Ndege ya Bangladesh yatua kwa dharura mji wa Chittagong

Ramani ya Bangladesh

Ndege iliyokuwa inafanya safari kutoka mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka kuelekea Dubai, ililazimika kutua kwa dharura baada ya kutokea jaribio la kuteka nyara ndege, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.

Ndege ya shirika la Binman, ikiwa na abiria 142, ilizungukwa na vikosi vya usalama katika uwanja wa ndege wa mji wa pwani wa Chittagong.

Abiria wa ndege BG 147 walitoka ndani ya ndege hiyo wakiwa salama, ripoti zilieleza zikinukuu polisi.

Mtu mmoja aliyekisiwa kujaribu kuvamia chumba cha rubani alikamatwa, Shirika la habari la Ufaransa limeeleza.

Ndege hiyo iliwekwa kwenye uangalizi mara moja ilipotua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Shah Amanat wakati polisi wakizungumza na mshukiwa huyo.

Picha zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha watu wakiwa katika makundi makundi huku ndege aina ya Boeing 737 ikionekana kwa nyuma.

Haijafahamika kwa nini mshukiwa huyo anayeaminika kuwa na umri wa miaka 25, alijaribu kuteka nyara ndege.