Makamu wa rais Tanzania: 'Afrika Mashariki iko katika mikakati ya kuweka mfumo sawa wa elimu'

Makamu wa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Makamu wa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Jumuia ya Afrika Mashariki iko katika mikakati ya kuweka mfumo sawa wa elimu ili kuwawezesha wanafunzi wa nchi hizo kuwa na vyeti vinavyolingana kwa ubora.

Ameyasema hayo akizungumza na BBC mjini Kampala alikoshiriki kongamano kuu la siku mbili linalowashirikisha viongozi wa Afrika na wadau wa mashirika binafsi pamoja na viongozi wa vijana ambalo limelenga kujenga mshikamano zaidi barani kuweza kuinua kiwango cha maendeleo hususan kwa kuwashirikisha vijana.

Bi Samia ameeleza kwamba jumuiya ya Afrika mashariki inapanga kuidhinisha mfumo huo utakao toa nafasi ya cheti cha mwanafunzi kutambulika kieneo.

'Popote anaposoma iwe Tanzania Kenya au Uganda ili mtoto akitoka na cheti popote ndani ya East Afrika kinajulikana. Itachukua muda lakini tunakwenda pole pole'. Amesema makamu huyo wa rais.

Wajumbe katika mkutano huo wamekuwa wakijadili nafasi ya Afrika na mageuzi yanayoshuhudiwa katika bara kiuchumi, kisiasa na katika maendeleo ya jamii.

Bi. Samia ameeleza haja ya kuwekeza katika mfumo wa elimu ili kuboresha ujuzi zaidi miongoni mwa wanafunzi badala ya elimu ya kufaulu kwa gredi au matokeo.

Amekiri kwamba Tanzania tayari imeidhinisha jitihada za kuhakikisha mwanafunzi anaendelea hadi kidato cha nne katika kuhakikisha wanafunzi wanaendelea na elimu ya shule ya msingi na zaidi 'kuwasaidia watoto wa kike kusalia masomoni na kumjenga na mawazo kujua wanapomaliza shul, ni kitu gani wanaweza kufanya'.

Tanzania miongoni mwa mataifa mengine kieneo yamekuwa yakikabiliwa na visa vya watoto wa kike kuacha masomo kutokana na matatizo yakiwemo mimba za utotoni.

Rais Magufuli alitangaza mnamo 2017, kwamba serikali yake haitoruhusu wasichana waja wazito kurudi shule.

Huwezi kusikiliza tena
Magufuli: Ukishapata mimba ni kwaheri shuleni

Mamilioni ya watoto Tanzania hawafiki katika shule ya upili au vyuo vya kiufundi. Inakadiriwa kuwa jumla ya watoto milioni 5.1 walio na umri wa kati ya miaka 7 hadi 17 hawaendi shuleni, na wengine wengi wakimalizia elimu katika shule za msingi, Human Rights Watch linasema.

Haki miliki ya picha KWA HISANI
Image caption Salma Kikwete mwenyekiti wa Wama, makamu wa Rais Samia Suluhu na Zakia Meghji aliyewahi kuwa waziri wa fedha na utalii nchini Tanzania

Anatazamaje uwakilishi wa wanawake katika Jumuiya ya Afrika mashariki?

Anasema 'hatujafika twendako, lakini tunakwenda vizuri'.

Bi Samia ametoa mfano wa Rwanda ambayo ina idadi kubwa ya wanawake bungeni na katika baraza la mawaziri.

Ameeleza kwamba Rwanda ni ya kupigiwa upatu kwa kupitisha kiwango cha 50/50 cha uwakilishi sawa wa kijinsia

Ikifuatwa na Uganda anayoeleza kuwa inakaribiwa kiwango hicho cha usawa.

Tanzania anasema ipo juu kidogo ya 40% na Kenya ikifuata nyuma katika kujaribu kulifikia hilo pia.

'Hatujafika twendako lakini tumeonyesha mfano, sisi Afrika mashariki tumekwenda vizuri' amesema Makamu wa rais Samia Suluhu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii