Brexit: Uingereza kujiondoa EU kutaathiri uuzaji wa maua ya Kenya?

A woman picks roses at a greenhouse in Kenya Haki miliki ya picha Getty Images

Uingereza inapojiandaa kuondoka kutoka kwenye Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi Machi, wakuzaji wa maua nchini Kenya wanafuatilia kwa karibu yanayojiri.

Hii ni kwa sababu jinsi Uingereza itakavyouhama muungano huyo inaweza kuathiri pakubwa mapato yao.

Sekta ya maua ni muhimu sana kwa mapato nchini Kenya na mapato yanayotokana na mauzo ya maua ya Kenya nje ya nchi yameongezeka maradufu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mengi ya maua ya Kenya yanapouzwa kwenye mnada Amsterdam, Uholanzi huelekezwa Uingereza.

Wakuzaji na wauzaji wa maua Kenya wanajiuliza swali moja - Je, Brexit itaathiri vipi biashara yao ifikapo 29 Machi?

Hali kwa sasa ikoje?

Wauzaji wa maua ya Kenya kwa sasa huwa hawatozwi kodi yoyote wanapouza maua yao katika Umoja wa Ulaya (EU), na ndani ya Uingereza.

Hii ni kupitia utaratibu wa muda ambao Kenya ilipewa baada yake kukubali kutia saini na kuidhinisha Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara (EPA) wa kati ya EU na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Uholanzi ni kituo muhimu kwa maua ya Kenya yanaposafirishwa kuuzwa katika mataifa mbalimbali Ulaya

Mpangilio huo ni wa muda tu hadi pale nchi nyingine wanachama ikiwemo Tanzania, zitakapoiidhinisha EPA ndipo ianze kutekelezwa kikamilifu.

Bidhaa nyingine za Kenya zinazouzwa Ulaya kama vile majani chai, matunda na mboga huuzwa kupitia mpangilio huo.

Ni kwa nini Uingereza ni muhimu kwa maua ya Kenya?

Uingereza ni ya pili kwa kununua maua kutoka Kenya, Uholanzi ndiyo ya kwanza.

Takriban asilimia 18 ya maua yanayouzwa nje kutoka Kenya huuzwa nchini Uingereza.

Sekta ya maua ni muhimu sana kwa uchumi wa Kenya na huchangia asilimia 1.06 ya jumla ya pato la taifa Kenya, kwa mujibu wa Baraza la Maua Kenya (KFC).

Aidha, ni miongoni mwa sekta zinazoajiri watu wengi zaidi Kenya ambapo moja kwa moja hutoa ajira kwa watu 100,000 moja kwa moja na hutegemewa na watu milioni mbili.

Na ingawa Uingereza imesalia kuwa mshirika muhimu wa Kenya kibiashara, biashara kati ya mataifa hayo mawili imeanza kushuka miaka ya karibuni.

Biashara ya Kenya na UK

Chanzo: Idara ya Takwimu ya Uingereza (ONS)

Kuna sababu ya wasiwasi kuhusu Brexit?

Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Maua Kenya Clement Tulezi anasema miundo mbinu ya kushughulikia maua iwapo yatasafirishwa moja kwa moja hadi Uingereza bado haijastawishwa vya kutosha.

Hii inalazimu maua mengi yanayoingizwa Ulaya kwa kusudi la kuuzwa Uingereza kupitia Amsterdam na mjini Liege, nchini Ubelgiji.

Kutokana na hili, wauzaji wa maua ya Kenya wanatumai sana kwamba Uingereza itafanikiwa kuwa na mkataba na EU wakati wa kuondoka kutoka kwenye muungano huo tarehe 29 Machi.

Mkataba uliokuwa umependekezwa na serikali ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kufikia sasa bado haujaidhinishwa na Bunge huku muda ukiendelea kuyoyoma.

Bi May anatarajia kuwasilisha tena mswada wa kuongoza kujiondoa kwa Uingereza kutoka EU katika Bunge la Ulaya mapema wiki ijayo na iwapo mswada huo utashindwa tena, huenda akawasilisha mswada wa kuchelewesha kujiondoa kwa Uingereza kutoka EU mnamo Alhamisi mnamo 14 Machi.

Mswada uliopendekezwa kwa sasa na Bi May utatoa fursa ya kuwepo kwa kipindi cha mpito cha hadi 2020.

Katika kipindi hicho cha mpito, Kenya itaendelea kuuza bidhaa zake katika soko la Uingereza kwa utaratibu uliopo sasa, huku mashauriano kuhusu mkataba wa baadaye wa kibiashara kati ya Kenya na Uingereza.

Haya ndiyo matumaini ya serikali ya Kenya, kwamba Uingereza haitaondoka EU bila mkataba na kwamba kutakuwa na kipindi cha mpito.

Katibu wa wizara anayesimamia masuala ya biashara katika serikali ya Kenya Dkt Chris Kiptoo aliambia BBC kwamba: "Muda wote tumekuwa tumehakikishiwa kwamba biashara haitavurugika kwa sababu kutakuwa na kipindi cha mpito cha hadi 2020 Desemba ambapo Uingereza itakuwa ikiendesha shughuli zake chini ya sheria za Eu.

"Kusipokuwa na mkataba (wa kuongoza kujioandoa kwa Uingereza kutoka EU), haitakuwa sisi pekee (tutakaoathiriwa), itakuwa kila mtu ambaye amekuwa akifanya biashara na Uingereza. Kila mtu atalazimika kutafuta njia ya kufanya biashara nao."

Msemaji wa serikali ya Uingereza aliambia BBC: "EU ina mpangilio wa muda wa kibiashara na Kenya na tunakusudia kudumisha hali sawa kwa Kenya kusalia na ruhusa ya kuuza bidhaa soko ya Uingereza bila kutozwa kodi ya forodha au kuwekewa vipimo."

Wakati wa ziara yake Kenya mwaka jana, Bi May alisema Kenya itaendelea kuuza bidhaa zake Uingereza chini ya mpangilio wa sasa kati yake na EU hata baada ya Brexit, kabla ya utaratibu mpya wa kibiashara kuwepo.

"Tutakapoondoka EU, tutakuwa na fursa ya kushauriana kuhusu mikataba hii ya kibiashara kama Uingereza badala ya kama sehemu ya EU," aliongeza.

Kenya inauza maua zaidi

Chanzo: Idara ya Taifa ya Takwimu Kenya & Mamlaka ya Mboga na Matunda Kenya

Na kusipokuwepo mkataba wa kujiondoa EU?

Lisha ya hakikisho hilo, bado kuna wasiwasi Kenya kuhusu kitakashotokea iwapo Uingereza itaondoka EU bila kuwa na mkataba.

Serikali ya Uingereza imesema inataka kunakili mikataba yote ya kibiashara iliyopo kati yake na EU ili kuhakikisha uendelevu baada ya Brexit.

Kuna jumla ya mataifa 70 ambayo Uingereza inafaa kutia saini mikataba nayo, mikataba ambayo huenda ikakosa kutumika tena iwapo Uingereza itaondoka EU bila mkataba.

Lakini barani Afrika, kufikia 21 Machi, Uingereza ilikuwa imetia saini mikataba na mataifa wanachama wa kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika (ESA), kanda inayojumuisha Madagascar, Mauritius, Ushelisheli na Zimbabwe.

Bila kuwepo na mkataba, na Uingereza ikiondoka EU bila mkataba, Uingereza huenda ikalazimika kuweka kodi ya forodha kwa bidhaa zinazotoka Kenya kwa mujibu wa sheria za Shirika la Biashara Duniani (WTO).

Ripoti ya mashirika ya Traidcraft Exchange na Fairtrade Foundation ya Uingereza inasema bidhaa za Kenya huenda zikatozwa kodi ya kati ya 8.5-12% chini ya sheria za WTO, kodi ambayo inaweza kugharimu wauzaji wa maua ya Kenya hadi £3.6m kila mwaka.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Sekta ya maua huajiri watu 100,000 moja kwa moja Kenya

Hili, mashirika hayo mawili yanasema kwenye ripoti yao, litaathiri sana ushindani wa maua ya Kenya na kuathiri mapato ya wauzaji na pia mapato ya wanaotegemea sekta ya maua Kenya.

Kuna pia wasiwasi kwamba kuwepo kwa vituo vya forodha mpakani ambavyo huenda vikachelewesha kufika kwa bidhaa sokoni Uingereza.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Kenya Anzetse Were anasema kusipokuwa na mkataba Uingereza ikijitoa EU huenda wafanyabiashara wanaouza maua ya Kenya Ulaya wakalazimika kuunda utaratibu mpya wa kuuza maua hayo Uingereza au walazimike kutumia mawakala.

Mapato ya Kenya kutoka kwa mauzo ya maua

Chanzo: Idara ya Taifa ya Takwimu Kenya, Mamlaka ya Mboga na Matunda Kenya

"Hii itakuwa ni kazi na gharama ya ziada kwao wakijaribu kuboresha mifumo yao ya kusafirisha na kuuza bidhaa zao kuhakikisha kwamba inaendelea kufanya kazi vyema kama vilivyokuwa mataifa ya Ulaya yalipokuwa kwenye soko moja," anasema.

Katika kipindi kirefu, Traidcraft Exchange na Fairtrade Foundation, wanahofia kwamba Uingereza huenda ikatoa kipa umbele kwa mikataba ya kibiashara na mataifa tajiri na yenye uwezo mkubwa kutokana na umuhimu wake kibiashara na bidhaa.

Lakini mashirika hayo yanaamini mataifa yasiyo na uwezo mkubwa kiuchumi yanahitaji hakikisho kwamba yataendelea kusaidiwa katika juhudi za kupunguza umaskini.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii