Serbia: Mpenzi wa waziri mkuu Ana Brnabic ajifungua mtoto wa kiume

Serbian Prime Minister Ana Brnabic attends a session within the 12th Economic Summit in Berlin

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Ana Brnabic alaumiwa kwa kushindwa kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja

Mpenzi wa jinsia moja wa waziri mkuu wa Serbia Ana Brnabic amejifungua mtoto wa kiume.

Ripoti zinasema kuwa mama aliyejifua anayefahamika kama Milica Djurdjic pamoja na mtoto aliyepewa jina la Igor wote wana afya nzuri.

Bi Brnabic mwenye umri wa miaka 43 amekuwa ni mwanamke wa kwanza ambaye anajihusisha katika mapenzi ya jinsia moja kuwa waziri mkuu mwaka 2017 mwezi Juni.

Kuchaguliwa kwake kuliwashangaza wengi kwa sababu taifa hilo halitambui ndoa za watu wa jinsia moja.

"Ana Brnabic ni waziri mkuu wa kwanza ambaye mwenza wake amepata mtoto wakati akiwa madarakani na vilevile ni mahusiano ya kwanza ya jinsia moja duniani kote kupata mtoto," AFP iliripoti.

Bi Djurdjic ambaye ambaye anafanya kazi kama daktari, alipata ujauzito kwa njia ya kupandikiza na sio asili.

Serbia ni nchi ambayo inafuata mila na desturi na ubaguzi ni jambo ambalo lipo kwa wingi.

Katiba ya nchi hiyo imeweka wazi kuwa ndoa inayokubalika ni ya mwanaume na mwanamke na mahusiano ya wapenzi wa jinsia moja hayatambuliki kitaifa.

Wapenzi wa jinsia moja nchini humo wamezuiwa kuasili watoto, ingawa mtu ambaye hajaoa au kuolewa anaweza kuasili mtoto.

Nchi hiyo ina sheria ambazo zinawabagua wapenzi wa jinsia moja hivyo kukabiliana na changamoto za kauli za chuki, kukosa haki licha ya wanaharakati wamekuwa wakipinga ukiukwaji huo wa haki.

Wakosoaji wamedai kuwa Bi Brnabic hajafanya lolote kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja.

Na hajawahi kusema kama atapenda kuhalalishwa kwa ndoa za jinsia moja nchini Serbia.