Mahakama: Waanzilishi wa jamiiForum wapatikana na kesi ya kujibu Tanzania

Mwanzilishi mwenza wa mtandao wa wa Jamii Forums Maxence Melo

Chanzo cha picha, MAXENCE MELO/FACEBOOK

Hakimu mkaazi wa mahakama ya kisutu ameamuru kwamba waanzilishi wa mtandao wa jamiiForum Maxence Mello na Micke William Mushi wana kesi ya kujibu.

Kulingana na mtandao wa The Citizen nchini Tanzania, hakimu mkaazi Thomas Simba amesema kuwa wawili hao walifaa kujitetea katika kesi ambayo wanatuhumiwa kuzuia uchunguzi baada ya kutotoa ,maelezo ya watu wanaochapisha habari katika mtandao huo kwa polisi.

''Nawataka watuhumiwa kutoa mashahidi zaidi ili kuiwezesha mahakama hii kukamilisha kesi hii kabla ya mwisho wa mwezi Machi'', alisema.

Awali ,wakili wa serikali Elia Athanas alikuwa ameuliza mahakama hiyo kuamua iwapo watuhumiwa hao wana kesi ya kujibu au la.

''Watuhumiwa wote wawili wamehudhuria kikao hiki na upande wa mashtaka unasubiri uamuzi'',alisema Athanas.

Mashahidi

Kulingana na mtandao huo ,hakimu huyo alisema kuwa upande wa mashtaka uliwaleta mashahidi watatu na ushahidi mmoja kuthibitisha mashtaka dhidi ya waanzilishi hao wa mtandao wa jamii Forum.

''Baada ya kusikiza ushahidi uliotolewa, mahakama imewapata watuhumiwa wote na kesi ya kujibu , hivyobasi watalazimika kujitetea'', alisema.

Wakili wa watuhumiwa Nashon Mkungu amesema kuwa watuhumiwa huenda wakatoa ushahidi kupitia kiapo walichokula na kwamba watawasilisha mashaihidi watano.

''Tunatumai kuwaleta mashahidi watano, hivyobasi tunataka tarehe kuwekwa ili tuanze kutoa ushahidi'', alisema wakili Mkungu.

Hakimu simba alitoa tarehe ya Machi 14 na 19 , mwaka huu kama siku za watuhumiwa kutoa ushahidi wao.

Uamuzi huo unajiri baada ya upande wa mashtaka kufunga ushaihidi wake , ambao uliwaleta mashahidi watatu , akiwemo afisa mkuu wa jinai katika eneo maalum la Dar es salaam SSP Ramadhan Kindai.

Mnamo mwezi Juni 2018 Jamii Forums ulikuwa kuwa miongoni mwa watoaji huduma za maudhui mtandaoni ambao waliathiriwa na kuanza kutekelezwa kwa sheria mpya za mtandaoni.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania iliwataka wahudumu wote ambao hawana leseni za kuchapisha mitandaoni kukoma kutoa huduma .

Mamlaka hiyo iliwataka wahudumu hao kuhakikisha wamejipatia leseni la sivyo wachukuliwe hatua.

TCRA ilisema wanaoathirika ni wamiliki wote wa blogu, majukwaa ya mitandaoni, redio na televisheni.

Wameandika kwenye mtandao wao:

"Kutokana na notisi iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) leo Juni 10, 2018 inayotoa muda mfupi wa kututaka kusitisha utoaji huduma mara kabla ya Juni 11, 2018, tunalazimika kutii mamlaka na hivyo huduma hii haitapatikana kwa muda wakati tukifanya jitihada za kuhakikisha huduma inarejea.

"Kwa wateja wetu walio nchi nyingine, huduma hii itarejea mapema zaidi lakini kwa walio Tanzania kurejea kwa huduma kutategemeana na matokeo ya hatma ya jitihada za wawakilishi wetu walio Tanzania.

"Tunasikitika kuwa tunalazimika kufikia hatua hii ghafla lakini ni matumaini yetu kuwa wateja wetu mtaendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki."

Ujumbe wa mwisho kutoka kwa jukwaa hilo kwenye Twitter ulipakiwa usiku wa manane, na ulikuwa wa kutangaza taarifa hiyo kutoka kwa TCRA.

Mwanablogu Carol Ndosi ni miongoni mwa walioathiriwa na kuanza kutekelezwa kwa sheria hizo, mwanzoni aliomba ufafanuzi kuhusu wanaotakiwa kusitisha kuchapisha taarifa mtandaoni.

Baadaye, aliandika kwamba amelazimika kusitisha uandishi wa taarifa mtandaoni.

Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe ni miongoni mwa walioshangazwa na hatua ya sheria hiyo kuanza kutekelezwa na Jamii Forums kulazimika kufunga huduma zao kwa muda.

Wamiliki wa huduma za mitandaoni Tanzania walikuwa wamepewa muda wa wiki mbili kujisajili baada ya serikali kushinda kesi iliofunguliwa na wadau wa habari kupinga kanuni za maudhui mitandaoni 2018.

Wanablogu wataopatikana na hatia ya kutoheshimu sheria hizo mpya watakabiliwa na faini ya hadi milioni 5 ama kifungo kisichopungua miezi 12 ama zote mbili kulingana na sheria hizo mpya, ilisema taarifa hiyo.

Mike Mushi, mwanzilishi mwenza wa Jamii Forums alikuwa awali ameambia BBC kwamba kanuni hizo, ambazo zinawataka wachapishaji wa taarifa zenye maudhui mtandaoni kuhifadhi maelezo ya wachangiaji kwa miezi 12 huenda zikaathiri mtandao wa Jamii Forums.

"Sheria hizi zinaenda kinyume na jinsi sisi huendesha shughuli zetu. Huwa twawaruhusu watumiaji wetu kuandika ujumbe bila majina yao kutambulishwa, hivyo itatulazimu kufikiria kwa kina iwapo tutaweza kuendeleza kuendesha shughuli zetu."

Alisema mtandao huo kufikia Aprili ulikuwa na watumiaji 3.7 milioni kwa mwezi na walikuwa wanapokea ujumbe takriban 20,000 kila siku.

Maelezo ya picha,

Wanablogu

Rais Magufuli alitoa agizo la kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote atakayechapisha habari za uongozi kuhusu serikali katika mitandao ya kijamii.

Idadi ya watumiaji wa mitandao nchini Tanzania ilipanda hadi asilimia 16 (watu 23 milioni) mwaka 2017. Hiyo ni sawa na asilimia 44 ya raia wa Tanzania.

Wengi hutumia simu kupata huduma za mtandao.