Ukame Kenya: Watu 10 wamefariki kutokana na uhaba wa chakula Turkana

drought Kenya
Image caption Mariam Loolio ni ajuza mwenye umri was miaka 85. Kwa siku tano anasema hajala chochote

Zaidi ya watu 10 wameripotiwa kufariki kutokana na ukame katika kaunti ya Turkana nchini Kenya,

Wengine zaidi ya 800,000 wakiendelea kuumia kwa makali ya njaa na kiu kwa mujibu wa wizara ya kudhibiti majanga na utumishi wa umma ya kaunti ya Turkana.

Serikali ya kaunti hiyo wiki iliyopita ilitoa hakikisho kwamba imeidhinisha mpango wa usaidizi kuwakinga wakaazi kutokana na madhara ya ukame uliopo.

Katika kijiji cha Kakwanyang' Turkana ya Kati, mizoga ya wanyama iliyotapakaa, na miti yaliyokauka inaashiria hali inayoshuhudiwa katika eneo hilo kutokana na na ukame.

Wakaazi wengi katika kijiji hiki hawajatia chakula chochote mdomoni kwa muda wa karibu siku 5 zilizopita.

Kwa sasa wakaazi hawa wanalazimika kutuliza makali ya njaa kwa kula matunda ya mwituni yajulikanayo kama Mkoma.

Moru Lomutan ni mzazi wa watoto sita na nilipofika nyumbani kwake nilimkuta akiwa analigonga gonga tunda la Mkoma ili kulifanya liwe laini kwake kutafuna.

"Najaribu kuligonga hili tunda kwa mawe ili nile kwa sababu sina hata nguvu ya kuliuma mdomoni"

Katika bwawa la maji, watu walikuwa wamejaa, kina mama na watoto.

Miale ya jua sio kizuizi kwa wanakijiji hao kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu ili kuweza kujipatia maji.

Karibu na bwawa hilo mizoga ya mbuzi na kondoo imetapakaa. Wakaazi wanadai kuwa mifugo hao walifariki baada ya kukosa chakula na maji.

Anna Emaret amepoteza mifugo wake 20. Anasema amekuwa akigawana chakula na mifugo wake, lakini chakula kilipoisha, wakafa.

Image caption Maji yamekuaka katika visima na mabwawa ya maji

"Kondoo wangu wote wamekufa, mbuzi pia wamekufa. Sasa sina mifugo, sina chakula, serikali isipotusaidia, tutakufa tu kama mifugo wetu"

Mariam Loolio ni ajuza mwenye umri was miaka 85. Kwa siku tano hajala chochote .

"Nimekaa hapa kungoja serikali ituletee chakula. Munavyoniona mimi ni mzee, tena kipofu. Hakuna jinsi ninavyoweza kutafuta chakula, hakuna kabisa. Kwa hivyo nasubiri tu serikali ije iniokoe ili nisife njaa. Sina namna"

Nancy Alimlim alimzika kakake siku ya Jumamosi. Anaelezea kwa uchungu huku akibubujikwa na machozi.

Image caption Anna Emaret anasema amekuwa akigawana chakula na mifugo wake, lakini chakula kilipoisha, wakafa.

Ukame umekuwa ukishuhudiwa kwa miaka mingi katika kaunti hii.

Kila mara ukame unapobisha hodi, maisha ya wakaazi na mifugo wao huwa hatarini.

Nchini Uganda katika Jimbo la Karamoja karibu na eneo hili la Turkana, Rais Museveni alijenga bwawa ambalo hutumiwa na jamii ya Karamoja ambayo ni jamii ya wafugaji.

"Kwanini serikali ya Kaunti na ile serikali kuu zisiungane pamoja na kutafutia wananchi suluhisho mwafaka na la kudumu kama ilivyofanywa na Rais Museveni upande ule mwingine?..." anauliza Paul Jaling'a, kiongozi wa vijana katika Kaunti ya Turkana.

"Inapaswa sisi kama vijana tuelimishwe jinsi ya kufuga mifugo kwa manufaa ya biashara. Isiwe tu kwamba tunafuga mifugo kisha kiangazi kikianza, tunarudi kuwa masikini.

"Kuuza mifugo wakati wa mvua na kuwekeza fedha ili kujinusuru wakati wa kiangazi itasaidia pakubwa katika kuhakikisha kwamba ukame unasalia kuwa historia".

Kwa mujibu wa mtazamo kuhusu uwepo wa chakula cha kutosha kwa Kenya 2019 , baadhi ya maeneo ya mashariki, kaskazini na kaskazini magharibi mwa Kenya ambapo kuna jamii za wafugaji, huenda zikakabiliwa na mzozo wa uhaba wa chakula.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii