Dini: Je wakati umewadia kwa serikali kudhibiti mashirika ya kidini?

Duara ya nuru kichwani inatokana na sanaa ya zama zile - zamani ilitumiwa katika michoro ya mungu wa jua (Apollo, au Sol Invictus) lakini iliongezwa kwenye kichwa cha Yesu kuonesha utakatifu na utukufu wake Haki miliki ya picha Alamy

Masuala ya imani ama dini mara nyingi yanachukuliwa kuwa ya kiroho- Hivyo basi kila mtu ana uhuru wa kuchagua njia ya kuabudu, sehemu ya kuabudu na kupitia dini gani.

Lakini swali ni je uhuru uliyopo wa kuabudu umepita kiasi?

Swali hili limeibuka kutokana na visa kadhaa ambapo waumini wamedaiwa kutapeliwa ama kutumiwa vibaya katika maeneo ya ibada.

''Suala la kudhibiti dini ama madhehebu mbali mbali ni suala muafaka kwa sababu duniani kitu ambacho hakidhibitiwi kinaacha pengo ambalo watu wabaya wanatumia kufanya maovu.

''Tumeshuhudia visa vya matapeli kuingia katika makanisa, wengine wamejiita mapastor ambapo wanafanya vituko vya kila aina.'' anasema mmoja mmoja wa msikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC mjini Kampala Uganda.

Haki miliki ya picha Thinkstock

Kutokana na kauli kama hizi BBC iliamua kulivalia njuga suala hili kwa kuzungumza na baadhi ya viongozi wa kidini kutoka nchini Kenya na Tanzania kutathmini ikiwa wazo hilo linaweza kuzingatiwa.

''Ni vyema kufahamu dini ilikujaje, kwani bila ya kujua historia ya dini tutakuwa tunajichanganya'' alisema mchungaji Osward Mlay ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano nchini Tanzania.

Aliongeza kuwa wakati dini ilipokuja ilikuwa inamlenga Mungu na ufalme wake.

Watu waliyokuwa wanafuata dini walikuwa wanafanya hivyo kiasi cha kuwa utadhani wanamuona Mungu isipokuwa ile sura yake.

Ndio maana watu walikuwa wanaishi kulingana na mafundisho ambayo mtu anahisi ni kama anamuona Mungu japokuwa hajamuona.

Mchungaji- Osward Mlay anasema kuwa siku hizi mambo yamebadilika.

Haki miliki ya picha UNIVERSAL HISTORY ARCHIVE

''Yamekuwepo mafundisho ambayo hata ukiangalia unaona siyo ya Mungu'' anasema mchungaji Osward.

Anaongeza kuwa siku hizi baadhi ya viongozi wa kidini wanauza maji ambayo wanasema yana ''upako,hakuna mahali ambayo imeandikwa Yesu aliuza maji yakawa na upako.

Katika kila jamii kuna watu wa dini tofauti na wote wanaishi pamoja bila shida yoyote,lakini baadhi ya viongozi wanatumia uhuru wa kuabudu vibaya.

''Kama utatumia ibada kuwa kero kwa wengine utakuwa unamkosea Mungu manake hakusema tumtukuze kwa kuwaadhibu wengine''

Akizingatia hilo mchungaji Osward anasema serikali ina wajibu wa kuhakikisha watu wanaishi pamoja kwa amani bila kukwazana.

Haki miliki ya picha Getty Images

Serikali ya kidunia haiwezi kudhibiti uhuru wa kuabudu ambao umetolewa na Mungu.

''Sisi ndio tunajenga serikali ya kidunia kwa hivyo haina uwezo wa kutudhibitI'' anasema Dr. Hassan Kinywa Omary, mwanazuoni kutoka Kenya.

Akipinga kauli ya mchungaji Osward, Dr. Hassan anasema Kenya kwa mfano kuna mamilioni ya watu wa dini tofauti na kwamba maeneo mengi watu wanafuata kanuni zilizopo.

Anasema maeneo ya ibada ambayo watu wanakera wengine au kuwahadaa wenzao ni machache sana.

''Maeneo mengi ni yale watu wanafuata mambo ambayo ni ya haki, lakini sasa tunasema kuwa serikali iko na uwezo wa kuwachukulia hatua wale ambao hawafuati utaratibu uliyowekwa na sheria.''

Bwana Hassan anasema si vyema kutumia mfano wa mtu mmoja kuwalaumu wengine.

Uhuru wa kuabudu na uhuru wa kujidhibiti ni jukumu la dini na madhehebu mbali mbali lakini changamoto zinazokabili makundi haya ya kidini ni kuwa kuna watu wengine wanaojificha miongoni mwao.

Ili kukabiliana na tatizo hilo makundi ya kidini nchini Kenya yana mpango wa kuwasilisha mswada bungeni kushughulikia suala hilo.

Hata hivyo viongozi hao wote wawili wanaafikiana kuwa ipo haja ya serikali na makanisa kukaa meza moja ili kutafuta suluhisho la kudumu.

Mwaka jana bunge la Rwanda liliidhinisha sheria ya kudhibiti mashirika ya kidini ilikukabiliana visa vya watu kutumia mashirika hayo kujinufaisha.

Je mataifa mengine ya Afrika pia yafuate mkondo huo?

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii