Shilingi Tanzania: 'Wakati mwingine tunalazimika kununua bidhaa nje ya nchi'

shilingi

Chanzo cha picha, Patrick AVENTURIER

Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani imezidi kushuka na kufikia kiwango cha chini zaidi katika miaka mitatu iliyopita.

Katika baadhi ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni mjini Dar es Salaam, dola moja ya Marekani inauzwa kwa kati ya shilingi 2,415 hadi na shilingi 2418 ya Tanzania.

Bei ambayo inatajwa kuwa kiwango cha chini zaidi kuwahi kutokea.

Siku chache ziliizopita benk kuu ya Tanzania ilikiri kushuka kwa thamani ya shilingi ikitaja sababu kama kuchelewa kwa ununuzi ya korosho, kutokuwa msimu wa watalii na kupungua kwa fedha za wahisani.

Hali hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wananchi, huku baadhi ya wafanyabiashara wakiona ni fursa ya kujizolea faida.

Bi Grace Silas, mmoja wa wafanyibiashara katika jiji la Dar es Salaam anasema pesa zeke zimekosa thamani.

'Tunapotaka kubadilisha shilingi kwenda kwa Dola inakuwa ni ndogo kiasi ya kwamba tunashindwa kununua bidhaa''

Maelezo ya picha,

Noti za Tanzania

Anasema wakati mwingine wanalazimika kwenda kununua bidahaa nje ya nchi hali ambayo inawapatia changamoto kufanya biashara.Lakini kwa wafanyibiashara ambao wanatumia dola moja kwa moja kutoka nje kufanya biashara yao hawajaathiriwa na kushuka huku kwa thamani ya shilingi.

Saadi Jaffer Shaaban ameiambia BBC kuwa kushuka kwa thamani ya shilingi kunampatia faida kwasababu anapokea fedha za kigeni zinazokuja kama dola ambazo anafanyia biashara.

Nini kinaiporomosha thamani ya shingi ya Tanzania kwa kasi inayoelezwa?

Mwanauchumi Dkt Lenny Kasoga kutoka chuo cha Mwalimu Nyerere anasema kumekuepo na kuingilia soko la fedha kwa namna fulani.

''Benki kuu ambazo ndizo mhimili wa fedha za kigeni ukiondoa benki kuu yenyewe na hali kadhalika tatizo lililojitokeza katika uuzaji wa zao la korosho ndio chanzo kuu ya kuporomoka huku kwa shilingi''

Chanzo cha picha, ISSOUF SANOGO

Maelezo ya picha,

Wakulima wa korosho wamekuwa wakikumbwa na changamoto mara kadhaa

Dkt Kasoga ameongeza kuwa zao la korosho limekuwa likichangia kwa wingi fedha za kigeni lakini upande wa uchimbaji na kadhalika watu wamekuwa na wasiwasi kidogo.

''Mmzunguko wa hela kwa ujumla umekuwa sio mkubwa sana''

Nini kifanyike kwa haraka kuinusuri hali hii?

Wataalamu wa kiuchumi wamekuwa wakijikuna vichwa kutafuta njia ya haraka ya kuleta uwiano mzuri wa thamani ya shilingi na dola.

Lakini Dkt Kasoga anasema suluhisho la haraka lipo kwenye uzalishaji kwa maaana ya kwamba mzalishaji awezeshwe kuzalisha kwa haraka zaidi.

''Thamani ya fedha inategemea uzalishaji'' alisema.

Mwezi wa Novemba mwaka uliyopita Benki Kuu ya Tanzania ilizipiga marufuku benki tano za kuendesha biashara ya sarafu za kigeni kwa muda wa mwezi mmoja kwa kukiuka sheria ya biashara hiyo.

Hatua hiyo ilitokana na ukaguzi wa ghafla kwenye maduka ya kubadilisha fedha za kigeni katika mji wa Arusha ambao ni kituo cha utalii na bishara ya madini.