Wanawake wanoalazimishwa kuamini makosa ni yao wanapobakwa

Kichwa cha msichana aliyebakwa na kaka yake
Image caption Mwanamke aliyebakwa na kaka yake, anasema amekuwa akiishi na maumivu ya kimwili na kisaikolojia

Wakiishi katika maeneo tulivu ya wilaya ya Megenagna mjini Addis Ababa, wasichana 7 au 8 wanaonekana wakiondoka kwenye makazi yaliyofungwa wakiwa wamewabeba watoto wachanga.

Ingawa walikuwa na watoto wachanga migongoni mwao, miongoni mwao hakuna yeyote ambaye ana umri wa kujifungua, jambo ambalo lingemfanya yeyote kuwa na shauku ya kujua ni nini walikuwa wanaongea kati yao.

Tulikwenda kuzungumza nao kwenye makazi.

Ana umri wa miaka 23. Ni vigumu kumtambua ni nani hasa kwa kumtazama. Ni mpole. Alipokuja kwenye makazi haya, miaka iliyopita, hakuja kutafuta kazi.

Bali kutafuta maficho dhidi ya maumivu ya mwili na ya kisaikolojia aliyoyapitia baada ya kubakwa na kaka yake.

Anakumbuka kuwa alikua ameanza kuwa na uoga wa watu baada ya magumu aliyoyapitia na kwamba asingeliweza kumtazama wala kuongea na mtu yoyote.

"Nilikuwa na maisha magumu na ya huzuni " anasema huku akikumbuka kipindi kilichopita.

Licha ya kwamba maumivu yake yalikuwa mazito anashukuru walau anajihisi walau anaweza kuendelea kuishi, anasema kwamba kutembea akitizama mbele wakati mwingine alihisi kana kwamba wakati mwingine haiwezekani.

Nyumba iliyompatia hifadhi baada ya tukio la kubakwa , 'Refuge for Women and Children' ndiko anakofanya kazi.

Huwashirikisha watu wengine habari yake ya maumivu, kwani anaamini kuwa kwa kufanya hivyo itasaidia kama mfano wa kuwanusuru wasichana wanaoweza kukabiliana na unyanyasaji wa kingono.

Kaka yake mkubwa ambaye alimpeleka mjini na kumuahidi kuwa atampleka shule alikuwa polisi. Alikuwa na umri wa miaka 16 wakati huo na wote waliishi kwenye nyumba moja ambayo ilikodishwa na kaka yake.

"Kwasababu nilikuwa mdogo, sikujua mengi na sikuweza hata kuongea wazi. Nilipokuwa nikiwaona watu, nilifikiri wangenidhuru pia", alielezea masaibu ya kisaikolojia aliyoyapitia.

Alikuwa akifikiria kwamba watu watagundua siri yake kwa kumtizama tu. Kwa hiyo taratibu akaacha kwenda shule.

Katika kipindi chote cha miaka 5 walichoishi pamoja, kaka yake alikuwa akimbaka. Katika kipindi hicho alipata uzauzito na kutoa mimba mara kadhaa.

Vitisho kutoka kwa kaka yake, umri mdogo na maumivu havikumuwezesha kuongea neno hata moja juu ya hili kwa yeyote, anasema.

Hata hivyo, anaeleza kwamba siku walipohamia nyumba nyingine alipata fursa aliyokuwa akiitaka.

Muda mfupi baada ya kuhamia kwenye nyumba yao mpya, mwenye nyumba aligundua namna alivyokuwa hapendi kuongea na akamuuliza "Ni kwanini wewe ni muoga sana wa kuwasogelea watu? Wewe ni ndugu yake?"

Maswali yote yalikuwa ni magumu kwake kuyajibu.

Kwasababu alikuwa anatafuta njia za kutoroka ili kulinda utu wake hakutaka kumdanganya mwanamke , lakini kumuambia ukweli lilikuwa ni tatizo jingine lililomuelemea.

Baada ya kufikiria na kuupiga moyo konde alipata nguvu ya kumueleza mwenye nyumba. Baada ya kusikia habari yake mwenye nyumba ambaye alishitushwa na aliyoyasikia kutoka kwa binti huyo alimpeleka mara moja kwenye kituo cha karibu cha polisi.

Baada ya kuhojiwa katika kituo cha polisi alichukuliwa kwenye nyumba ambako wanawake wenye matatizo kama yake hupelekwa na kupewa mahala salama na usaidi wa kisheria.

Haki miliki ya picha ZELALEM ABERA (AWSAD)
Image caption Msichana aliyebakwa an kaka yake anasema jamii huwalaumu na kuwashutumu wanawake kwa ubakaji wanaofanyiwa

Kesi ilipofika mahakamani, familia ambayo ilifahamishwa kuhusu hali ya mambo walimgeuka " Hawezi kufanya jambo kama hilo, anaongea hivi kwasababu ni mtoto" walisema, hawakumuamini .

"Kila mtu katika familia yangu, isipokuwa mama yangu walikasirishwa sana na mimi " alieleza namna alivyogeuka na kuwa mwenye makosa ili hali akiwa yeye ndie muathiriwa.

Pia anasema kuwa kutokana na kwamba kawaida kituo vcha polisi hakipokei wanawake wenye matatizo kama yake, ni jambo lililomuongezea uwoga.

Anasema hawakuwa watu wa kumsikiliza na bila huruma walimuuliza maswali mabaya "Ulikuwa unafanya nini mpaka leo hii" wakimaanisha kuwa hakujitokeza mapema vya kutosha.

Hii ndio hali inayowakumba wanawake wengi. Wengi wanalazimishwa na jamii kuamini kuwa ni makosa yao. Watu wanaowazingira huwalaumu kwa mambo waliyofanya, mambo ambayo wangepaswa kufanya na mengine mengi, hivyo kuwalazimisha wengi kuendelea kujificha na kutosikika.

Katika hifadhi alipata maficho ambayo kwa sasa yamekuwa mahala pake pa kazi, na sasa amekutana na wanawake ambao waliwahi kubakwa na kaka zao, baba zao n ahata babu zao. Anaeleza kuwa wote walilaumiwa na jamii kwa kuwa chanzo cha ubakaji wao.

"Sifahamu mengi juu ya mfumo wa sheria. Lakini kwa yale niliyoyashuhudia, naweza kusema mfumo wa sheria ni mbaya "Anasema.

Mara nyingi wabakaji hutembea huru. Anasema tangu alipompeleka kaka yake mahakamani hakuna matokeo yoyote aliyoyapata kutokana na kesi na kaka yake anatembea huru.

" Nilipata maumivu makali sana na nikasimama mahakamani bila mafanikio. Afadhali nisizungumzie hili " aliongeza.

"Tunahitaji kuwa tayari kusaidiwa"

Kutokana na uaviaji mimba wa mara nyingi alioupitia alihitaji kupitia matibabu mbali mbali.

Baada ya haya yote "niliumia zaidi kisaikolojia. Hasa kwa namna familia yangu ilivyopokea taarifa ya kubakwa kwangu iliniuma sana" anasema.

Alipokuwa nyumbani, hakuweza kula wala kumuamini yeyote aliyekuwa karibu nae. Alikuwa na ndoto moja tu na ilikuwa ni ya kujiua na kujimalizia maumivu yote mara mara moja .

Amesema aliweza kuyashinda majaribu kwa msaada wa kufuatiliwa kwa karibu kisaikolojia.

Alipopata tena matumaini alianza kufanya masomo mbali mbali.

Makazi hayakumpatia tu ujuzi mbali mbali ili kuwezesha kuwa mtu anayejitegemea tu, bali yalimuwezesha kujiamini kupitia mafunzo ya Taekwondo ambayo pia yalimnufaisha.

Wakati watu wanapoumizwa hawahitaji mengi. Mara nyingi huwa hawataki kusikia wala kuwa tayari kuelewa chochote "licha ya kwamba kuna watu wengi walio tayali kutoa msaada wao, tunahitaji kuwa tayari kusaidiwa" anasema.

Ili kuondoka katika maumivu ya kimwili na kisaikolojia anasema alipata nguvu mwenyewe "Nilijiamini mwenyewe na niliamini ninaweza kujitatulia mwenyewe tatizo la maisha yangu yaliyotawaliwa na huzuni ."

Anasema kwamba licha ya kwamba wanawake wengi hawazungumzi wazi, anadhani wameweza kukabiliana na mambo mengi mabaya kuliko aliyoyapitia. Anaongeza kwamba anaamini kuwa kama jamii isingewapuuza wanawake hawa wengi wangejifunza kutokana na uzoefu wa aina hiyo.

"Tunapowaona wanawake wamevaa vitambaa na kutembea kana kwamba uzito wa dunia uko kwenye mabega yao, ninadhani pia wanaishi maisha yangu" kwa hiyo anasema huwa anawafuata na kuongea nao , kuwasikilizana kuwakumbatia.

Anasema anaamini kwamba jamii inahitaji kujifunza kuwahusu wanawake na masaibu wanayoyapitia ili kuwasaidia na kuwasaidia wanawake ambao wamejipata katika hali kama yake. Anaongeza kuwa kwasababu hii itawezesha kuzuwia mashambulio sawa na hayo.

Familia zinapaswa kufahamu kuwa mavazi, chakula na masomo ambayo watoto wao wanapokea havitoshi, anasema wanahitaji kutambua kuwa wanaweza kuwa katika hali ya hatari kokote wanapoenda.

"Ni nani angependa kuwa nami sasa?"

Makazi yanajitahidi kufanya kazi na wanawake waliopitia hali sawa na yangu, wanaamini kwamba hawatakiwi na jamii na mara nyingine hupanga kujiua. Makazi yamekuwa yakiwasaidia wanawake kisheria na kisaikolojia kwa miaka 15 sasa.

Maria Munir, muasisi wa makazi hayo alililieleza jarida la 'Temsalet Gets' nchini humo kwamba hakuna chochote kinachompatia furaha kuliko kuwaona wanawake ambao awali walitaka kujiua wakifanya vizuri shuleni na hata kitaaluma.

Makazi hayo yameweza kuwawezesha wanawake kuwa Wahandisi, Viongozi na katika Nyanja nyingine kupitia mafunzo wanayopata mjini Addis Ababa, Dessie na vituo vingine. Mwanamke mdogo aliyetushirikisha habari yake kwa sasa ni mkufunzi na anacheo cha meneja.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii