Usafiri katika uwanja wa ndege JKIA Nairobi watatizika, ndege zaelekezwa Tanzania

JKIA

Usafiri wa ndege umetatizika na abiria wamekwama katika uwanja mkuu wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi huku baadi ya ndege zikielekezwa kutua katika nchi jirani Tanzania.

Wafanyakazi wa usafiri wa ndege wameanza mgomo kupinga mpango wa kuunganishwa shughuli za usimamizi vya uwanja huo wa ndege kati ya shirika kuu la ndege nchini Kenya Airways na mamlaka ya usimamizi wa viwanja wa ndege KAA.

Kadhalika wafanyakazi wanatuhumu na kupinga makosa yanayofanyika katika uajiri wa wafanyakazi.

Muungano wa wafanyakazi hao (KAWU) umeuliza maswali kuhusu mipango hiyo ya kuunganisha shughuli kati ya pande hizo mbili na sasa unaitisha mageuzi katika usimamizi wa Kenya Airways na shirika la usimamizi wa viwanja vya ndege KAA.

Image caption Mgomo wa wafanyakazi watatiza usafiri katika uwanja wa ndege JKIA

Hatahivyo mamlaka hiyo ya KAA imetoa taarifa hapo jana ikieleza kuwa ilani ya mgomo iliowasilishwa na muungano huo wa wafanyakazi wa usafiri wa ndege umesitishwa kufuatia agizo la kuzuia mgomo kutoka kwa mahakama ya uajiri na leba lililotolewa hapo jana, Jumanne.

Katika ujumbe wake, mamlaka hiyo imetoa hakikisho la shughuli kuendelea kama kawaida:

Ujumbe huo ulijibiwa na wananchi waliolezea kutatizika kwao kutokana na hali iliyoshuhudiwa hivi asubuhi:

Vyombo vya habari nchini vinaeleza kwamba licha ya mamlaka hiyo ya viwanja vya ndege kutangaza kwamba mgomo umesitishwa, ndege zote hazikusafiri kutoka uwanja huo wa JKIA.

Taarifa zinaeleza kwamba hakuna ndege iliyoondoka tangu saa tisa alfajiri Jumatano huku mamia ya wasafiri wakikwama.

Oliver Sang raia aliyekuwa katika uwanja huo wa ndege ameelezea kutatizika kwa baadhi ya abiria waliokwama katika uwanja huo wa ndege tangu saa sita usiku.

Mwandishi wa BBC Lynne Wachira aliyepo katika uwanja huo anaeleza kwamba umati wa watu umekusanyika katika uwanja huo wa ndege na shughuli zimesita.

Nini chanzo cha mgomo huo?

Wafanyakazi hao walikusanyika asubuhi hii katika maandamano ya amani ambayo yalitibuliwa baadaye na maafisa wa usalama na katibu mkuu wa muungano huo kutiwa mbaroni kwa kile kinachotajwa kuwa ni kushiriki mgomo haramu.

Awali katika taarifa yake, Muungano huo wa (Kawu) umesema kwamba " ni makosa kabisa, na pia uhalifu, kufikiria kwamba KQ itadhibiti JKIA."

Image caption Moss Ndiema, katibu mkuu wa muungano wa wafanyakazi KAWU

"Kenya itapoteza mabilioni ya pesa katika mapato, na pia watu watapoteza ajira na huenda maisha yao yakaharibika," amesema katibu mkuu wa KAWU Moss Ndiema.

Akizungumza na BBC Katibu mkuu huyo ameongeza kwamba watarudi kazini iwapo tu wakuu wa mamlaka na shirika hilo wataondolewa.

Na wanataka pia Kenya Airways iwache kutumia wafanyakazi wa kutoka mashirika mengine ambao wanalipwa malipo duni ikilinganishwa na wale walio chini ya makubalinao ya majadilinao jumla ya mshahara yaliojadiliwa kati ya KQ na muungano huo.

Kenya Airways inamilikiwa kwa 48.9% na serikali na 7.8 % na kampuni ya ndege Air France-KLM.

Ndege 25 za nchi za nje huhudumu nje ya uwanja mkuu wa ndege Nairobi, ikiwemo Turkish Airlines, Emirates, South African Airways na Ethiopian.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii