Kuadimika kwa kondomu Njombe, Tanzania kwaleta hofu ya maambukizi ya Ukimwi

Kondomu

Chanzo cha picha, Getty Images

Mipira ya kiume ya kondomu nchini Tanzania imeadimika ama kupanda bei katika baadhi ya sehemu hususani mkoa wa Njombe ambao maambukizi ya Virusi vya Ukimwi yapo juu.

Hali hiyo imetokana na mabadiliko katika mifumo ya usambazaji wa mipira hiyo. Awali, serikali pamoja na baadhi ya mashirika binafsi nchini humo yalikuwa yakipata ruzuku kutoka kwa taasisi ya Afya ya Global Fund.

Lakini sasa, ruzuku hiyo wanapatiwa serikali pekee, hii inamaanisha Wizara ya Afya ya nchi hiyo ndiyo itakuwa inasimamia uingizwaji wa kondomu kwa mpango huo.

Naibu Waziri wa Afya Tanzania Dkt Faustine Ndugulile ameiambia BBC Swahili kuwa kwa sasa mfumo huo upo kwenye kipindi cha mpito na matokeo yake ni kuwa baadhi ya maeneo hususani mkoa wa Njombe yameathirika vibaya.

Hata hivyo amesema si kweli kuwa hakuna kabisa kondomu katika maeneo hayo.

"Bado kuna mashiika mengine ambayo si ya kiserikali yanaingiza komdomu kwa mifumo yao binafsi na kuna zile ambazo zinaingizwa kupitia wafanyabiashara.

Chanzo cha picha, iStock

"Kondomu zilizoadimika ni zile ambazo zilikuwa zikitolewa bure ama kwa bei nafuu. Na hili ni suala la mpito tu, karibuni mambo yatakuwa sawa kama awali."

Kutokana na uhaba huo, bei za kondomu mkoani humo zimepaa kwa kasi.

Gazeti la Mwananchi la Tanzania linaripoti kuwa bei ya pakiti iliyokuwa ikiuzwa kwa shilingi 5,000 ($2.14) sasa imefika 12,500 ($5.36).

Mwanaharakati wa kupambana na maambukizi mkoani humo Michael Uhahula ameiambia BBC kuwa bei za rejareja zimechupa kutoka wastani wa shilingi 500-1000 ($0.21-$0.43) mpaka shilingi 1,500-2,500 ($0.64-$1.7) kulingana na sampuli.

Njombe yaongoza kwa maambukizi

Wakati wastani wa kasi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa Tanzania inaripotiwa kuwa asilimia 4.5, kwa mkoa wa Njombe wastani wa maambukizi ni asilimia 14.

Mkoa huo ndio unaongoza kwa maambukizi Tanzania, na uhaba huo unaleta hofu ya tatizo kuongezeka.

Maelezo ya picha,

Mkoa wa Njombe unaongoza kwa kasi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi,Tanzania.

"Kwa sasa, bidhaa hii muhimu haipatikani katika yale maeneo ambayo yanauhitaji mkubwa kama vilabuni na vijijini. Serikali inabidi ichukue hatua za dharura ili kuokoa hali iliyopo huku," Uhalula ameiambia BBC.

Kwa mujibu wa Dkt Ndugulile, serikali inachukulia hali hiyo kwa uzito unaostahiki na tayari wameshaagiza kondomu za kutosha.

"Kwanza, sisi hii tunaichukulia kama chachu ya kuoneza kasi yetu, kutokana na hali ya maambukizi ya mkoa huo, tunafurahi kuona uhitaji wa kondomu Njombe ni mkubwa, na hivi karibuni mzunguko utakuwa kama awali."

Kwa mujibu wa Ndugulile, serikali inataraji kondomu milioni tisa zitaingia nchini mwishoni mwa mmwezi Februari na kondomu nyengine milioni 90 mwezi Machi.