Kim Jong-un aondoka kwa treni kuelekea Vietnam ili kukutana na Trump Jumatano

Treni inayoaminika kumbeba Kim Jong Un ikiwa imewasili Beijing

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Treni inayoaminika kumbeba Kim Jong Un

Kiongozi wa Korea Kaskazini,Kim Jong-un ameondoka kuelekea Hanoi kwa Treni kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Aliwasili katika mji wa mpaka wa China Dandong siku ya Jumamosi.

Mkutano kati ya Marekani na Korea Kaskazini unatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano na Alhamisi mji mkuu wa Vietnam.

Mkutano huu unakuja baada ya mkutano wa kwanza wa kihistoria mwaka jana nchini Singapore.Macho yote yatakua yakitazama kama kuna hatua yeyote iliyopigwa tangu wakati huo kuhusu kuteketeza silaha za nuklia.

Kim Jong-un amesafiri na dada yake Kim Yo Jong na mmoja kati ya washauri wake muhimu, Jenerali wa zamani Kim Yong Chol.

Kwa nini wanakutana tena?

''Tulipendana,'' Trump aliuambia mkutano mwezi Septemba mwaka jana kuhusu Kim.'' aliniandikia barua nzuri.''

Pamoja na maneno hayo mazuri, miezi kadhaa baada ya mkutano wa mwezi Juni mwaka jana ilitawaliwa na kauli za msuguano na mahusiano yasiyoridhisha.

Mkutano huu unatarajiwa kuendeleza misingi ya mkutano uliopita kuhusu masuala ya silaha za nuklia, ambapo wataalamu wanasema jitihada zilizofanyika ni kidogo.

Siku chache kabla ya mkutano wa Hanoi, ajenda za mkutano hazijawekwa wazi.

Ni mafanikio gani yaliyopatikana baada ya mkutano wa awali?

Mkutano wa mwezi Juni nchini Singapore, kati ya viongozi hao ulikua mkutano wa kihistoria.

Hata hivyo,makubaliano waliyoyatia saini hayakuwa dhahiri na hatua kidogo zimechukuliwa kuhusu lengo la kukomesha silaha za nuklia.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Trump na Kim wakiwa wameshikana mkono

Donald Trump aliahidi kukomesha vitendo vya majaribio ya silaha za nuklia ikishirikiana na Korea Kusini ambavyo vimeighadhabisha Korea Kaskazini, lakini miezi imepita sasa wengi wakihoji yeye amepata nini kwa upande wake?

Matarajio ya mkutano huu

Wakati huu viongozi hawa watakuwa makini kuhakikisha kuwa wanapata majibu yatakayoonyesha ishara ya kufikia malengo yao au angalau kupata picha ya njia ya kuyafikia.

Wachambuzi wa mambo watakuwa wakifuatilia kwa karibu wakati viongozi hao wakijiandaa kwa mkutano huo.

Msimamo wa Washington awali ni kuhakikisha kuwa Korea Kaskazini inateketeza silaha zake za nuklia kabla ya kupata nafuu ya vikwazo.

Lakini siku chache zilizopita, rais Trump alisema ''hana haraka'' kushinikiza hilo.

Kwa nini mkutano unafanyika Vietnam?

Chanzo cha picha, KCNA

Maelezo ya picha,

Kim Jong-un akiwa ziarani Pyongyang (2017)

Mkutano huu unafanyika Vietnam kwa sababu nyingi.Ina mahusiano mazuri ya kidiplomasia na Marekani na Korea Kaskazini,ingawa iliwahi kuwa na uadui na Marekani hivyo inaweza kuwa kama mfano wa nchi mbili zinazofanya kazi pamoja na kuweka kando tofauti zao.