Trump: Ni wakati kutambua kuwa milima ya Golan inamilikiwa na Israel na sio Syria

Picha inawaonyesha wanajeshi wa Israel wakipiga doria katika milima hiyo. Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Milima ya Golan ina umuhimu wa kisiasa

Rais Donald Trump amebadilisha sera ya miongo kadhaa ya Marekani kwa kusema kuwa ni wakati kuitambua Israel kama mmiliki halisi wa milima ya Golan ambayo iliiteka kutoka kwa Syria 1967.

Katika chapisho la Twitter , bwana Trump alitangaza kwamba milima hiyo ni muhimu sana katika usalama wa Israel na uthabiti wa eneo la mashariki ya kati.

Israel iliunganisha milima hiyo na taifa lake hatua ambayo haikuungwa mkono na jamii ya kimataifa.

Syria ambayo imekuwa katika harakati za kuikomboa milima hiyo haijatoa tamko lolote.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye ameonya kuhusu Iran kuingilia vita vya Syria alituma ujumbe wa shukran kwa bawana Trump kupitia mtandao wa twitter.

''Katika wakati ambapo Iran inataka kuitumia Syria kama eneo la kuikabili Israel, Bwana Trump aliitambua Israel kama mmiliki rasmi wa milima ya Golan.

Richard Haass, afisa mwanadamizi katika wizara ya kigeni nchini Marekani ambaye ndiye rais wa baraza la uhusiano wa kigeni alisema kuwa hakubaliani na bwana Trump.

Alisema kuwa hatua ya kuitambua Israel kuwa mmiliki wa milima hiyo ni ukiukaji mkubwa wa azimio la Umoja wa Mataifa , ambalo linapinga unyakuzi wa eneo moja kupitia vita.

Uamuzi huo wa rais unajiri wakati ambapo Netanyahu anakabiliwa na ushindani mkali katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu tarehe tisa mwezi Aprili mbali na msururu wa madai ya ufisadi.

Mwaka 2017, bwana Trump aliitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kuagiza kuhamishwa kwa ubalozi wa Marekani katika mji wa Tel Aviv.

Uamuzi huo ulishutumiwa na Palestina ambayo inataka mashariki mwa Jerusalem kuwa mji mkuu wa taifa la Palestina na Umoja wa mataifa unataka kufutiliwa mbali.

Cha kushangaza kuhusu Trump

Je ujumbe wa twitter wa rais Trump uliwashangaza hata wandani wake wa karibu?

Vyombo vya habari vilivyokuwa vikisafiri na waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Mike Pompeo vilikuwa vikisubiri nje kwa waziri mkuu Netanyahu kusikia kutoka kwa viongozi wote wawili, wakati bwana Trump alipofanya uamuzi huo.

Wawili hao walichelewa sana mpaka wanahabari wakahisi kana kwamba walikuwa wakishindwa kutoa tamko la pamoja.

Lakini iwapo tangazo hilo liliwashangaza wengi , lilimshangaza zaidi bwana Netanyahu -Nimefurahi zaidi , ni maneno yake ya kwanza alipotoka.

Israel imepata uungwaji mkono katika ikulu ya Whitehouse na baadhi ya wanachama wa bunge la Congress kwa kuhoji kwamba Iran inaitumia Syria kama kambi ya kushambulia Israel huku milima hiyo ya Golan ikiwa eneo la mbele la Vita.

Lakini utambuzi huo haubadilishi chochote katika eneo hilo, Israel tayari ilikuwa imejihami vilivyo katika milima hiyo ikiwa na ushawishi mkubwa.

Hivyobasi wakosoaji wamesema kuwa hilo ni jaribio la wazi kumpiga jeki Netanyahu katika uchaguzi ulio na ushindani mkali.

Iwapo hilo ndio lengo basi ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa wanasema.

Bwana Trump ameunga mkono unyakuzi wa eneo fulani hivyobasi hana maadili kuilaumu Urusi kwa kutekeleza kitendo kama hicho katika eneo la Crimea nchini Ukraine.

Je milima ya Golan ina muhimu gani?

Eneo hilo liko yapata kilomita 60 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Syria na lina ukubwa wa kilomita 1,200 mraba.

Israel ililiteka eneo hilo kutoka kwa Syria mwisho mwisho wa vita vya mashariki ya kati , na kuzuia jaribio la Syria kulikomboa eneo hilo wakati wa vita vya 1973.

Mataifa hayo mawili yalikubaliana kuweka eneo lisilo na wanajeshi kati yao litakalopigwa doria na wanajeshi wa Umoja wa mataifa .Lakini bado mataifa hayo mawili yanasalia kuwa katika hali ya kivita.

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Syria haitakubali makubaliano ya amani na Israel hadi itakapoondoka katika milima hiyo

Mwaka 1981, bunge la Israel lilipitisha sheria ya usimamizi na umiliki wa milima hiyo ya Golan hatua ilioonyesha kulichukuwa na kuliunganisha eneo hilo na taifa lake.

Lakini jamii ya kimataifa haijatambua hatua hiyo na kusisitiza kuwa milima hiyo ya Golan inamilikiwa na Syria.

Azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilitangaza hatua hiyo kuwa haramu.

Miaka mitatu iliopita wakati aliyekuwa rais Barrack Obama alipokuwa afisini , Marekani ilipiga kura ya kuunga mkono azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likionyesha wasiwasi kuwa bwana Netanyahu hatorejesha milima hiyo kwa Syria.

Syria imekuwa ikisistiza kwamba haitakubali kuweka amani na Israel hadi pale itakapoondoka katika milima hiyo.

Mazungumzo ya mwisho ya amani yalioongozwa na Marekani mwaka 2000 yalivunjika huku Uturuki ikiingilia kati na kuanzisha mzungumzo hayo 2008 ambayo pia hayakufua dafu.

Kuna zaidi ya makaazi 30 ya Israel katika milima hiyo ya Golan ambayo ni nyumbani kwa raia 20,000.

Makaazi hayo yanatumbulika kuwa haramu chini ya sheria ya kimataifa , ijapokuwa Israel inapinga hilo.

Wakaazi hao wanaishi pamoja na raia 20,000 wa Syria wengi wao wakiwa Waarabu wa kabila la Druze ambao hawakutoroka wakati milima hiyo ilipotekwa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii