ACT-Wazalendo yasema Dola inataka kuifuta ACT

Zitto
Image caption Kiongozi wa ACT -Wazalendo Zitto Kabwe

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe amesema barua ya msajili wa vyama vya siasa haina nia njema kwa chama chake na kudai kuwa ilivujishwa makusudi na ofisi ya msajili kutimiza dhamira ovu waliyonayo dhidi yao.

''Ni wazi serikali imetishwa na wimbi hili la watu kujiunga na ACT kwa mamia na maelfu.CCM wameshikwa na mchecheto kwamba watanzania sasa wamepata chama cha kisiasa walichokuwa wakikililia kwa muda mrefu na sasa wako tayari kupigania mabadiliko waliokuwa wakiyalilia kwa muda mrefu''.Alisema Zitto.

Chama hicho kimedai kuwa Barua ya msajili wa vyama vya siasa iliyodai kuwa ACT imekiuka sheria ya vyama vya siasa kwa kutopeleka kwake hesabu zilizokaguliwa mwaka 2013/2014 kama sheria inavyotaka ni tuhuma zisizo na ukweli kwa sababu wajibu wa chama cha siasa ni kuwasilisha hesabu zake kwa mkaguzi wa hesabu za serikali, hesabu ambazo ziliwasilishwa.Kilichotokea ni kuwa chama kilianzishwa na kupata usajili wa kudumu tarehe 5.5.2014 miezi miwili kabla mwaka wa fedha kuisha.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania umekipa chama cha ACT-Wazalendo wiki mbili kujitetea kwa nini wasifutiwe usajili wao wa kudumu.

Wiki moja iliyopita, kundi la viongozi kutoka chama cha CUF wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad walijiunga na ACT baada ya mgogoro wa muda mrefu wa madarka ndani ya CUF.

Machi 18, Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam ilimthibitisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF, hali iliyopelekea Maalim Seif na washirika wake kukihama chama hicho.

Toka hapo, mamia ya wanachama na wafuasi wa CUF hususani katika visiwa vya Zanzibar wamekuwa wakijiunga na ACT, na chama hicho sasa kuonekana ni ngome mpya ya upinzani.

Kwa mujibu wa barua kutoka ofisi ya msajili, vitendo vilivyotokea wakati wa hama hama hiyo ni miongoni mwa sababu za kutoa kusudio la kukifungia chama cha ACT.

"...kumezuka vitendo vya uvunjifuwa Sheria ikiwemokuchoma moto bendera za chama za CUF, vinavyofanywa na mashabiki wa Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, ambao wanadai sasa ni wanachama wa ACT-Wazalendo. Kitendo cha kuchoma moto bendera ya chama cha siasa ni kukiuka kifungu cha 11C cha Sheria ya Vyama vya Siasa," inasema sehemu ya barua hiyo.

Image caption Maalim Seif na viongozi wengine wa CUF wamepokelewa ACT wiki iliyopita

Msajili pia amedai kuwa kupitia mitandao ya kijamii, kuna video inayoonesha watu wakipandisha bendera ya ACT kwa kutumia tamko takatifu la dini ya Kiislamu (Takbira). Kitendo hicho, kwa mujibu wa msajili kinavunja vifungu 9(1)(c) na 9(2)(a) vinavyokataza kuchanganya shughuli za vyama vya siasa na dini.

Kwa mujibu wa barua, Machi 19 Msajili alitoa taarifa kwa umma kukemea vitendo hivyo: "Kitendo cha viongozi wa ACT-Wazalendo kutokemea kinaonesha kuwa chama chenu kimeafiki au kilielekeza vitendo hivyo kufanyika," barua ya Msajili imeeleza.

Sababu nyengine iliyotajwa na msajili ni ACT kushindwa kuwasilisha ripoti ya hesabu za fedha za chama kwa mwaka 2013/2014.

Utetezi wa ACT-Wazalendo

Image caption Kiongozi wa ACT Zitto Kabwe kuongea na wanahabari baadae leo Jumanne, Machi 26

Kiongozi wa ACT Zitto Kabwe ameiambia BBC Swahili kuwa hoja zote za msajili hazina mashiko na wataandika utetezi rasmi kama walivyotakiwa.

Zitto amesema sheria inawataka kuhakikisha wanachama wao hawavunji sheria na si watu baki, "...kama ilivyoandikwa kwenye barua ya Msajili, wale ambao wamefanya vitendo hivyo si wanachama wetu. Hatuna wajibu nao."

Kuhusu taarifa ya ripoti ya hesabu za chama kwa mwaka 2013/2014 Zitto amesema taarifa hizo zilijumuishwa kwenye hesabu za mwaka 2014/2015. "ACT ilianzishwa miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha (2014/15) kuisha, hivyo kiuhasibu na kama tulivyoshauriwa na Mkaguzi, tulijumuisha hesabu hizo za miezi miwili katika hesabu za mwaka uliofuatia 2014/2015."

ACT wanatarajiwa kuwa na mkutano wa dharura leo na baadae Zitto ataongea na waandishi wa habari kuanzia saa tano asubuhi.

BBC pia imeongea na mchambuzi wa siasa Tanzania Said Msonga ambaye amesema ACT kwa sasa inapitia wakati mgumu na kuna uwezekano wa mambo mawili kutokea, aidaha chama kishindwe kuvumilia vishindo na kusambaratika ama "kiive na kuwa moja ya nguzo za upinzani nchini. Ni kama mkate kwenye bekari tu wanaweza kuungua ama kutka wakiwa mkate ulio bora."

Hatua hiyo ya msajili pia imezua mjadala mtandaoni.

Mada zinazohusiana