Salaam za rambirambi zaendelea kutolewa na mashabiki wa Clouds FM baada ya kifo cha Ephraim Kibonde

Ephraim Kibonde Haki miliki ya picha Mashughuli Blog
Image caption Mtangazaji Mahiri wa Clouds FM Ephraim Kibonde aaga dunia

Salaam za rambirambi zimeendelea kutolewa, baada ya kutokea kifo cha Mfanyakazi na mtangazaji mahiri wa Clouds fm Ephraim Kibonde

Mganga Mkuu wa mkoa wa Mwanza Dokta Thomas Rutachunzibwa ametoa taarifa kuhusu kifo cha Ephraim Kibonde kilichotokea alfajiri ya siku ya Alhamisi.

Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Bugando ilipokea mwili wa marehemu Kibonde akitokea hospitali ya Uhuru jijini humo.

Buriani Ruge Mutahaba

Kabla ya kufikishwa Mwanza Kibonde alipata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera.

Taarifa ya Mganga mkuu inasema umauti ulimkuta akiwa njiani kuelekea hospitali ya rufaa ya Bugando kwa ajili ya kupata matibabu.

Alianza kujisikia kuumwa tangu alipokua kwenye msiba wa Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji marehemu Ruge Mutahaba huko Bukoba.Kisha kupelekwa kwenye hospitali ya Bukoba kabla ya kuamua kumpeleka Mwanza.

Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga amesema mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam, leo Alhamisi usiku ukitokea jijini Mwanza.

Kibonde alikua mtangazaji mahiri wa kipindi cha JAHAZI cha Clouds fm, kipindi ambacho kimejizolea wasikilizaji wengi kutokana na namna yeye na watangazaji wenzie wanavyowasilisha maudhui mbalimbali ya kipindi hicho kinachoruka majira ya jioni kila siku.