Upinzani Tanzania: Chadema chaanza harakati za kuachiliwa kwa Mbunge Halima Mdee

Mbunge wa Kawe Halima Mdee

Chanzo cha picha, Mdee/ facebook

Chama cha Chadema kimeamrisha idara yake ya sheria kuanzisha mikakati ya kuhakikisha kuwa kuwa mbunge wa Kawe Halima Mdee anaanchiliwa huru.

Kulingana na taarifa iliotolewa siku ya Jumamosi ,Februari 23, na chama hicho inasema kuwa mbunge huyo amekataliwa kuachiliwa kwa dhamana baada ya saa kadhaa za kuzuiliwa na kuhojiwa.

Mawakili pia wameamrishwa kuiomba mahakama ya juu kuwaita maafisa wa polisi waliomnyima dhamana mbunge huyo.

Vitengo vya usalama pia vimekumbushwa kutekeleza majukumu yao kulingana na katiba na sheria zinazotawala taifa hilo, ilisema taarifa.

Taarifa hiyo iliongezea kuwa dhamana hiyo ilikuwa haki iliotolewa na sheria na sio malengo ya mtu binafsi.

''Maafisa wa polisi wanakumbushwa kwamba kukandamiza ama kumnyima mtu dhamana ni miongoni mwa mambo ambayo yanafaa kupingwa na kushutumiwa na wanaharakati wa haki za kibinaadamu nchini humo''.

Chanzo cha picha, Chadema Media

Kwa nini alikamatwa

Maafisa wa Polisi mjini Dar es Salaam walimkamata mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuhusiana na tuhuma za kutoa kauli ya kumkosea heshima Rais Magufuli.

Kamanda wa Polisi wa Kanda maalum Dar es Salam Lazaro Mambosasa amesema Mwanasiasa huyo amekamatwa na si kuitwa kuhojiwa anavyodai wakili wake Hekima Mwasipu.

Bwana Mwasipu anasema Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema, amehojiwa kwa muda wa saa mbili na kunyimwa dhamana.

"Polisi wamemhoji kwa masaa mawili kutokana na kauli aliyoitoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Mikocheni Februari 21, 2018," amesema wakili Hekima.

Halima Mdee aliandika kupitia Mtandao wa Twitter kuwa ameitwa na polisi na wala hajui ameitiwa nini.

Ahojiwa na polisi

Mdee ambaye alifika kituoni hapo saa tatu asubuhi alianza na kuhojiwa saa kadhaa baadaye na hatimaye kuzuiliwa.

Haijabainika nini kitakachofuata baada ya hatua hiyo ya kukamatwa kwake.

Huku hayo yakijiri Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania cha Chadema kimelaani hatua ya Polisi kumkamata mbunge wake.

Taarifa ya iliyotolewa mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa chama hicho Tumaini Makene imesema kuwa chama imewaagiza wanasheria wake kuomba Mdee afikishwe mahakamani au aachiliwe huru siku ya Jumatatu.

Kupitia taarifa hiyo Chadema pia kimelaani na kukemea kitendo hicho cha polisi ambacho inadai ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Chama hicho kinadai kuwa huo ni mwendelezo wa vitendo vya polisi maeneo mbalimbali nchini,kuhangaisha wafuasi, wanachama na viongozi wa Chadema kinyume na taratibu za sheria za nchi.