Raia wa Senegal wapiga kura leo kumchagua Rais wa nchi hiyo

Watu wakiwa kwenye mstari wakisubiri kupiga kura leo

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Zaidi ya watu milioni sita wamejiandikisha kupiga kura

Wapiga kura nchini Senegal wanapiga kura katika uchaguzi wa urais nchini humo.

Rais wa Senegal Macky Sall anawania muhula wa pili huku akikabiliwa na wapinzani wanne.

Tangu aingie madarakani, Bwana Sall alijikita kwenye uboreshaji wa miundo mbinu, lakini wakosoaji wake wanasema hajawajibika vya kutosha kuhakikisha hali za raia wa kawaida nchini humo zinaimarika.

Pia anashutumiwa kuwazuia wapinzani wake wa kisiasa kuwania uongozi.

Mwezi uliopita, wapinzani maarufu nchini humo walizuiwa kuwania uongozi kwa sababu ya shutuma za rushwa walizokuwa wakikabiliwa nazo.

Khalifa Sall, meya maarufu wa Dakar na Karim Wade, mtoto wa rais wa zamani, walizuiwa kwa sababu ya kesi za rushwa walizokabiliwa nazo.

kutokana na uamuzi huo, si chama cha Socialist wala Democratic, vinavyowania nafasi ya urais.

Sheria ilipitishwa mwaka 2018 ikiwataka wanaowania urais kuwa na idadi fulani ya sahihi kutoka kwa wapiga kura ili kuweza kuwania nafasi hiyo.

hatimaye, wagombea watano pelee wamehalalishwa kuwania tofauti na wagombea 12 kwenye uchaguzi uliopita.

Bwana Sall amekua akijisifu kuwa amesaidia kupandisha uchumi kwa zaidi ya 6% kwa mwaka.

Zaidi ya watu milioni 6.6 walijiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi huu.

Ikiwa hakutakuwa atakayepata kura zaidi ya mwezie nchi itaingia kwenye duru la pili tarehe 24 mwezi Machi.