Vinasaba vya samaki aina ya papa vyaweza kusaidia matibabu ya saratani na magonjwa yatokanayo na uzee

Shark

Chanzo cha picha, Getty Images

Papa aina ya 'great white' inawezekana wakawa wanashikilia siri za kutibu saratani na maradhi mengine yanayoambatana za uzee.

Watafiti kwa kutumia mfumo wa vinasaba wa papa hao wamebaini pingili ambazo zinawalinda samaki hao dhidi ya saratani na magonjwa mengine.

Wanasayansi wanaamini kuwa utafiti zaidi unaweza kusaidia kutimia matokeo hayo katika kutibu magonjwa yatokanayo na umri mkubwa kwa binaadamu.

Aina hiyo ya papa wanaweza kujitibu vinasaba vyao katika namna ambayo haiwezekani kwa vinasaba vya binadamu.

Utafiti huo umefanyika katika chuo kikuu cha Nova Southeastern Florida, Marekani.

Jeni, au sehemu ya vinasaba inayorithisha tabia au maumbile fulani, ambazo si thabiti za binaadamu ndizo ambazo hufanya watu kupata maradhi ya saratani na mengine ambayo huendana na uzee.

Papa hao wapo baharini kwa zaidi ya miaka milioni 16 sasa, dahari na dahari kabla ya uwepo wa binadamu, na hufikia mpaka urefu wa futi 20 na ukubwa wa uzito wa tani tatu.

Chanzo cha picha, Reuters

Vinasaba vya papa ni vikubwa kwa mara moja unusu zaidi ya binadamu, hiyo ina maana kuwa kuna vitu samaki hao wanaweza kuvifanya ambayo binadamu hawawezi.

Na wanasayansi sasa wanatazamia kufumua siri hizo ili kutatua maradhi hayo kwa binadamu.

Pia papa hao wanatazamiwa kusaidia matibabu ya kuzuia damu kuvuja sababu wana uwezo mkubwa wa kupona majeraha hatari.

Utafiti huu sasa utaongeza umaarufu wa samaki hao ambao ni moja ya wanyama wanaoogopwa zaidi kutokana na meno yao makubwa na makali.

Chanzo cha picha, Reuters

Mpiga picha Kimberly Jeffries hivi karibuni ameiambia BBC kuwa hakujihisi kuwa kwenye hatari alipoogelea na moja ya papa mkubwa zaidi wa jamii hiyo afahamikaye kama Deep Blue.

"Ni fursa adimu..." amesema bi Kimberley na kuonya watu hata hivyo kutowakaribia wanyama hao. "Hawa ni wawindaji wenye nguvu, hivyo inabidi waheshimiwe."

Papa hao huwinda jamii nyengine za samaki hususani wale ambao ni walegevu.

Tafiti pia zinaonesha kuwa papa ni muhimu kwenye mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa viumbe wanaowawinda zaidi ni wale ambao huchafua zaidi hewa baharini.