Simba na Yanga: 'Nilizimia baada ya kumuweka mke rehani kwa shabiki wa Simba'

Simba na Yanga: 'Nilizimia baada ya kumuweka mke rehani kwa shabiki wa Simba'

Je unaweza kumweka mkeo au mumeo rehani ukiwa na matumaini kuwa timu unayoishabikia itashinda mechi yake dhidi ya mpinzani wake wa jadi?

Jimmy Kindoki ni shabiki wa sugu wa klabu ya Yanga ya Tanzania, lakini mapenzi kwa klabu yake nusura yamtokee puani wikendi.

Siku ya Jumamosi timu yake ilikutana na watani wao wa jadi klabu ya Simba.

Akiwa na matumaini makubwa ya ushindi, Kindonki aliweka dau ambalo baadae alilijutia na shabiki mmoja wa Simba aitwaye Justine Kessi.

Mapatano yao yalikuwa endapo Yanga itashinda, Kessi angempa Kindoki mshahara wake wote. Na endapo Yanga wangefungwa basi Kindoki angemoa Kessi mke wake akae nae kwa muda wa wiki moja.

Mpira ukapigwa, dakika tisini kuisha, Simba ikaibuka na ushindi wa goli moja bila majibu.

Kessi akamfuata Kindoki ili ampe mkewe kama walivyokubaliana. Kindoki alizimia kwa uchungu na woga. Picha za video za tukio la kuzimia kwake zilitapakaa kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, wawili hao mwishowe wamekubaliana malipo ya pesa. Kindoki sasa atamlipa Kessi dola 200 badala ya kumtoa mkewe kwa siku saba.