Mahakama kuu Kenya yaahirisha uamuzi wa iwapo kuhalalisha au kuendelea kupinga mapenzi ya jinsia moja

Brian na Yvonne ni wanaharakati wa kutetea haki za jamii ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja
Maelezo ya picha,

Brian na Yvonne ni wanaharakati wa kutetea haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja

Mahakama ya Kenya leo imeahirisha uamuzi uliokuwa unatarajiwa kuhusu uhalali wa sheria inayoharamisha mapenzi kwa watu wa jinsia moja.

Kwa mujibu wa jaji katika mahakama hiyo hii leo asubuhi, kesi hiyo imebidi iahirishwe kutokana na kuzidi kwa majukumu.

Chini ya sheria za Kenya, mapenzi ya jinsia moja ni hatia iliyo na hukumu ya miaka 14 gerezani.

Nchini Kenya, kama ilivyo katika mataifa mengi barani Afrika, uhusiano wa jinsia moja haukubaliki kwa jamii.

Brian na Yvonne ni wanaharakati wa kutetea haki za jamii ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, pamoja na wale waliojibadilisha jinsia na hisia.

''Tunadharuliwa, tunakabiliwa na ghasia, tunaumia, tunateswa, tunakosewa. Tukienda kutafuta huduma za afya tunaangaliwa kwa dharau, tunatukanwa, tunatemewa mate, tunafanywa kama sisi sio Wakenya, na kama sisi sio Binaadamu, ni kama sisi ni viumbe wasiotoka katika dunia hii'.

Chini ya sheria za Kenya zilizoandikwa enzi za ukoloni, mapenzi ya jinsia moja yametambuliwa kama kitendo kisicho cha kawaida, na kuwekwa katika kitengo kimoja na hatia ya kufanya mapenzi na Wanyama.

Wanaharakati wanasema kwamba kuwepo kwa sheria hii kumezidisha ubaguzi, huku watu wakifurushwa kutoka nyumba walizokodisha, kunyimwa nafasi za kupata matibabu na pia kuhangaishwa na polisi, yote kwa sababu ya jinsia zao.

Aidha wanaharakati wanasema kutoelewa sheria hii kumechangia dhuluma za aina nyingi.

''Unapata, wakati mwingi mtu akisema kitu kibaya au kufanya kitu kibaya dhidi ya jamii yetu. Mtu anasema, hata Kenya hairuhusiwi, sheria inapinga, kwa sababu sio watu wengi wanaokwenda kwenye hicho kifungu cha sheria kuelewa inasema nini. Yeye amesikia tu sheria, inasema,' amefafanua Yvonne.

'Kwahivyo inawasukuma watu kuendelea kuwachukulia na kuwafanyia watu wa jamii hii vibaya. Kwasababu kuna hii fikra kwamba sheria imesema. Sasa ndio maana tumekwenda kotini hiyo sheria iondolewe kwanza, ndio sasa tuongee' ameongeza mwanaharakati huyo.

Katiba ya Kenya inasema nini?

Katiba ya Kenya inaonya dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote, ikiwemo ubaguzi wa kijinsia.

Wasemaji wa jamii hii wanahoji kuwa hata kama sheria hii haitaondosha kabisa ubaguzi, angalau wana matumaini ya kuwa itawanyang'anya polisi nguvu za kuwakamata kiholela.

Lakini wanaounga mkono sheria hii, wakiwemo baadhi ya makundi ya dini, wanasema kuwa kuondolewa kwa sharia hii huenda ikatoa fursa ya kuhalalisha ndoa kwa watu wa jinsia moja, ambayo kwa sasa haitambuliki kwenye katiba.

Mnamo 2016, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu limegundua kwamba wapenzi wengi wa jinsia moja wanaoishi nchini Kenya wanakabiliwa na 'wasiwasi wa usalama kila siku'.

Kumekuwepo na shinikizo kutoka mataifa mengi duniani kwa taifa la Kenya kuhalalisha mapenzi ya Jinsia moja.

Lakini wakenya wengi, akiwemo rais Uhuru Kenyatta , wanahoji kuwa taifa hili lina shida kubwa zaidi za kushughulikiwa, na zinazopaswa kupewa kipa umbele.

Je, wanahisi vipi juu ya wazo hili?

'Hata mimi nakubalina na hilo, lakini shida ni kwamba Wakenya wenzetu ndio wanaozidi kutudhulumu na kutunyanyasa. Sasa juu ya shida nyingine nchini Kenya, ni lazima tushughulikie pia unyanyapaa huu kutoka kwa Wakenya wenzetu.

'Kama tungekuwa tu Wakenya sisi wote tunakubaliana, basi tukabiliane na shida zetu kwa pamoja kama Wakenya. Tukubali utofuati wetu na tukabiliane na shida zetu kwa pamoja. Lakini sio kusema, nyinyi kwasababu ya hali zenu, tuwapige kwanza hawa, ndio tukabiliane na rushwa' amefafanua Yvonne.

Uamuzi uliopangiwa kutolewa leo ulikuwa umetarajiwa sana sio nchini Kenya tu, bali pia katika bara zima la Afrika.

Mapenzi ya jinsia moja ni hatia katika zaidi ya nusu ya mataifa ya bara la Afrika.