Siasa Tanzania: Edward Lowassa sasa awaomba watanzania wamuunge mkono rais Magufuli

Edward Lowassa

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewaomba watanzania waliompigia kura katika uchaguzi mkuu uliyopita kumuunga mkono, Rais John Magufuli.

Lowasa amesema hayo mkoani Arusha alipokuwa akiwahutubia mamia ya wafuasi wa chama cha mapinduzi CCM, waliojitokeza kumpokea baada ya kukabidhiwa rasmi kadi ya uanachama.

"Nimerudi nyumbani msiniulize nimerudi kufanya nini, nimerudi nyumbani," alisema Lowassa huku akiwapungia mkono wafuasi wa CCM ambao walilipuka kwa shangwe na vigelegele.

Akiendelea kuzungumza alisema "Katika uchaguzi nilipata kura zaidi ya milioni sita si haba, naomba wote walionipigia kura tumuunge mkono Rais John Magufuli."

Pia aliwashukuru viongozi wa Chadema na wanachama wao japo alikuwa na hofu tamko laki hilo lisipotoshwe.

Lowassa aidha alielezea kwanini ameamua kurudi CCM.

Kwa upande wake katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amempongeza Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa kwa kurejea CCM na kuweka siasa pembeni kwa kujali Taifa.

Akizungumza katika hafla ya kumpokea Lowassa na wanachama wengine wa upinzani jana viwanja vya CCM wilaya ya Monduli,

Polepole alisema kwa Lowassa amefuata taratibu zote za kujiunga CCM, baada ya kikao cha tawi analotoka kukubali kurejea CCM, ikifuatiwa na kikao cha kamati ya siasa ya kata nyumbani ambao

wamekubali arejee CCM.

Makada watiifu wa bwana Lowassa aliohama nao CCM na kutoka Chadema, Matson Chizii na Hamis Mjega pia wameandamana nae katika ziara hiyo ya kwanza tangu aliporejea tena katika chama tawala.

Mgeja ambaye aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa wamerejea nyumbani CCM.

"Tumerudi nyumbani mimi na Lowassa ni marafiki nina imani tutaendelea kukijenga chama chetu CCM," alisema.

Baada ya kutua Arusha, Lowassa alipokewa na mjumbe wa baraza la kitaifa wa mkoa wa Arusha Daniel Awakii na kusalimiana na wana CCM wengine.

Lowassa alirejea rasmi CCM mwanzo wa mwezi machi na kuwaambia viongozi na wananchi waliofika kushuhudia kuwa "nimerudi nyumbani."

Haki miliki ya picha CHAMA CHA MAPINDUZI
Image caption Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na Rais wa Tanzania,Dr John Magufuli akimkaribisha Edward Lowassa

Hatua iliyowashtua wengi kwani haikutarajiwa kutokana na mvutano uliokuwa hapo awali.

Lowassa aliwahi kuonekana mara kadhaa akikutana na Rais Dokta John Magufuli na kufanya naye mazungumzo katika Ikulu ya Tanzania.

Japo umma haukufahamu chochote kuhusu mazungumzo yao, minong'ono ilizuka kuwa ana mipango ya kurudi CCM.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, kumekuwa na wimbi la wapinzani kuhamia CCM, hatua ambayo imeelezwa na wachambuzi wa mambo kuwa upinzani unadhoofika.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii