Kimbunga Idai: Msumbiji katika hatari kimbunga kingine kikali kikitua

Kimbunga Idai kinatarajiwa kuikumba Msumbiji
Maelezo ya picha,

Kimbunga Idai kinatarajiwa kuikumba Msumbiji

Watu wanaoishi katika mji mkuu wa Msumbiji Maputo wameonywa kutokea kwa hali mbaya zaidi kutokana na kimbunga kikali.

Tufani iliyopewa jina la Idai, ambayo inabeba upepo wenye kasi ya kilomita 225 kwa saa itasababisha kimbunga kikali karibu na bandari ya Beira, mji wenye watu wapatao laki tano.

Mvua kubwa iliyonyesha nchini humo tayari imesababisha vifo vya watu 100 nchini Msumbiji na Malawi.

Beira ni mji wa nne kwa ukubwa nchini Msumbiji ambapo bandari yake iko katika mdomo wa mto Pungwe ambao umekwenda mpaka Zimbabwe.

Kitengo cha hali ya hewa cha Ufaransa ambacho kinashughulikia maeneo yanayodhibitiwa na Ufaransa katika eneo la Bahari ya Hindi kimeonya kuwa hali inaweza kuwa mbaya kutokana na maji kujaa mengi.

Baadhi ya picha zilizotumwa katika mitandao ya kijamii zinaonesha madhara katika mji huo wa Beira wakati kimbunga hicho kikikaribia kwa miti mingi kuanza kung'oka.

Maelezo ya picha,

Miti iking'oka

Msumbiji imekumbwa na vimbunga vingi katika siku za nyuma ikiwemo kimbunga Eline mwaka 2000 kilichoua watu 350 na wengine 650,000 kuyakimbia makazi yao. Na mji wa Beira ndio mara kwa mara unakumbwa na hali hiyo.

Msumbiji ni nchi ambayo iko katika hatari ya kuathiriwa zaidi barani Afrika pale hali mbaya ya hewa inapotokea