Ethiopian Airlines: Ni nani waliopoteza maisha?

Eneo ambalo ndege ilianguka Kusini-Mashariki mwa Addis Ababa.
Image caption Eneo ambalo ndege ilianguka Kusini-Mashariki mwa Addis Ababa.

Abiria kutoka kwa zaidi ya mataifa 30 walikua kwenye ndege ya Ethiopian Airlines kutoka Addis Ababa kuelekea Nairobi iliyoanguka na kugharimu maisha ya watu 157 siku ya Jumapili.

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni raia 32 wa Kenya, 18 Canada, 9 Ethiopia na 7 raia wa Uingereza,hii ni kwa mujibu wa orodha ya abiria iiyochapwa na maafisa wa Ethiopia.

Abiria kadhaa wanaaminika kuwa na uhusiano na Umoja wa Mataifa.

Uganda

Polisi nchini Uganda wanaomboleza kifo cha kamishna wa polisi nchini Uganda Alalo Christine ambaye alikua akifanya kazi na kikosi cha kulinda amani cha AMISOM nchini Somalia akitumiakia nafasi ya kamishna wa polisi msaidizi.

Alikua anarejea kutoka Italia kuelekea Mogadishu,Somalia akiwa mmoja kati ya abiria wa ndege hiyo iliyoanguka siku ya Jumapili.

Kamanda wa polisi alifikisha taarifa hizo kwa familia yake na kuratibu taratibu za kuhakikisha mweili wa Bi Alalo unarejea nyumbani

Kenya

Haki miliki ya picha Hassan Katende/Facebook
Image caption Captain Yared (kulia) ana asili ya Kenya na Ethiopia

Kapteni Mulugeta Gatechew,ambaye ana asili ya Kenya na Ethiopia, alikua rubani mkuu kwenye ndege namba 302.

Amekua akifanya kazi na Shirika la ndege la Ethiopia tangu mwezi Novemba mwaka 2007.

Ni ''mwenye kusifika kwa utendaji wake'' akiwa ametumia zaidi ya saa 8,000 angani, Kampuni imeeleza.

Rafiki wa Kapteni Yared anasema ''nywele zake zilimsimama'' aliposikia kuwa amepoteza maisha.

Katika mahojiano na BBC kwa lugha ya Amharic, Hassan Katende amesema alipata taarifa za ajali kwenye mitandao ya kijamii.

''Siwezi kulala.Imenishtua sana.Ni vigumu kuamini, huwezi kuamini kwa kweli,'' alieleza.

Haki miliki ya picha Georgetown Law
Image caption Cedric Asiavugwa

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni Cedric Asiavugwa, Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa shahada ya sheria chuo cha Georgetown.

Alikua akisafiri kwenda Nairobi kuhudhuria mazishi ya nduguze, ripoti zimeeleza.

''Familia ya Georgetown imepoteza mwanafunzi wake kinara, rafiki wa wengi, na mahiri kwenye taaluma yake ya sheria Afrika Mashariki na duniani,'' alieleza mkuu wa idara ya Sheria chuo cha Georgetown, William Treanor.

Bwana Asiavugwa ametumia taaluma yake ya masuala ya haki za jamii, hasa haki za wakimbizi na makundi ya jamii zisizo na utetezi, kilieleza chuo hicho.

Pia alianya utafiti katika mada mbalimbali kuhusu amani, usalama wa chakula nchini Kenya, Uganda, Tanzania na Sudani Kusini.

Hussein Swaleh, Mwamuzi wa mchezo wa soka, pia amepoteza maisha kwenye ajali hiyo, Shirikisho la Soka Afrika limeithibitishia BBC.

Rais wa shirikisho la soka nchini Kenya ameandika kwenye ukurasa wa twitter kuwa ''ni siku ya huzuni kwa wapenda soka''

Inaelezwa Swaleh alikua akirejea nyumbani baada ya kuchezesha mchezo wa ligi ya kilabu bingwa Afrika, huko Alexandria,Misri.CAF imeeleza kwenye taarifa yake.

Salamu za rambirambi zimeendelea kumiminika kutokana na kifo cha Mwanahabari Anthony Ngare 49, aliyepoteza maisha kwenye ajali ya ndege.

Bwana Ngare alikua akiwakilisha Kenya kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Paris na alikua akielekea Nairobi.

Alikua Mhariri wa Standard Group na pia kwenye shirika la serikali.

Kabla ya kifo chake alikua akifanya kazi na UNESCO kama Mkurugenzi msaidizi wa mawasiliano.

Tume ya Taifa ya UNESCO Kenya imemtaja Bwana Ngare kuwa ''mmoja kati ya Nyota zinazong'ara''.

Canada

Haki miliki ya picha Carleton University
Image caption Pius Adesanmi

Canada imethibitisha kuwa mmoja kati ya watu waliowatambua ni Profesa Pius Adesanmi, mzaliwa wa Nigeria, Mkuu wa Taasisi ya taaluma ya masomo ya Afrika, Chuo cha Carleton

''Mchango wake chuoni ni mkubwa,'' alisema kiogozi wa idara ya Sanaa na Sayansi ya jamii, Pauline Rankin.

''Alifanya kazi bila kuchoka kuijenga taasisi ya masomo ya Afrika, akishirikiana vizuri na wanafunzi.Alikua mkufunzi na mwalimu wa kaliba ya juu ambae ameacha alama chuon Carleton.''

Kifo chake kimewashtua, wasomi na waandishi wa habari.

Profesa Adesanmi alikua akisafiri kuelekea Nairobi kushiriki mkutano ulioratibiwa na Umoja wa Afrika, ripoti zimeeleza.

Haki miliki ya picha Danielle Moore/Facebook
Image caption Danielle Moore

Danielle Moore,24 ,alikua akisafiri kwenda Nairobi kuhudhuria mkutano wa mazingira wa Umoja wa Mataifa.

Tarehe 9 mwezi Machi aliandika kwenye ukurasa wake wa facebook : ''Ninafurahi sana kuwashirikisha kuwa nimechaguliwa kuhudhuria na niko njiani nakwenda kwenye mkutano wa mazingira wa Umoja wa Mataifa jiini Nairobi Kenya .''

''Wiki ijayo nitapata nafasi ya kujadili masuala ya mazingira, kushirikishana habari na kukutana na vijana wengine na viongozi kutoka duniani kote.Ninafurahia fursa hii na ningependa baadae kuwashirikisha wengine nikirejea nyumbani.''

Bi Moore alikua mwanafuzi wa chuo kikuu cha Dalhousie baadae Taasisi ya Sayansi ya bahari Bermuda mwaka 2015.

Ethiopia

Sara Gebre Michael alikua Kiongozi wa wahudumu wa ndege ya shirika la ndege la Ethiopian Airlines namba 302.

Msanii maarufu nchini Ethiopia ambaye alikua jirani yake Tesfaye Mamo, ameiambia BBC kuwa alikua mama anayejali, na atakumbukwa sana.

Amemuacha mume na watoto watatu.

Tesfaye pia ameweka picha za Sara Gabre Michael kwenye ukurasa wake wa facebook.

Haki miliki ya picha Family handout
Image caption Joseph Waithaka

Joseph Waithaka,55, ana uraia pacha wa Uingereza na Kenya.Mtoto wake Ben Kuria, amesema alipata mshtuk baada ya kusikia kuwa baba yake ambaye alihamia Uingereza mwaka 2004, alikua ndani ya ndege hiyo.

Bwana Kuria amemuelezea baba yake kuwa ni mtu ''aliyependa haki''