Amnesty International: Marekani inawauwa raia wasio na hatia Somalia

Wanajeshi wa Marekani

Majeshi ya Marekani yanayoendesha mashambulizi ya angani nchini Somalia dhidi ya ngome za wapiganaji wa Al Shabab nchini humo yamelaumiwa kwa madai ya kuwaua raia katika mashambulizi hayo.

Amnesty International linasema kuwa katika mashambulizi matano iliochunguza , watu 14 waliuawa na wengine saba kujeruhiwa. Hatahivyo Marekani imekana kwamba raia waliuawa katika operesheni hizo mbili.

Lakini kulingana na afisa wa shirika la Amnesty International Seif Magango mashambulizi hayo yaliwalenga raia wasio na hatia ambao walikuwa wakiendelea na shughuli za kawaida na ambao hawakuwa na uhusiano wowote na kundi la al-Shabab.

Magango amesema kuwa mashambulizi hayo yalifanyika katika jimbo la Lower Shebelle katika mitaa kadhaa ikiwemo Faraweis, Darusalaam na Ilimei.

Katika far aweis watu saba waliuawa ikiwemo wanawake na watoto huku wakulima watatu waliokuwa wakiendelea na shughuli zao za kilimo wakipigwa kombora na kuuawa papo hapo katika eneo la Darusalaam.

Haki miliki ya picha Getty Images

Afisa huyo amesema kuwa hali hiyo ilianza tangu rais Trump kutangaza kuwa jeshi lake litakuwa likitumia ndege zisizokiuwa na rubani kukabiliana na wapiganaji hao katika eneo hilo linalodaiwa kuwa na vita.

''Tangu rais Trump aingie madarakani kumekuwa na mashambulizi zaidi ya 100 na tunachouliza ni kwamba je ni watu wangapi watakaouawa itakapofika mwisho wa mwaka huu'', alihoji.

Lakini saa chache tu baada ya kutoa ripoti hiyo, Jeshi la Marekani limetoa taarifa yake likikanusha habari hizo na kusema kwamba kikosi cha AFRICOM kinazuia mauaji ya raia wasio na hatia wakati wa mashambulizi yake dhidi ya kundi la wapiganaji wa Al-Shabab.

Katika taarifa hiyo AFRICOM inasema kuwa lengo la mashambulizi yake ni kuwalinda raia wa Somalia dhidi ya ugaidi mbali na kuisaidia serikali ya Somalia kukabiliana na changamoto za kiusalama.

''Amnesty International ilitoa ripoti ikidai kwamba mashambulizi manane ya AFRICOM kati ya 2017 na 2018 yalisababisha vifo vya raia. Tunashukuru juhudi za Amnesty International kuturuhusu kuchangia katika ripoti hiyo kabla ya uchapishaji wake licha ya kwamba tunaamini kwamba sio ya ukweli, ilisema taarifa hiyo''.

''Tumechukulia madai ya mauaji ya raia na uzito mkubwa bila kutazama wanakotoka. Wakati wa utafiti wa ripoti yake , shirika la Amnesty International liliwasilisha madai 13 dhidi yetu mnamo mwezi Oktoba 2018 na Februari 2019. Uchunguzi wetu ulibaini kwamba hakuna shambulio hata moja la AFRICOM lilisababisha maafa ama majeruhi. Uchunguzi wetu ulihusisha mbinu za kijasusi ambazo haziwezi kutumiwa na mashirika yasiokuwa ya kijeshi'', iliongezea ripoti hiyo ya Marekani.

Kulingana na ripoti yake AFRICOM ilitekeleza mashambulio 110 nchini Somalia tangu mwezi Juni 2017 na kuweza kuwaua wapiganaji 800.

Imesema kuwa mashambulizi ya kikosi hicho hutekelezwa katika maeneo yasio na idadi kubwa ya watu na kwamba inazingatia sheria ya vita vya silaha huku ikitilia mkazo tahadhari ili kuzuia maafa ya raia wasio na hatia.

AFRICOM imedai kwamba kundi la alshabab ndilo ambalo limekuwa likitoa taarifa za uongo na uchochezi kuhusu mauaji ya raia mbali na kuzirai jamii fulani kutoa taarifa za uongo dhidi ya mashambulizi yanayotekelezwa na Marekani.

''Kundi la wapiganaji wa Alshabab na lile la ISIS nchini Somalia yamekuwa na historia ya kuweka wapiganaji wake na vifaa vyao katika maeneo yalio na idadi kubwa ya raia ili kuficha vitendo vyao. Hivyobasi AFRICOM huchunguza maeneo inayolenga ili kuhakikisha kuwa ni wapiganaji wa al-Shabaab na wenzao wa ISIS wanaolengwa''.

Ripoti hiyo imeongezea kuwa AFRICOM hufanya uchunguzi wa ziada ili kuhakikisha kuwa malengo ya kikosi chake yanaafikiwa na kwamba hakuna raia anayeuawa.

Imesema kuwa shinikizo dhidi ya makundi hayo ya wapiganaji kwa ushirikiano wa serikali ya Somalia na vikosi washirika zimesaidia kuimarisha usalama wa raia wa Somalia.

Kulingana na AFRICOM ndani ya kipindi cha miaka miwili iliopita vikosi vya Somalia vimekomboa eneo moja karibu na mji wa bandari wa Kismayu kuelekea sehemu za juu za jimbo la mto Juba, na hivyobasi kuwaruhusu zaidi ya watu 1000 walioachwa bila makao kurudi nyumbani na kusababisha kuimarika kwa uchumi na uthabiti wa maisha.

Lakini shirika la Amnesty International linasema kuwa lina ushahidi wa kutosha kuthibitisha uchunguzi wake.

Shirika hilo la haki za kibinaadamu linadai kwamba visa kama hivyo vinaweza kuorodheshwa miongoni mwa visa vya uhalifu wa kivita.

Limesema kuwa familia za waathiriwa pamoja na jamii hazina njia za kuripoti visa kama hivyo .

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii