Sanaa ya 'Art String' yamsukuma Veronica Kihampa kuachana na ajira

Art string
Maelezo ya picha,

Mchoro wa picha uliotumia misumari nyuzi na mbao

Sanaa ya mikono ya utengenezaji wa picha za mapambo kwa kutumia misumari nyuzi na mbao, ijulikanayo kama string art ni sanaa ambayo haijazoleka sana katika jamii nyingi nchini Tanzania na hata Afrika mashariki kwa ujumla.

Lakini Veronica Kihampa,23, ni msichana ambaye ameamua kujikita katika utengenezaji wa mapambo hayo imekuwa ajira mpya na kulazimika kuacha kazi yake ya kuajiriwa.

"Niliamua kuacha kazi ya kuajiriwa ili kujikita zaidi katika utengenezaji wa picha hizi za mapambo kwa kuwa zinanilipa zaidi kuliko kazi niliyokuwa nimeajiwa"

Maelezo ya picha,

Veronica akiandaa mchoro kabla ya kuanza kutengeneza

Msichana huyu anatengeneza picha hizi nyumbani kwao na akiita sehemu yake hiyo ya kazi kwa jina la Ms Craft.

Awali alikuwa ameajiriwa kwenye duka moja la kuoka na kuuza keki jijini Dar es Salaam.

Mjasiriamali huyo pia alishindwa kuendelea na masomo yake katika chuo cha ustawi wa jamii akiwa mwaka wa kwanza baada ya kukosa ada, alikuwa anasomea baishara ngazi ya shahada.

Vifaa anavyotumia kutengeneza picha hizo ni mbao ambazo huwa ananunua kisha kuzipiga msasa na kuziandaa kwa mchoro anaotaka kutengeneza kisha hugongelea misumari na baada ya hapo hufuma kwa nyuzi za rangi tofauti ili kuweza kupata picha za kuvutia .

Picha anazotengeneza zinatumika kama mapambo katika maofisi majumbani ila wengi wa wateja wake wananunua picha hizo kwa ajili ya kuwapa wengine zawadi.

Maelezo ya picha,

Mchoro wa kuvutia wa ramani ya Africa baada ya kumalizwa kutengenezwa na Veronica Kihampa

Veronica anaeleza kuwa licha ya kufanyia kazi zake nyumbani kwao, anatumia mitandao ya kijamii kuwafikia wateja wengi kwa wakati mmoja na wateja wamekuwa wanaongezea tofauti na awali alipoanza kazi hiyo.

Wanunuzi wakubwa wa bidhaa ya sanaa hii ni " Wanawake wengi ndio wanunuzi wa kazi zangu ambao hununua kwa ajili ya zawadi ila kwa upande wanaume ni wachache sana wanahesabika na walionunua wengi wanataka kwa ajili ya maofisini tofauti na wanawake wanaonunua kwa ajili ya zawadi"