Burundi AMISOM: Burundi imetishia kuoyaondoa majeshi yake Somalia

Wanajeshi wa Amisom wamekuwa wakikabiliana na wapiganaji wa al-Shabab

Chanzo cha picha, BBC Sport

Maelezo ya picha,

Wanajeshi wa Amisom wamekuwa wakikabiliana na wapiganaji wa al-Shabab

Burundi imetishia kuondoa wanajeshi wake 5,000 nchini Somalia ambako wamekuwa wakihudumu chini ya kikosi cha kulinda amani cha Muungano wa Afrika, AMISOM kufikia mwisho wa mwezi huu.

Muungano wa Afrika umeitaka Burundi kuwaondoa wanajeshi 1000 kutoka kikosi cha AMISOM kufikia mwisho wa mwezi huu hatua ambayo serikali ya Burundi inapinga.

Waziri wa ulinzi Emmanuel Ntahomvukiye, amewaambia wabunge kuwa serikali tayari imetoa ilani kwa AU kuhusiana na suala hilo.

Mataifa matano ya Afrika yanachangia wanajeshi wao katika kikosi cha kulinda amani cha AMISOM nchini Somalia.

Japo kuna hofu kuwa taifa hilo la upembe wa Afrika bado linakabiliwa na tishio kutoka kwa kundi la Al Shabab.

Chini ya makubaliano ya umoja wa mataifa zaidi ya wanajeshi 20,000 wa kulinda amani wanatakiwa kuondoka kwa awamu ili kuipokeza majeshi ya Somalia usukani wa ulinzi wa taifa lao.

Chanzo cha picha, Reuters

Ufadhili umetajwa kuwa changamoto kubwa kwa vikosi vinavyolinda usalama nchini Somalia.

Kila mwezi zaidi ya wanajeshi 20,000 wanaohudumu chini ya jeshi la pamoja la muungano wa afrika AMISOM, wanalipwa zaidi ya dola elfu moja kila mmoja.

Mshahara wao umekuwa ukilipwa na Muungano wa Ulaya moja kwa moja kupitia mataifa yao kwa kutumia sarafu za kigeni.

Wanajeshi hao hata hivyo hulipwa mishahara yao kwa sarafu ya nyumbani.

Serikali ya Burundi haioni kwanini mpango wa sasa wa AU wa kupunguza wanajeshi katika kikosi hicho unalenga wanajeshi wake pekee.

Sio mara ya kwanza Burundi kutishia kuwatoa wanajeshi wao kutoka Amisom lakini hatua hii ya sasa huenda ikawa na athari kubwa.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza

Mwaka 2017 Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza alitangaza kuwa serikali yake itaishtaki Muungano wa Ulaya kuwa kuzuia mshahara wa vikosi vya Burundi vilivyoko nchini Somalia kwa karibu mwaka mmoja.

''Tatizo liliko kwa sasa ni kwamba kikosi cha Amisom hakina ufadhili iliyokuwa nao hapo awali baada ya Muungano wa Ulaya EU kujiondoa sasa mataifa ambayo yanachangi kikosi hicho yanalazimika kkugharamia uwepo wa majeshi yao'' anasema mtaalamu wa masuala ya usalama nchini Kenya George Musamali.

Bwana Msamali anasema Uganda pia ilitishia kuondoa wanajeshi wake sawa na Ethiopia ambayo iliondoa wanajeshi wake na kisha kisha kuwarejesha baadae.

Hatua hatua ya Burundi inaiacha Somalia katika hali tata hasa ikizingatiwa mzozo wa kidiplomasia uliyoibuka hivi karibuni kati yake na Kenya licha ya kuwa imekuwa mshirika wake mkuu katika juhudi za kupambana na wanamgambo wa Al-shabab.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Wapiganaji wa Al shabab

''Somalia haina budi kupambana na hali yao kwasababu hawataishi kwa kutegemea mataifa ya kigeni kuleta majeshi yao na kugharamia ili hali vita dhidi ya Alshabab havionekani kufikia kikomo'' anasema George Msamali.

Nini kifanyike kutatua mvutano huu?

Muungano wa Afrika umeshauriwa kuepuka na mazoea ya kutegemea ufadhili wa kigeni kutatua changamoto zinazoikabili Somalia.

Umoja huo umeshauriwa kukaa meza moja na mataifa wanachama wake kujadili kwa kina hatua zitakazochukuliwa kutatua tatizo la ufadhili katika kikosi cha AMISOM na pia kutafuta suluhicho la kudumu kwa masuala ya usalama nchini Somalia.