Shambulio Mali: zaidi ya wanakijiji 130 wa kabila la Fulani wauawa

Kijiji cha jamii ya Fulani nchini Mali Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jamii ya Fulani ni ya wafugaji

Zaidi ya watu 130 wameuawa na watu wenye silaha kwenye kijiji katikati mwa nchi ya Mali .Washambuliaji hao walikua wamevalia mavazi ya kijadi ya uwindaji.

Watu wenye silaha walikizunguka kijiji majira ya alfajiri kabla ya kuwashambulia watukatika makazi yao katika eneo la Ogossagou mjini Mopti.

Washambuliaji walikua wakiwalenga jamii ya Fulani ambao wanashutumiwa kuwa na uhusiano na wanamgambo.

Shambulio hilo lilijitokeza wakati mabalozi wa Umoja wa Mataifa walipokua nchini Mali kujadili ongezeko la machafuko nchini humo.

Ujumbe kutoka baraza la usalama la umoja wa mataifa ulikutana na Waziri mkuu Soumeylou Boubeye Maiga kuzungumza kuhusu ongezeko la vitisho kutoka kwa wapiganaji wa jihadi katikati mwa Mali.

Wanakijiji walishambuliwa kwa ''risasi na mapanga'', shirika la habari la Ufaransa, AFP limeeleza.

Mashambulizi ya Marekani yalaumiwa Somalia

Wanamgambo 66 wa al-Shabab wauawa na mashambulizi ya anga

Mashuhuda pia wameiambia AFP kuwa karibu kila nyumba ya kijiji hicho zilichomwa moto.

Meya wa kijiji jirani cha Ouenkoro,Cheick Harouna Sankare amesema mashambulizi hayo ni ''mauaji ya kikatili''.

Mapigano kati ya wawindaji na wafugaji wa jamii ya Fulani hutokea kwa kugombea ardhi na maji.

Wawindaji wa jamii ya Dogon huwashutumu jamii ya Fulani kuwa na mahusiano na wapiganaji wa jihadi .Jamii ya Fulani inadai kuwa Jeshi la Mali limewapatia silaha wawindaji ili wawashambulie.

Mwaka jana, mamia ya watu waliuawa kwenye mapigano kati ya Dogon na Fulani .

Siku ya Ijumaa, Kundi la nchini Mali lenye uhusiano na al-Qaeda limesema lilifanya mashambulizi juma lililopita katika ngome ya kijeshi na kuwaua wanajeshi zaidi ya 20.

Wanamgambo wanasema shambulio hilo dhidi ya jamii ya Fulani lilikua la kisasi baada ya mashambulizi dhidi ya wanajeshi.

Mada zinazohusiana