Uganda yasisitiza ina uhusiano mzuri na Rwanda licha ya tuhuma za mgogoro

Rais Kagame na Rais Museveni

Chanzo cha picha, PETER BUSOMOKE

Serikali ya Uganda imetupilia mbali madai kwamba uhusiano wake na utawala wa Rwanda umezorota.

Ufafanuzi huu unafuatia kile kinachotajwa kuwa mgogoro kati ya mataifa hayo jirani ambapo Rwanda inaikosoa Uganda kwa kuwasaidia wapinzani wake walio chini ya vuguvugu la Rwanda national Congress, kutatiza uthabiti Rwanda.

Katika mahojiano ya hivi karibuni na gazeti moja la Afrika Mashariki, Rais wa Rwanda Paul Kagame alinukuliwa akisema kuwa mgogoro kati ya nchi zao unaendelezwa kwa sababu Uganda imeamua kuamini uvumi unaosambazwa na raia wa Rwanda walioko Afrika Kusini badala ya kuamini kile ambacho serikali yake inaiambia.

Hatahivyo, Msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo amekanusha madai kwamba Uganda hutegemea uvumi katika kufuatilia masuala ya mahusiano yake na nchi zingine.

'Ni jambo la kuchekesha kwa yoyote kusema kwamba serikali ya Uganda, haina taasisi zake za kupata habari za kuchunguza badala ya kwenda na habari za uzushi. Hususan habari za Rwanda zilizojitokeza kutoka Afrika kusini au taifa lolote' amesema Opondo.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo amelezea kuwa marais wawili Museveni na Kagame hukutana mara kwa mara

'Kama ingelikuwa hivyo, serikali ya Uganda ingekuwa matatani na serikali zote duniani. Kwasababu katika mataifa haya, kuna watu walio na midomo mibaya au wanaozungumzia vibaya serikali ya Uganda au mataifa yao, hivyo serikali haisikizi habari zozote za tetesi kutoka taifa lolote ambalo linatofuatiana na taifa jingine, hilo halipo' ameongeza msemaji huyo wa serikali ya Uganda.

Madai ya kuwepo kwa mgogoro unaofukuta kati ya Uganda na Rwanda yamendelea kuripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

Safari hii mawaziri wa serikali ya Rwanda na hata rais mwenyewe wamenukuliwa wakielezea masikitiko yao kuhusu kuyumbayumba kwa mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

Upinzani: 'Mlio wa ngoma ya vita na wananchi hawajatayarishwa?'

Huku serikali Uganda ikiyakanusha hayo, Kinara wa upinzani bungeni Ibrahim Semujuu ameitaka serikali itoa ufafanuzi muafaka kuhusu suala hilo.

'Tungependa kufahamu kutoka kwa Museveni pamoja na makamanda wake kile kinachoendelea kati ya Uganda na Rwanda. Nimefuatilia mahojiano ya Paul Kagame, anasema hafahamu kwanini wanaongea tu bila ya vitendo.

'Sisi kama chama, tunawajibu wa kujua kiongozi wa taifa na makamanda wake, wanatoa sauti ya mlio wa ngoma ya vita na hawajatayarishwa wananchi wake kwa vita hivyo?' ameuliza kinara wa upinzani Semujju.

Msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo anaeleza kuwa marais wawili Museveni na Kagame hukutana mara kwa mara na iwapo kuna hoja zozote, wao huzisuluhisha.

'Bado tunathibitisha kwamba tuna uhusiano mzuri na serikali ya Rwanda na raia wa Rwanda. Walikutana katika mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, na nje ya kikao hicho walizungumza.

Na kama kuna matatizo kati ya serikali ya Uganda na Rwanda, nafikiri wameligusia.'

Hatua ya kuwafukuza wakuu wa kampuni ya mawasiliano ya MTN akiwemo raia mwanamke wa Rwanda kutoka Uganda kwa madai kuwa walihatarisha usalama wa nchi inaelezewa na Ibrahim Semujju kuwa miongoni mwa ishara kuwa kuna jambo.

Mara kwa mara jeshi la polisi la Uganda limekosolewa na raia wa Rwanda walioko nchini humo kuwanyanyasa baadhi wakikamatwa na kulazimishwa kurudi kwao.

Rais wa Rwanda aliliambia gazeti la Afrika mashariki kwamba juhudi za serikali yake kutatua tofauti zao na Uganda katika kipindi cha miaka miwili hazijafua dafu.

Chanzo cha picha, MICHELE SIBILONI

Walikoanzia Kagame na Museveni:

Rais Kagame, alipokea mafunzo ya kijeshi katika mataifa tofuati ikiwemo nchini Uganda na Tanzania yaliomfanya kuonekana kama mpanga njama mzuri wa kijeshi.

Ameishi kama mkimbizi katika nchi hiyo jirani Uganda kwa miaka mingi.

Yeye alikuwa mfuasi muasisi wa jeshi la waasi la rais Yoweri Museveni mnamo 1979.

Alikiongoza kitengo cha ujasusi, na kumsaidia Museveni kuingia madarakani mnamo 1986.

Lakini muungano huu uliingia dosari wakati wa vita vya Congo kati ya mwaka 1998 na 2003 wakati mataifa hayo mawili yalipounga mkono makundi hasimu ya waasi.

Hatahivyo, kadri muda ulivyosogea, mataifa hayo yalipatana taratibu.

Rwanda imekuwa ikiishutumu Uganda kwa kuyasaidia makundi yanayopingana na serikali yake, huku nayo Uganda imekuwa ikiwatuhumu baadhi nchini Rwanda kwa ujasusi.

Tuhuma ambazo pande zote mbili zinakana kuhusika nazo.

Wachambuzi wanataja kwamba kauli hizi sio nyepesi na pengine inaashiria kazi nzito iliopo.