Siasa Uganda: Je, ni kweli Museveni anamuandaa mwanawe kumrithi madaraka?

Luteni Jenerali Kainerugaba Muhoozi
Maelezo ya picha,

Luteni Jenerali Kainerugaba Muhoozi anadaiwa kupikwa ili amrithi baba yake Yoweri Museveni uraisi wa Uganda

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amempandisha cheo mwanawe wa kiume na kufikia cheo cha pili kwa ukubwa zaidi jeshini.

Kainerugaba Muhoozi sasa amepanda kutoka kuwa Meja Jenerali na kufikia Luteni Jenerali katika jeshi la Uganda.

Kwa cheo hicho sasa Muhoozi mwenye miaka 44 yupo cheo kimoja nyuma ya baba yake ambaye ni Jenerali kamili.

Ndani ya miaka sita iliyopita, Jenerali Muhoozi amepanda vyeo mara tatu. Japo amekuwa mkuu wa vikosi maalumu vya jeshi la Uganda na sasa anahudumu kama mshauri wa rais wa operesheni maalumuupandaji wake wa vyeo unaonekana ni wa kasi kubwa.

Kasi hiyo ndiyo ambayo wakosoaji wa rais Museveni na wanaharakati wanadai ni kielelezo kuwa kuna mipango unaosukwa wa mtoto huyo wa rais kumrithi baba yake.

Museveni tayari ana miaka 74 na ameshadumu madarakani kwa miongo mitatu.

Hata hivyo, Jenerali Muhoozi amekuwa akikanusha kuwa ana mipango ya kujiingiza kwenye masuala ya siasa.

Chanzo cha picha, Reuters

Mwaka 2013 kipindi hicho akiwa Brigedia Jenerali na mkuu wa vikosi maalumu Jenerali Muhozi alidai kuwa Uganda haina utawala wa kifalme.

"Uganda sio ufalme ambapo uongozi unarithiwa kutoka baba hadi kwa mwanawe...uamuzi wa kuamua ambavyo Uganda itaongozwa ni jukumu la wananchi wenyewe wala sio mtu mmoja kama wanavyosema baadhi ya watu,'' ilisema taarifa rasmi yake rasmi.

Mwaka huo, Magazeti ya Daily Monitor na Red Paper yalichapisha barua iliyofichuliwa na ambayo ilikuwa na maudhui ya mpango wa kumrithisha mamlaka mwanawe Museveni. Barua hiyo iliandikwa na Jenerali mkuu katika jeshi, David Sejusa, akidai kuwa Museveni ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka 1986 anamuandaa mwanawe kumrithi.

Sejusa, kwa jina lengine Tinyefuza, alikimbilia nchini Uingereza baada ya kudai kuwepo mpango wa kuwaua wanajeshi wanaopinga mpango huo, ingawa madai hayo yalikosolewa na majenerali wengine jeshini.

Magazeti hayo mawili na vituo viwili vya redio vilifungiwa kwa siku 10 kwa kuchapisha barua hiyo.