Marufuku tano maarufu za utawala wa rais John Magufuli nchini Tanzania

Left: Man reading a newspaper in Tanzania, followed below by people at a political rally in Tanzania, followed below by schoolgirls holding books, followed below by a plane at Dar es Salaam airport Right: Tanzanian leader John Magufuli Haki miliki ya picha AFP

Mwezi Januari ulianza na katazo jipya nchini Tanzania - hospitali zote za umma zilipigwa marufuku kuonesha tamthilia na kutakiwa kuonesha vipindi vyenye maudhui ya afya tu.

Toka Raisi John Pombe Magufuli alipochukua hatamu za uongozi wa nchi hiyo mwezi Novemba 2015, serikali yake imekuwa maarufu kwa kutoa maamuzi ya haraka.

Siku chache tu toka alipokula kiapo cha uraisi, alifuta sherehe za Uhuru na kuelekeza pesa zilizoandaliwa kwa shughuli hiyo ziende kwenye ujenzi wa kipande cha barabara ambacho kilikuwa na msongamano mkubwa wa magari.

Hakupoteza muda kuwatimua vigogo kadhaa serikalini katika vita vyake dhidi ya rushwa, hatua hizo aliziita kutumbua majipu. Pia alizuru bila kutoa taarifa awali kwenye ofisi kadhaa za umma ambazo zilikuwa na matatizo kwenye kutoa huduma, na kuchukua hatua.

Hatua hizo hazikufurahiwa ndani ya Tanzania tu, bali Afrika nzima. Watumiaji wa mtandao wa kijamii wa twitter wakaja na 'hashtag' ya #WhatWouldMagufuliDo? ambapo marais wengine imma walidhihakiwa ama kutakiwa kuiga mfano wa Magufuli katika utendaji kazi.

Kufikia mwaka wa 2019, maoni na mitazamo juu yake na serikali yake yamegawanyika mno.

Haya ni makatazo matano ambayo yamechangia kujengeka kwa taswira ya Magufuli na serikali yake ndani na nje ya Tanzania.

1) Safari za Nje

Haki miliki ya picha AFP

Katika wiki yake ya mwanzo ofisini, Magufuli alisitisha safari zote za nje ya nchi kwa watumishi wa umma.

Pale ilipotokea dharura, kibali cha kusafiri kilikuwa kikitolewa na Magufuli mwenyewe ama Katibu Mkuu Kiongozi, kipindi hiko alikuwa balozi Ombeni Sefue.

Magufuli alisisitiza kuwa watumishi waongeze safari za ndani hususani kwenda vijijini kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania masikini.

Hatua hiyo ilipokewa kwa mikono miwili na umma, maana watumishi katika macho ya raia walikuwa wakionekana kama wafujaji wa fedha za walipakodi kwa kusafiri mara kwa mara ughaibuni tena wakipanda madaraja ya juu kwenye ndege.

Mpaka sasa safari za nje kwa watumishi bado zinadhibitiwa, na ijapokuwa rais hatoi vibali, lakini ruhusa hiyo inatolewa na mamlaka ambazo zipo chini ya uangalizi wa karibu wa ofisi ya rais.

Ripoti ya Benki Kuu ya nchi hiyo iliyotolewa mapema 2016 ilibainisha kuwa, Tanzania iliokoa dola milioni 429.5 kwa kudhibiti safari za nje katika kipindi cha kuanzia Novemba 2015 mpaka Novemba 2016.

Magufuli mwenyewe bado hajasafiri nje ya Afrika Mashariki toka alipoupata uraisi. Ametembelea tu nchi jirani za Uganda, Kenya na Rwanda.

Safari yake ya mbali zaidi ni kwenda nchini Ethiopia mwezi Januari 2017 kuhudhuriia kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika (AU).

Mara kadhaa amenukuliwa akisema anaepuka kusafiri nje ya nchi japo anapata mialiko ili kuokoa fedha za walipakodi.

2) Matangazo mubashara ya bunge

Haki miliki ya picha Getty Images

Matangazo mubashara ya bunge kwenye televisheni yalianzishwa mwanzoni mwa utawala wa rais Jakaya Kikwete ambaye ni mtangulizi wa Magufuli madarakani.

Chini ya uongozi wa Spika Samuel Sitta, bunge likajizolea umaarufu kwa viwango na kasi. Serikali ya Kikwete ikatikiswa haswa na bunge hususani kwenye kashfa kubwa za rushwa/ufisadi.

Mijadala ya bunge kuhusu kashfa ya Richmond - ambapo uchunguzi wa kamati ya bunge ulibaini makosa kwenye utoaji wa mkataba wa kufua umeme kutoka Marekani - na kupelekea kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Edward Lowassa ilirushwa mbashara kwenye televisheni.

Pia 'sarakasi' za kashfa ya Escrow mwaka 2014 iliyowaondoa madarakani mawaziri wawili waandamizi na Mwanasheria Mkuu pamoja na kuwatia lawamani, wafanyabiashara wakubwa, wanasiasa mpaka majaji.

Hayo pamoja na mengine yalifanya matangazo hayo maarufu kama 'Bunge Live' kuwa lulu miongoni mwa wananchi.

Hata hivyo, mwanzoni mwa 2016, serikali ya Magufuli iliminya matangazo hayo kwa kuanza na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) na baadae mpaka kwa televisheni binafsi.

Kwa sasa, matangazo mubashara ni yale ya kipindi cha maswali na majibu tu. Mijadala hairushwi mubashara tena.

Kambi ya Upinzani pamoja na asasi za kiraia zilipinga vikali hatua hiyo wakisema imefanywa kwa makusudi kulitenganisha bunge na wananchi.

Nape Nnauye, ambaye alikuwa waziri wa habari wakati huo, aliitetea uamuzi huo akisema kuwa ilikuwa ni mzigo mzito kifedha kwa TBC kurusha matangazo hayo mbashara.

Alisema kwa siku moja TBC ilikuwa ikiingia gharama ya Tsh 4.2 sawa na dola milioni 1.8.

Pia alidai kuwa Tanzania si nchi ya kwanza katika Jumuiya ya Madola kufanya hivyo.

3) Wanafunzi wanaopata ujauzito

Haki miliki ya picha Getty Images

Kuweka rekodi sawa, si serikali ya Magufuli ambayo iliasisi katazo la wanafunzi wanaopata uja uzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Hata hivyo, Magufuli amezuia jitihada za kuondosha katazo hilo ambalo limedumu kwa zaidi ya miongo minne.

Kwa miaka kadhaa, wanaharakati wa haki za binaadamu - pamoja na baadhi ya wanasiasa kutoka chama tawala CCM na upinzani walikuwa wakifanya kampeni za kuwawezesha mabinti kurudi katika shule za umma baada ya kujifungua.

Hatimaye mwaka 2015, CCM katika ilani yake ya Uchaguzi Mkuu iliahidi kuwa wanafunzi hao wataruhusiwa kuendelea na masomo.

Suala hilo likaibuka bungeni mwezi Mei 2017 wakati wa mjadala wa bajeti ya wizara ya elimu. Upinzani na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii wakiishauri serikali kuwa muda muafaka wa kufanya mabadiliko kwenye sera hiyo ulikuwa umewadia.

Hata hivyo, mjadala mkali ukaibuka kati ya waliotaka mabadiliko na wahafidhina ndani ya bunge.

Miongoni mwa wahafidhina (ambao walikuwa wakipinga mabadiliko kufanyika) ni Mke wa Rais Mstaafu Mama Salma Kikwete ambaye sasa ni mbunge wa kuteuliwa na rais.

Mwezi mmoja baadae, katika hafla ya ufunguzi wa barabara eneo la Chalinze ambapo Mama Kikwete alikuwepo, rais Magufuli aliweka wazi msimamo wake juu ya suala hilo, akisema kuwa serikali yake haitaruhusu wasichana hao kuendelea na masomo.

Uamuzi huo wa Magufuli umepingwa vikali na wanaharakati pamoja na mashirika kadhaa. Mwaka jana, Benki ya Dunia ilizuia mkopo wa thamani ya dola milioni 300 kwa Tanzania ikiitaka nchi hiyo kuachana na sera hiyo.

Hata hivyo, katazo hilo linaishia Tanzania Bara tu, visiwani Zanzbar kuna sera ya tofauti ambapo wasichana wanaopata ujauzito wanaruhusiwa kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

4) Mikutano ya siasa

Haki miliki ya picha AFP

Mara baada tu ya kuingia Ikulu ya Magogoni, Magufuli aliweka wazi msimamo wake kuwa hatopenda kuwaona wanasiasa wakizunguka nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara.

Hoja yake kubwa ni kuwa "watu waachwe wafanye kazi na kulijenga taifa" na wanasiasa wasubirie kampeni za Uchaguzi wa 2020 ili kuzunguka nchi kujinadi.

Vyama vya Upinzani kama ilivyotarajiwa walipinga vikali katazo hilo. Vyama hivyo vimekuwa vikiitumia mikutano ya hadhara katika kunadi sera na kuwafikia wananchi hususani wa maeneo ya nje ya miji mikubwa.

Chama kikuu cha upinzani cha Chadema kilitangaza operesheni ya kupinga kile walichokiita Udikteta Tanzania (UKUTA) na kudhamiria kufanya maandamano ya nchi nzima mwaka 2016, lakini waliisitisha kabla ya kuanza.

Toka kipindi hiko, polisi wamewashughulikia makumi ya viongozi wa upinzani wanaodaiwa kukaidi marufuku hiyo - na takriban wabunge 17 wa upinzani kwa sasa wapo mahakamani kukabiliana na mashtaka.

Mwishoni mwa mwaka jana, Magufuli alionya wapinzani kupitia waziri mkuu wa zamani ambaye ni kada wa zamani wa Chadema Edward Lowassa kuwa wasipoitii sheria wataishi jela.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chadema yupo mahabusu pamoja na mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko toka mwezi Novemba 2018 kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana.

Hata hivyo akiongea na viongozi wa dini ikulu mwezi Januari, Magufuli amedai kuwa hakuna mwanasiasa aliyezuiwa kufanya mikutano ya hadhara, isipokuwa wanatakiwa kuifanya kwenye majimbo wanayowakilisha tu.

Wakosoaji wa Magufuli pia wanamlaumu kwa kuminya uhuru wa habari na kujieleza kwa ujumla wake.

Kwa kupitia zinazoitwa sheria kandamizi dhidi ya uhuru wa habari, vyombo vya habari kadhaa vimefungiwa kwa muda tofauti kwa kutangaza ama kuchapisha taarifa ambazo mamlaka inadai kuwa ni 'chonganishi' ama zenye 'kupotosha'.

Mwaka 2017 aliwaonya wamiliki wa vyombo vya habari kuwa wajiangalie, na kuwa hawana uhuru kwa kiasi wanachofikiria.

5) Usafirishwaji wa makinikia nje ya nchi

Haki miliki ya picha AFP

Mwezi Agosti 2016, rais Magufuli alipiga marufuku kusafirishwa kwa mchanga wa madini au makinikia nje ya nchi.

Wachimbaji wa madini nchini Tanzania wamekuwa wakisafirisha tani za makinikia kwenda Mashariki ya Mbali na Ulaya kwa ajili ya kuchenjuliwa.

Hata hivyo, kilichomo ndani ya mchanga huo na thamani yake limekuwa jambo lenye utata mkubwa.

Wachimba madini wanadai kuwa mchanga huo una madini kiasi kidogo na hayana thamani kubwa kibiashara, lakini hilo limekuwa likipingwa.

Mwezi Machi 2017, kampuni kubwa zaidi ya uchimbaji dhahabu nchini humo Acacia Ltd, iliyosajiliwa kwenye soko la hisa la London, ilishutumiwa kukiuka marufuku hiyo.

Magufuli alizuru bandarini jijini Dar es Salaam na kukuta makontena ya makinikia ya kampuni hiyo yakiwa tayari kusafirishwa nje. Aliamuru makontena hayo zaidi ya 250 yazuiliwe.

Kiongozi huyo aliunde tume mbili kuchunguza sakata hilo. Tume ya kwanza ilichunguza kilichomo ndani ya makinikia na tume ya pili ikachunguza thamani yake kiuchumi.

Tume zote mbili zilitoa ripoti ambazo zilikuwa 'mabomu' kwa Acacia, wakiituhumu kampuni hiyo 'kudanganya' thamani halisi ya madini ndani ya makinikia, na kupelekea kukwepa kodi kwa kiwango kikubwa.

Kutokana na ripoti hizo, serikali ya magufuli iliitoza Acacia deni la kodi ya dola bilioni 190 ambayo ilijumuisha miaka yote 17 ambayo kampuni hiyo iliyofanya shughuli zake Tanzania.

Japo Acacia muda wote imekuwa ikikanusha tuhuma dhidi yake, kampuni mama ya Barrick Gold, yenye maskani yake nchini Canada iliingia kwenye mazungumzo na serikali ya Magufuli.

Mwezi Oktoba 2017, pande hizo mbili ziliafikiana kuwa kampuni hiyo kuilipa Serikali ya Tanzania hisa ya asilimia 16 na mgawo wa asilimia hamsini ya mapato ya mauzo ya dhahabu kutoka migodi 3 inayoimiliki..

Barrick pia walikubali kutoa dola milioni 300 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kutokana na biashara ya kampuni hiyo.

Makubaliano hayo hata hivyo hayajatekelezwa - na mazungumzo ya kufanikisha utekelezwaji wake bado yanaendelea.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii