Je Maalim Seif 'ametimuliwa' katika uongozi wa CUF?

Katibu Mkuu wa chama cha CUF Maalim Seif Sharrif Hamad Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Maalim Seif Sharrif Hamad

Chama cha Wananchi (CUF) kimemchagua Khalifa Suleiman Khalifa kuwa katibu mkuu wake mpya kufuatia uchaguzi uliofanywa na baraza kuu la chama hicho.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemtangaza Khalifa ambaye ni mbunge wa zamani wa Gando kuchukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad leo Jumamosi katika makao makuu ya CUF jijini Dar es Salaam.

Wengine waliyochaguliwa na Magdalena Sakaya ambaye sasa ni naibu katibu mkuu bara huku Fakhi Suleiman Khatibu akichaguliwa naibu katibu mkuu upande wa Zanzibar.

Mabadiliko hayo yanakuja licha ya mgogoro wa uongozi ambao umefanya chama hicho kumeguka huku Bwana Hamad akiongoza mrengo mmoja na Profesa Lipumba akiongoza mrengo mwingine.

Mzozo katika chama CUF ulianza baada ya Prof Lipumba kuwasilisha barua ya kujiuzulu kama mwenyekiti mwaka 2015 lakini akarejea tena wakati chama ilipokuwa inajiandaa kumchagua mwenyekiti mpya.

Lipumba alijiuzulu kupinga uteuzi wa Edward Lowassa kuwa mgombea wa uraisi wa muungano wa vyama vya upinzani uliyofahamika kama Ukawa katika uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015.

Image caption Chama cha CUF ni cha pili cha upinzani kwa kuwa na wawakilishi wengi bungeni

Mgogoro wa sasa unaingia katika awamu nyingine ambapo wanachama na wafuasi wamegawanyika katika pande hizo mbili, huku wakiwa katikati ya giza nene kuelekea katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 visiwani Zanzibar na Tanzania Bara.

Matokeo ya mgogoro huo yameonekana pia baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, chini ya Jaji Dk. Benhajj Masoud mnamo mwezi Februari 18 mwaka huu kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) wa kambi ya Profesa Ibrahim Lipumba.

Nguvu na ushawishi wa Maalim Seif

Katibu mkuu huyo amekuwa na nguvu ya kisiasa visiwani Zanzibar, wakati Lipumba anaonekana kuteka nguvu ya kisiasa ya chama hicho kwa upande wa Tanzania Bara.

Maalim ana nguvu kisiasa na ushawishi mkubwa katika pande hizo, ndiyo maana baadhi ya wanasiasa wanaendelea kumpigania na kuonyesha imani kubwa waliyonayo kwake.

Image caption Maalim Seif Sharrif Hamad

Wakati hatua hiyo ya Mahakama ikivunja sehemu ya nguvu za kambi ya Lipumba, bado upo mwendelezo wa mgogoro ndani ya chama hicho, ambapo uamuzi wa kesi ya msingi ya kupinga uhalali wa uenyekiti wa Lipumba bado haujatolewa.

''Tukiacha suala la hukumu ya Mahakama, ndani ya chama cha CUF makundi yote mawili ya Maalim Seif na Profesa Lipumba yanachukuliwa kuwa na nguvu za aina yake, hali ambayo imekuwa ikikiteteresha chama hicho kadiri ya siku zinavyokwenda.'' anasema Markus Mpangala, mchambuzi wa siasa nchini Tanzania.

Haki miliki ya picha AZANIA POST
Image caption Julius Mtatiro, Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya Chama cha upinzani (CUF)

Miongoni mwa viongozi wengine waliokihama chama hicho ni Julius Mtatiro (aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF kambi ya Maalim Seif Sharif Hamad), Maulid Mtulia (aliyekuwa mbunge wa chama hicho katika jimbo la Kinondoni), Abdallah Mtolea (aliyekuwa Mbunge wake wa chama hicho katika jimbo la Temeke), na Zuberi Kuchauka (aliyekuwa Mbunge wa chama hicho katika jimbo la Liwale mkoani Lindi).

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii