UN: Ghasia huko DR Congo ni sawa na uhalifu dhidi ya binaadamu

Moja ya Kaburi yanayoelezwa kuzikwa watu wengi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Moja ya Kaburi yanayoelezwa kuzikwa watu wengi

Ripoti ya Uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa imesema ghasia Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika kipindi cha mwaka uliopita ni sawa na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Ripoti hiyo imesema takriban watu 500 waliuawa ikiwemo familia kuchomwa moto ndani ya nyumba zao na mtoto wa miaka miwili kutupwa ndani ya tanki la maji machafu.

Ghasia za kikabila zilitokea pia wakati jamii moja ilipotaka kuzika mmoja ya viongozi wao wa Kitamaduni katika ardhi ya jamii nyingine.

Aidha uchunguzi huo umeonesha pia vurugu zinaweza kuibuka tena wakati wowote.

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamefahamisha kuwa ghasia zilizotokea kati ya Desemba 16 na 18 zilikuwa zimepangwa.

Jamii ya kabila la Batende walivamia na kushambulia vijiji vya wa Banunu, na watu wachache tu ndio waliofanikiwa kutoroka.

Taarifa hiyo, imeongeza pia Mamlaka katika eneo la Yumbi, kwenye jimbo la Mai-Ndombe, magharibi mwa nchi, zilishindwa kuwajibika kwa kuwalinda raia.

Idadi ya watu waliokufa inaweza kuwa zaidi ya 535, iliyowekwa katika ripoti hiyo ya uchunguzi.

Januari mwaka huu, Umoja wa Mataifa umesema watu 890 waliuawa.

Timu hiyo ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa iliweza kuvifikia vijiji vitatu kati ya vinne, wakati wa mashambulizi yalipopamba moto.

Miili ya watu inaaminika pia ilitupwa katika mto Congo.

Haki miliki ya picha ATLAS
Image caption Ramani ya DRC

Kutokana na ghasia hizo, zoezi la upigaji kura katika uchaguzi mkuu nchini humo uliopangwa kufanyika Desemba 30, umeahirishwa mpaka Machi 31.

Hata hivyo tayari aliyekuwa kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi ametangazwa kuwa mshindi na sasa ndio Rais wa nchi hiyo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii