Burkina Faso: Taifa ambalo ni hatari kuenda shule

Samuel Sawadogo at a school in Foubé, Burkina Faso

Mashambulio ya wanamgambo na mapigano ya kijamii kaskazini mwa Faso yamewazuia watoto 150,000 kuenda shule.

"Shule nyingi zimechomwa moto, walimu wameshambuliwa na baadhi yao kuuliwa," anasema mmoja wa wakuu wa shule hizo, Samuel Sawadogo.

"Mwalimu anapouawa, hakuna hatua yoyote inayochukuliwa - kwa hivyo inabidi tujiokoe sisi wenyewe."

Jumla ya shule 1,111 kati ya 2,869 zimefungwa katika miezi ya hivi karibuni nchini Burkina Faso.

Zaidi ya watoto 150,000 wameathiriwa na hatua ya kufungwa kwa shule hizo.

Bwana Sawadogo anasema vikosi vya usalama vimeshindwa kuwahakikishia usalama wakaazi wa maeneo hayo, lakini ana matumaini kuwa shule zitafunguliwa hivi karibuni

Wazazi wanaogopa

BBC ilitembelea shule kadhaa katika maeneo yaliyoathiriwa na kutapata taswira ya kamili ya kwanini shule zimefungwa au kwanini madarasa hayana wanafunzi.

Baadhi ya shule hasa katika mkoa wa Sahel zinalengwa na wanamgambo wa kiislam ambao wanapinga ''elimu ya magharibi.''

Zingine zilizo katika mji wa unaofahamika kama Foubé, zimefungwa na waalimu ambao wanahofia huenda wakashambuliwa.

Image caption Wazazi mara nyingi huwatoa watoto wao shuleni kwa kuhofia huenda wakashambuliwa

Baadhi ya shule zimefunguliwa lakini hayana wanafunzi kwasababu wazazi wanahofia watoto wao huenda wakashambuliwa wakiwa njiani kuelekea shuleni.

Karibu na kijiji cha Foubé, waandishi wa BBC walipata shule ambayo imefunguliwa lakini wanafunzi hawako madarasani.

"Sidhani wanafunzi watarejea," alisema Joseline Ouedraogo, mmoja wa waalimu wa shule hiyo aliiambia BBC.

"Lakini wengine wakirudi, tutafanya kila juhudi kufidia muda," alisema.

Madarasa ya dharura

Masomo katika baadhi ya mashule huenda yasiendelee kwa muda mrefu.

Hii ni kwasababu shule hizo zimegeuka kuwa makaazi ya maelfu ya wakimbizi wa ndani waliyotoroka vijiji vyao na wanatumia shule kama kambi ya dharura.

Idadi ya wakimbizi wa ndani imeongezeka kutoka watu 43,000 mwezi Disemba hadi 100,000 mwezi January mwaka huu.

Image caption Watoto katika kambi ya wakimbizi ya Barsalogho

Ukosefu wa usalama nchini humo haujatokana na wanamgambo wa kiislam pekee.

Katika kambi ya wakimbizi ya Barsalogho, kaskazini mwa nchi hiyo zaidi ya watu 1,000 ambao wamewasili hivi karibuni wametoroka mapigano ya kijamii.

Katika kijiji cha Gorgadji, eneo la Sahel, watu 1,000 wametoroka makundi yaliyojihami karibu na mji wa Soum.

Kwa mujibu wa msimamizi kijiji hicho, Boniface Kaboré, ni watoto 30 pekee wanaosoma katika shule 32 zilizopo katika eneo hilo

Image caption Karibu watu 100,000 wamekimbia makwao kutokana na ghasia

Serikali inasema kuwa inafanya kila juhudi kukabiliana na suala la ukosefu wa usalama.

"Tumepeleka vikosi vya usalama katika maeneo tofauti'', Msemaji wa serikali Remis Dandjinou aliiambia BBC.

Kwa miaka kadhaa Burkina Faso haikuwahi kuathiriwa na makabiliano ya wanamgambo na serikali katika mataifa jirani ya Mali na Niger.

Lakini mashambulio kadhaa hatari yanashukiwa kutekelezwa na wanamgamo wa kiislamu nchini humo, kwa mujibu wa mashirika ya kiraia .

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Usalama umeimarishwa kaskazini mwa Burkina Faso

Serikali imekiri kuwa ''inajutia'' uamuzi wa kufanya mazungumzo na makundi ya kidini yaliyo na misimamo mikali.

"Kwa miaka kadhaa tumekuwa na jeshi ambalo jukumu lake ni kulinda utawala uliyo madarakani badala ya kutoa ulinzi kwa taifa letu," anasema Dandjinou.

"Kulikuwa na makubaliano ya serikali kutoa njia salama kwa magaidi ili nao waondoke nchini humo bila kushambuliwa na vikosi vya usalama."

Makubaliano hayo yalivunjika baada ya Roch Marc Christian Kaboré kuchaguliwa kuwa rais mwaka 2015.

''Ni hapo ndipo mashambulia yalipoanza ikiwa ni shambulio kubwa dhidi ya mji mkuu wa Ouagadougou'', aliongeza msemaji wa serikali.

Kwa sasa wazazi wengi na watoto wao wataendelea kuishi kwa hofu hali ambayo hawajui itakuja kutatuliwa lini.

Hadi wakati huo masomo shuleni sio jambo la msingi kwao.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii