Athari za unyanyasaji wa watoto mtandaoni

Mitandao ya kijamii imekua ikiwadhalilisha watoto
Image caption Unafahamu namna ambavyo mitandao inavyowakatili watoto?

Kutokana na ongezeko la ukatili dhidi ya watoto katika nchi nyingi barani Afrika, nchini Tanzania , mashirika zaidi ya 40 yamekutana kutafuta mbinu za kukomesha udhalilishaji wa watoto nchini Tanzania.

Hatua hii inakuja wakati ambapo kuna ongezeko la watumiaji wa mitandao na watoto wakiwa miongoni mwao.

Katika kizazi cha sasa ambapo unakuta teknolojia imekuwa , si jambo la ajabu kukuta picha ya mtoto kwenye mitandao bila ridhaa yake.

Dr.Herzon Zakaria Onditi,mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es salaam amefanya utafiti juu ya unyanyasaji wa kwenye mitandao na kubaini kuwa si watoto wa Tanzania pekee wanaoathirika bali ni tatizo linaloikabili dunia kwa ujumla.

Takribani asilimia 42 ya watoto ambao ni sawa na watoto wanne kati ya kumi, wameonyesha kuwa wamewahi kuwanyanyasa wenzao kwenye mtandao.

Walifanya hivyo kwa kuwatumia ujumbe wa kuudhi au picha ambazo hazina staha.Na hao wanaofanya vitendo hivyo ni wale wanaowafahamu na wakati mwingine hawawafahamu.

Asilimia 60 ya watoto wameripoti kunyanyaswa katika mtandao.

Image caption Watoto wamekua wakidhalilishwa mitandaoni kwa kujua au kutokujua

"Kwa mfano kuna mtoto ambaye alikuwa na marafiki zaidi ya 500 ambao hawafahamu hivyo anaponyanyaswa huwa ni vigumu sana kusema alichofanyiwa hivyo unakuta anakaa kimya na kuumia moyoni na wengine unakuta wanaathirika kisaikolojia, katika mahusiano yao na familia au marafiki ,wanakumbwa na sonona ,wanaathirika kitaaluma na kushindwa kuwa makini katika kusoma na kujifunza" Onditi alieleza.

Mtafiti huyo aliongeza kuwa tafiti zinaonyesha athari za watoto kunyanyaswa katika mitandao ni kubwa zaidi ya kupingwa kofi, maana kofi mtu atasamehe na kusahau lakini mtandao utatunza kumbukumbu.

Kwa upande wa watoto ambao walihojiwa na BBC, kwa ridhaa ya Shirika la Utu wa mtoto, CDF, walisisitiza kuwa elimu dhidi ya unyanyasaji wa watoto ni muhimu sana kwa jamii. Wanaamini kuwa inawezekana kuna watu ambao wanawafanyia watoto unyanyasaji kwa makUsudi au bila kujua.

" Watoto wengi ambao wanaishi kwenye mazingira magumu wamekuwa wakipigwa picha zao ili wapatiwe msaada,jambo ambalo baadae mtu anaweza kuona kuwa anadhalilishwa badala ya kusaidiwa," mtoto wa kidato cha tano alieleza.Huku mwingine alisema,

"Watoto wamekuwa wakiadhibiwa kupitia mtandao,mfano unaweza kukuta video ya mtoto amefanya kitendo kibaya na inasambazwa kwenye mtandao na lengo linakuwa kama kuadhibiwa katika mtandao, wakati mtoto huyo angeweza kubadilika labda alifanya jambo hilo kwa sababu ya hali ya utoto,"mtoto mwingine alieleza.

Image caption Wataalamu wanasema ni muhimu kuomba ridhaa kabla ya kutumia picha za watoto mitandaoni

Daktari Katanta Simwanza ambaye mtaalamu wa masuala ya jinsia kutoka shirika la Plan international anasema unyanyasaji wa kijinsia uko katika wigo mkubwa haswa katika masuala ya mimba za utotoni,ufanyishwaji kazi katika mazingira magumu na unyanyasaji wa kijinsia vitendo vya kingono, kiuchumi, kisaikolojia.

"Ni vizuri kuvunja ukimya maana unyanyasaji mwingi uko kwenye vyombo vya habari, simu, intaneti na kwenye mitandao ya kijamii kwa ujumla, ili kuona namna gani unyanyasaji huo unaathiri afya ya mtoto.

Mtoto anayefanyiwa unyanyasaji kwanza anakuwa hana amani lakini pia hawezi kuzingatia vizuri masomo yake.

Hata serikali yenyewe inatoa muongozo hata wa kupiga picha tu, lazima mzazi awe ameridhia na mtoto pia.

Misri kuweka sheria kali zaidi katika mitandao

Mvulana wa Kenya atunukiwa na Mesut Ozil

Kuna watu ambao wamekuwa wakitumia picha cha watoto na kutumia bila ridhaa na hata kwa upande wa maadili.

''Bahati nzuri mimi ni daktari, na kwenye upande wa afya kuna miiko pia ya kutomdhalilisha .Unaweza kukuta mzazi anakubali mtoto wake apigwe picha ili apate msaada jambo ambalo si sahihi kwa mtoto mwenyewe.Ugonjwa ni siri ya mgonjwa.Kuna namna ambayo mtoto anapaswa kulindwa."Dr.Katanta aliongeza

Ni jukumu na wajibu wa wazazi kuwashauri na kuwasimamia watoto wao katika matumizi chanya ya simu na mitandao.