari wameshapiga marufuku ama kuzuia kampuni ya Huawei kusambaza mitambo kwa ajili ya miradi yake ya baadae ya mfumo wa mawasiliano ya intaneti ya simu ya 5G.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Huawei imesema hawahatarishi usalama wa nchi yeyote ikiwemo Marekani

Wakati huo huo Canada inafanya tathmini kuona iwapo kampuni hiyo ni tishio kwa usalama wake.

"Kama taa zitazimwa Magharibi, Mashariki kutaendelea kung'aa. Na kama Kaskazini kutaingia kiza, bado Kusini kupo. Marekani haiwakilishi dunia. Marekani ni sehemu tu ya dunia."

Kitengo cha Usalama wa Kimtandao wa Uingereza kimesema kuwa hatari yeyote itakayotokana na kutumia teknolojia ya Huawei inaweza kudhibitiwa.

Makampuni mengi ya mawasiliano ya Uingereza wanaitumia Huawei katika maandalizi yao ya kuhamia katika mfumo wa 5G. H

Hata hivyo, tathmini rasmi ya serikali inatarajiwa kutolewa mwezi Machi ama Aprili na itawapa muongozo iwapo waendelee kutumia Huawei ama la.

Akizungumzia uwezekeno wa kupigwa marufuku Uingereza Bw Ren amesema: "hatutajiondoa nchini Uingereza kutokana na hili. Zaidi tutaongeza uwekezaji wetu maana bado tunaimani na Uingereza na tunaamini Uingereza itaendelea kutuamini zaidi. Na kama Marekani hawatuamini basi tutawekeza Uingereza kwa nguvu kubwa zaidi."