Marekani: Profesa Nathan Alexander asifiwa kwa kufundisha huku amembeba mtoto wa mwanafunzi wake

Professor Nathan Alexander hold baby Assata Haki miliki ya picha Twitter/@Original_Vaughn
Image caption Profesa Nathan Alexander anasema mtoto huyo kwa jina la Assata alikuwa ametulia sana alipombeba

Profesa mmoja wa hesabu nchini Marekani amepokea sifa nyingi mara baada ya picha yake akiwa amembeba mtoto wa mwanafunzi wake akiwa anafundisha darasani, kusambaa mitandaoni.

Mtoto huyo Assata alikuwa amekuja darasani na baba yake, Wayne Hayer, ambaye alikuwa amekosa mtu wa kumsaidia kumlea mtoto huyo nyumbani.

Mara baada ya mwanafunzi huyo kuelezea hali iliyomkuta kwa Profesa Nathan Alexander, mwalimu huyo aliamua kumbeba mtoto huyo kwa muda wa dakika 50 wa kipindi chake chote kwa nia ya kumpa fursa mwanafunzi wake Hayer kuandika dondoo ya kile alichokuwa anakifundisha.

"Sijabahatika kuwa na mtoto hivyo hata wakati nambeba mtoto huyu nilikuwa nna hofu kuwa atalia, lakini cha ajabu ni kuwa alikuwa ametulia vizuri sana".

Profesa Alexander anafundisha katika darasa la wanaume lililoko kwenye chuo cha kihistoria cha watu weusi huko Atlanta, Georgia.

Profesa Alexander mwenye umri wa miaka 34, aliripotiwa akimwambia mwanafunzi wake Hayer kuwa anaweza kuwa anamleta mtoto wake darasani kila siku mara baada ya kugundua kuwa mwanafunzi huyo huwa anawahi kutoka ili kuwahi kumlea mtoto wake.

Profesa Alexander alipohojiwa na chombo cha habari cha Marekani cha CNN, alisema "Huyu mwanafunzi huwa ana kazi mbili nazo ni kuhudhuria kusoma siku nzima na kuwa mzazi na mlezi".

Picha hii inasaidia kuwakumbusha wazazi majukumu yao na kile ambacho wanapaswa kufanya kila siku na kuna umuhimu gani kwa mtu kuwa mlezi mzuri wa mtoto.

"Na mtoto huyo alipoanza kulala, niliwaambia wanafunzi wangu kuwa nahisi nimeanza kuwachosha sasa" Profesa Alexander alisema.

Picha hiyo ilishirikishawa na watu wengi kwenye mitandao ya kijamii ikiwa ina lengo ya kumuunga mkono Alexander kwa namna anavyofundisha.

Mitandao ya kijamii imemsifu baba yake Assata kwa uthubutu wa kuja na mtoto darasani.

Maprofesa wengine pia wamejitolea kumsaidia mwanafunzi huyo katika malezi ya mtoto .

Katika mtandao wa kijamii wa Facebook, mama yake Assata, Firda Haye alielezea shukrani zake kwa Alexander na watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii kwa kuwapa moyo.

Profesa Alexander aliandika katika kurasa yake ya Tweeter kutoa shukrani kwa upendo ambao watu wameuonyesha , na kueleza kuwa yeye ni mwalimu wa kawaida tu hana tofauti na wengine ingawa kila mwalimu ana mbinu yake ya ufundishaji."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii