Je wanaume nao wanafaa kuchukua jukumu la kupanga uzazi?

Nchini Tanzania rais John Pombe Magufuli amewataka wananchi kutopanga uzazi

Licha ya ongezeko la idadi ya wanawake wanaotaka kuzuia mimba, matumizi ya vifaa vya kisasa vya kuzuia mimba katika jangwa la sahara yamesalia kuwa ya viwango vya chini.

Kwa mfano nchini Kenya robo tatu ya wanawake waliopo katika ndoa kati ya umri wa miaka 15 hadi 49 wanataka kuzuia kupata mimba ama hata kuchelewesha kwa miaka miwili, ijapokuwa ni asilimia 39 inayoripoti kutumia mbinu hizo za kisasa.

Ongezeko la matumizi ya mbinu hizo za kuzuia mimba huenda likasababisha mimba chache zisizo na mpango , kushuka kwa vingo vya maambukizi ya HIV kutoka kwa mama hadi mtoto visa vichache vya uavyaji mimba mbali na vifo vya watoto.

Ni kutokana na sababu hizo ambapo wanasayansi wamelazimika kutengeneza dawa ya kuzuia mimba ambayo wanasema ina athari ya viwango vya juu, iko salama na haiathiri hamu ya utendaji ngono.

Majaribio ya dawa hiyo kwa jina dimethandrolone undecanoate or DMAU, yalifanikiwa nchini Marekani.

Watafiti wamegundua kwamba dawa hiyo inakandamiza nguvu za homoni za kiume hadi kuziangamiza.

Homoni za Testosterone ndio homoni zinazodhibiti nguvu za kiume.

Lakini Je wakati umefika kwa wanaume kuchukua jukumu la kupanga uzazi?

Je watakuwa tayari kuchukua gharama, athari za kudhibiti uzazi na badala yake kuchukua jukumu ambalo limekuwa likiachiwa wanawake?

Kuna majaribio mengi yenye matokeo mazuri kuhusu mbinu hiyo ya kuzuia mimba miongoni mwa wanaume huku ripoti zikisema kuwa kuna matumaini ya kuwa na dawa hiyo ama hata sindano katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Tulimuuliza Charles mwenye umri wa miaka 33 iwapo angetumia dawa hiyo ya kupanga uzazi.

Alifikiria swala hilo kwa sekunde chache halafu akauliza , ''Subiri dakika moja, je inamaanisha kwamba nitakuwa siwezi kutoa kitu wakati wa tendo la ndoa ama?''.

Charles ambaye hajaoa lakini ana uwezo wa kufanya ngono anaendelea kuelezea, ''Unajua ni kwa nini wanaume wengi watakujibu hapa''.

''Kwa sababu hata iwapo mwanamume hataki mtoto, bado wanataka kuwa na uwezo wa kuweza kuzalisha. Najua dawa hiyo haitaathiri uwezo wangu wa kushiriki tendo la ngono lakini siwezi''.

Jimmy Mumbo ambaye ni kijana aliyeoa hivi majuzi anasema kuwa kuhusika kwa wanaume kupanga uzazi hakutaathiri shughuli yote ya upangaji wa uzazi .

Anasema kwamba wanawake ndio wanaobeba mimba hivyobasi wao ndio muhimu kuhusika zaidi.

Lakini daktari Charles Ochieng ambaye anahusika na ukataji wa mirija ya mwanamume katika shughuli ya upangaji uzazi anapinga wazo hilo akisema kuwa sio mwanamke anayejipatia mimba pekee.

Daktari huyo anasema kuwa kuna baadhi ya wanawake ambao hupata madhara wanapotumia dawa hizo wakati wa kujifungua ama hata baada ya miaka kadhaa hivyobasi anawataka wanaume kuchukua jukumu hilo la kupanga uzazi badala ya wanawake.

''Kuna sababu ambazo zinafanya mwanamume kujishughulisha katika maswala ya upangaji wa uzazi lazima umchunguze mkeo afya yake na ujue anapata matatizo gani pengine kwa mfano anapojifungua'', alisema.

Lakini Catherine Henry ambaye ni mzazi nchini Tanzania anasema kuwa swala la afya ya uzazi ni swala la kifamiia.

Anasema kwamba familia inayopanga uzazi inakuwa na malengo mazuri kiuchumi , kijmii na hata kiafya.

'' Hili sio swala la mzazi mmoja kuamua, zama za kutegemea mwanamke ambaye ndiye anayeshika mimba kupanga uzazi limepitwa na wakati, inapendeza kuona kwamba pia akina baba nao wanashiriki katika mpango huu'', alisema bi Catherine.

Matatizo yote ya uzazi hulimbikizwa akina mama

Hoja hiyo imeungwa mkono na mhadhiri wa chuo kikuu cha Kyagombo nchini Uganda Ida Mtenyo ambaye anasema kuwa matatizo yote hulimbikiziwa wanawake.

''Kwa nini wanaume wanakwepa upangaji uzazi, wana malengo yapi, kila mara Upangaji wa uzazi ni wa akina mama, kuzaa watoto wengi ni akina mama kutozaa ni akina mama shinda zote zinazotokana na upangaji uzazi ni za kina mama.

Hatahivyo Jimmy Mumbo amelipinga hilo na kusema kuwa mwanamke ana mwili anao uelewa na kwamba sio lazima atumie dawa fulani ili kupanga uzazi.

''Kuna njia nyingi za kupanga uzazi, sio lazima mwanamke atumie dawa ndio apange uzazi kuna njia za mawazo''.

Lakini Daktari Charles anasisistiza kuwa kuna njia kadhaa ambazo zinaweza kutumika kuzuia mimba kama vile utumizi wa mipira na kudungwa sindano lakini anaongezea kuwa mbinu hizo zina viwango vya kuweza kufeli kwa hivyo njia mwafaka ni mwanamume kufungwa kizazi chake.