Saudia yamtangaza mwanamke wa kwanza kuwa balozi taifa la kigeni

Bintimfalme Rima mwana wa Bandar al-Saud 2018

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Bintimfalme Rima anafuata nyayo za babake wa kambo ambaye alishikilia wadhfa huo hadi mwaka 2005

Saudi Arabia imetangaza kwamba binti mfalme Rima bint Bandar al-Saud atakuwa balozi wake nchini Marekani -akiwa mwanamke wa kwanza kuwa balozi wa ufalme huo.

Uteuzi wake ulifanywa hadharani kwa amri ya ufalme huo siku ya Jumamosi. Bintimfalme Rima aliishi Washington DC nchini Marekani katika kipindi kirefu cha utoto wake.

Anachukua wadhfa huo wakati mgumu , huku Saudia ikijaribu kukabiliana na hisia za jamii ya kimataifa kuhusu mauji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.

Baada ya kutoa taarifa zenye utata , ufalme huo baadaye ulikiri kwamba Khasshoghi ambaye alikuwa mfanyikazi wa ufalme huo, aliuawa baada ya kuingia ubalozi wa taifa hilo uliopo Instanbul mwaka uliopita.

Kabla ya kifo chake mwandishi huyo alikuwa akiliandikia gazeti la The Washington Post ambapo mara kwa mara alikuwa akiikosoa serikali ya Saudia.

Saudia imekana kwamba mwanamfalme Mohammed Bin Salman alihusika katika kifo chake madai ambayo idara ya ujasusi nchini Marekani inatiliashaka.

Wabunge nchini Marekani wamejaribu kuishinikiza Ikulu ya Whitehouse kuchunguza kisa hicho.

Hivi majuzi wanachama wa bunge la Congress walichunguza uhusiano kati ya Saudia na Marekani katika maeneo mengine, ikiwemo kuhusu teknolojia ya Kinyuklia pamoja na vita nchini Yemen.

Afuata nyayo za babake

Binti mfalme Rima atachukua jukumu lote la nduguye mdogo mwanamfalme , mwanamfalme Khalid bin Salman, ambaye ameteuliwa kuwa naibu waziri wa ulinzi nchini humo

Chanzo cha picha, Handout via Getty

Maelezo ya picha,

Rais Trump ameshutumiwa kuhusiana na uhusiano wake wa karibu na mwanamfalme huyo wa Saudia anayehusishwa na kifo cha Khasshogi

Anafuata nyayo za babake Bandar bin Sultan al-Saud ambaye alishikilia wadhfa huo wa ubalozi wa Marekani hadi 2005.

Kwa sababu ya jukumu lake , alitumia kipindi kirefu cha utoto wake nchini Marekani.

Anashkilia shahada ya sanaa ya masomo ya kumbukumbu kutoka chuo kikuu cha George Washington University.

Tangu kurudi kwake mjini Riyadh 2005, binti mfalme Rima amefanya kazi katika nyanja za kibinafsi na zile za umma.

Ameshikilia nyadhfa tofauti za kibiashara , ikiwemo ile ya afisa mtendaji mkuu katika kampuni ya Harvey Nichols Riyadh.

Bintimfalme huyo anaonekana kuwa mpiganiaji mkuu wa haki za kibinaadamu za wanawake katika taifa ambalo linakosolewa kwa rekodi yake ya usawa wa kijinsia.

Hivi majuzi alikuwa akifanya kazi katika halmashauri ya michezo nchini Saudia akiwa na lengo la kuimarisha idadi ya wanawake wanaoshiriki katika michezo.

Pia anajulikana kwa kazi yake nzuri katika kampeni dhidi ya saratani ya matiti.