DR Congo: Maafisa wa serikali wadaiwa kuhusika na mauaji ya Yumbi

Upigaji kura katika eneo la yumbi uliahirishwa p[amoja na maeneo mengine mawili kaskazini mwa Kivu Haki miliki ya picha AFP

Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imekiri kwa mara ya kwanza kwamba maafisa wa serikali walitumika katika mauaji ya mamia ya watu mwezi Disemba mwaka jana.

Takriban raia 535 waliuawa kati ya tarehe 16 na 17 mwezi Disemba katika vijiji vitatu vya Yumbi , eneo la mashambani magharibi mwa DR Congo ukingoni mwa mto Congo yapata kilomita 350 kaskazini mwa Kinshasa.

Mauaji ya kikabila yalifanyika kwa siri kubwa mara ya kwanza kwa sababu yaliendeshwa siku kadhaa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa urais.

Siku kadhaa zilipita na habari zikaanza kuchipuka na ilichukua takriban mwezi mmoja kabla ya kiwango cha muaji hayo kubainika.

"kile kilichotokea katika eneo la Yumbi mnamo mwezi Disemba sio kitu cha fahari kwa taifa langu'', alisema waziri wa mashirika ya haki za kibinadaamu nchini DRC Marie-Ange Mushobekwa ambaye kwa sasa yuko mjini Geneva.

"Wanasiasa na maafisa wa utawala walihusika katika mauaji hayo , na kusababisha ndoto mbaya tunayozungumzia kwa sasa," alisema Mushobekwa akidai kwamba mauaji hayo yanahusishwa na mzozo wa ardhi.

Mauaji yalifanyika lini?

Mauaji hayo yalihusisha kukatwa mapanga kwa wanawake wajawazito pamoja na kunyofolewa sehemu zao za siri, alisema.

Waziri huyo alikuwa akizungumza katika mkutano wa baraza la Umoja wa mataifa kufuatia kuchapishwa kwa ripoti ya Uchunguzi wa Umoja wa mataifa mnamo tarehe 17 hadi 26 mwezi Januari.

Matamshi ya waziri huyo yanajiri huku wanaharakati wa haki za kibinaamu nchini humo wakishinikiza kuwasilishwa mahakamani kwa watuhumiwa wa mauaji hayo haraka iwezekanavyo.

Mwanaharakati wa haki za kibinaadamu Jean Claude Katende anasema kuwa mashirika hayo yanataka kujua ni akina nani waliohusika kupanga mauaji hayo upande wa serikali pamoja na upande wa raia.

''Tunataka kujua kwa nini walifanya hivyo hatujui walitaka kuzuia uchaguzi ama sijui kwa malengo yapi. Kwa sasa tunasubiri ripoti ya makundi ya haki za kibinadamu juu ya mauaji hayo'', alisema bwana Katende

Je mauaji hayo yaliopangwa?

Wakati wanahabari wa shirika la AFP walipotembelea eneo hilo baadaye mwezi Januari, duru ziliarifu kuwa mauaji hayo yalikuwa yamepangwa kwa siri na watu wa jamii ya Batende dhidi ya watu wa jamii ya Banunu.

Shambulio hilo lilitekelezwa kwa matumizi ya mbinu za kijeshi huku washambuliaji wakionekana kuvaa magwanda ya kijeshi , kulingana na vyanzo hivyo vya habari.

Duru hizo ziliwatuhumu baadhi ya maafisa wa jeshi na maafisa wa utawala wa eneo hilo katika mauaji hayo.

Baada ya umwagikaji huo wa damu, serikali iliwabadilisha maafisa waliokuwepo ikiwemo maafisa wa polisi na wakuu wa ujasusi , wanajeshi na maafisa wa serikali ya Utawala.

Wachunguzi wa Umoja wa mataifa UN wiki iliopita walisema kuwa wamegundua kwamba visa vya kufanana vya ghasia vilitokea baada ya mazishi ya chifu wa utamaduni wa jamii ya banunu.

Ripoti hiyo ilielezea visa vya kutisha ikiwemo kisa cha mtoto wa miaka miwili aliyetupwa katika shimo la maji taka huku mwanamke mmoja akibakwa baada ya mumewe kuuawa huku mtoto wao wa miaka mitatu akikatwa mikono.

Uhalifu wa kivita

Shambulio hilo linaweza kuorodheshwa miongoni mwa mashtaka ya uhalifu wa kivita ,kulingana na wachunguzi hao.

Uchunguzi huo hatahivyo ulishindwa kubaini iwapo serikali ilihusika na mauaji hayo.

Lakini jukumu la serikali linahusishwa baada ya uchunguzi huo kubaini kwamba utawala wa kitaifa na ule wa mkoa ulionywa kuhusu hatari ya ghasia hizo lakini haikuchukua hatua zozote za kuzuia kitendo hicho, ulisema uchunguzi huo.

Mushobekwa alisema kuwa rais mpya wa DR Congo Felix Tshisekedi , aliagiza uchunguzi kuhusu kile kilichotokea na ripoti yake itatumwa kwa Umoja wa Mataifa katika kipindi cha siku chache zijazo.

"Wale waliotekeleza mauaji haya watakamatwa na kuwasilishwa mahakamani ili kujibu majukumu yao. Tunajua kwamba bila haki hakutakuwa na amani ya kutosha nchini DR Congo''.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii