Uhusiano wa Kenya na Iran wakumbwa na songombingo

Ahmad Abolfathi na Seyyed Mansour Mousavi Haki miliki ya picha AFP

Uhusiano kati ya taifa la Kenya na Iran umeathirika baada ya wizara ya kigeni nchini Iran kuwasilisha malalamishi rasmi kwa ubalozi wa Kenya nchini humo kufuatia hatua ya mahakama ya kilele kubatilisha uamuzi wa kuwaachilia huru raia wawili wa Iran waliokamatwa kutokana na tuhuma za ugaidi.

Inadaiwa kuwa mkurugenzi mkuu wa maswala ya Afrika katika wizara ya kigeni nchini Iran alimtaka balozi wa Kenya nchini Iran Rukia Ahmed Subow kufika mbele yake siku ya Jumamosi.

Msemaji wa taifa hilo katika wizara ya maswala ya Kigeni Bahram Qassemi alinukuliwa siku ya Jumapili akisema kuwa afisa huyo wa Iran aliwasilisha malalamishi hayo ya taifa lake huku wakimrudisha nyumbani balozi wake kwa majadiliano.

Msemaji huyo aliongezea kuwa balozi huyo wa Kenya alisema kuwa ataielezea serikali ya Kenya kuhusu pingamizi hiyo iliowasilishwa na taifa hilo la Kiislamu.

Siku ya Ijumaa mahakama ya kilele ilibatilisha uamuzi wa mahakama ya rufaa kuhusu kuwaaachilia watuhumiwa hao wa ugaidi Ahmad Abolfathi na Seyyed Mansour Mousavi waliokuwa wamefungwa miaka 15 baada ya kupatikana na hatia ya mashtaka matatu ya ugaidi.

Haki miliki ya picha UHURU KENYATTA / FACEBOOK

Mwaka 2016, jaji mmoja nchini Kenya alipunguza hukumu ya kifungo cha maisha waliopatiwa raia hao wawili wanaodaiwa kupanga mashambulizi ya mabomu hadi miaka 15.

Kesi hiyo ilizua hisia kuhusu mpango wa Iran kutaka kushambulia maeneo fulani katika taifa hilo la Afrika mashariki.

Ugaidi

Wawili hao walikamatwa mnamo mwezi Juni 2012 na kuhukumiwa mwaka mmoja baadaye kwa kupanga njama za kutekeleza mashambilizi mbali na kumiliki kilo 15 za vilipuzi vya RDX.

Kulingana chombo cha habari cha AP, maafisa nchini Kenya walisema kuwa maajenti hao wa Iran walilenga kushambulia maeneo yanayomilikiwa na Israel, Marekani , Uingereza na Saudia nchini Kenya.

Cha kushangaza ni kwamba siku moja tu baada ya kukamatwa kwao, ubalozi wa Marekani jijini Nairobi ulionya kuhusu uwezekano wa shambulio la kigaidi mjini Mombasa na kuwataka raia wake kuondoka mara moja mjini humo hadi tarehe mosi mwezi Julai.

Kenya imekuwa ikipata usaidizi kutoka kwa mashirika ya kimataifa kama vile FBI na polisi wa Kimataifa Interpol katika kukabiliana na tisho la usalama.

Mmoja wa watuhumiwa hao alisema mahakamani kwamba alihojiwa na kuteswa na maajenti wa Israel akiwa kizuizini madai yaliopingwa na Polisi wa Kenya.

''Wawili hao walitarajiwa kuachiliwa kabla ya mahakama hiyo ya Kenya kubatilisha uamuzi huo siku ya Ijumaa'', alisema Qassemi said.

Uhusiano wa kibiashara

Katika kipindi cha miaka kadhaa iliopita , taifa la Iran limeonekana kufanya juhudi kuimarisha ushawishi wake katika eneo la Afrika mashariki hususan nchini Kenya, ambapo serikali yake inatarajia uwekezaji mkubwa.

Mwaka 2009, wakati wa ziara ya aliyekuwa rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad nchini Kenya , taifa hilo lilitia saini makubaliano 13 kati yake na Kenya.

Iran ilikubali kuipatia Kenya mkopo wa dola bilioni 16 kuimarisha sekta za nyumba, ujenzi wa mabwawa, matibabu na usaidizi wa kibinaadamu.

Hatahivyo kiwango cha biashara kati ya mataifa hayo mawili kimeonekana kupendelea sana Iran.

Kati ya mwaka 2007 na 2009, kiwango cha biashara cha Iran kilifikia shilingi bilioni 19 huku Kenya ikipeleka Iran mali ilio na thamani ya shilingi milioni 613 pekee.

Mji wa Mombasa ambao ndio wa pili kwa ukubwa nchini Kenya na eneo lenye wakaazi wengi wa Kiislamu , ndio unaolengwa sana na uwekezaji wa Iran.

Katika sherehe iliohudhuriwa na maafisa wakuu wa Kenya na Iran mwaka 2011, Mkurugenzi wa bandari ya Iran alisisitiza kuhusu umuhimu wa bandari ya Mombasa kama kiingilio rahisi cha soko la Afrika.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii