Polisi jijini Dar es Salaam wazuia mkutano wa ACT-Wazalendo

POLISI Haki miliki ya picha ACT
Image caption Polisi wanadai kuna viashiria vya uhasama baina ya CUF na ACT

Chama cha ACT Wazalendo kimefanya mkutano wake makao makuu ya chama hicho baada ya kushindwa kufanya mkutano wao wa ndani wa chama hicho baada ya kuzuiwa na Polisi

Chama hicho, kinachoongozwa na Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe, kilikua kimepanga kufanya mkutano wake katika ukumbi wa PR uliopo Temeke jijini Dar es Salaam.

Jana Jumanne Zitto alitangaza kuwa wanachama wapya 12,000 walitarajiwa kupokelewa kupitia mkutano huo.

Katika mkutano huo Mwanachama namba moja wa ACT Wazalendo Maalim seif Shariff Hamad amesema ACT ni chama chenye muelekeo , ametupia lawama dola kuwa inataka kuendelea kuwepo madarakani

na kukihofia chama ambacho kinaonekana tishio kuwa kinaweza kuwaondoa madarakani.

Juzi Jumatatu, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania alikipatia notisi ya siku 14 chama cha ACT-Wazalendo ikieleza kususdio la kukifutia usajili wa kudumu chama hicho.

Wiki iliyopita, mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Maalim Seif Sharif Hamad na wafuasi wake walikihama chama cha CUF na kujiunga na ACT.

Hama hama hiyo imetokea baada ya Mahakama Kuu kumthibitisha hasimu wa Maalim, Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF.

Haki miliki ya picha ACT
Image caption Maalim Seif aitaka serikali kutenda haki

Kwa mujibu wa msajili, wafuasi wa Maalim Seif wamevunja sheria kwa kuchoma bendera za CUF na kutumia matamshi ya kidini wakati wa kupandisha bendera ya chama cha ACT. Pia chama hicho kimeshindwa kuwasilisha taarifa yake ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/14.

Madai yote hayo yamekanushwa na ACT na kusema "kuna nia ovu ya dola kukifuta chama hicho."

Image caption Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akikabidhiwa kadi za waliokuwa wanachama wa CUF

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, kamanda wa Polisi wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema wameuzuia mkutano huo baada ya kufanya uchunguzi na kubaini viashiria vya kutokea vurugu katika mkutano huo.

Mambosasa amedai viashiria hivyo vinatokana na uhasama baina ya CUF na ACT.

"Mkutano wa ndani hauhitaji maombi ya kibali, ila shida kipindi hiki cha mpito hivi vyama vya ACT na CUF kumekuwa na uhasama wa chini kwa chini, tumepata taarifa watu wa CUF walikuwa wamejipanga kufanya vurugu pale." Mambosasa amenukuliwa akisema na Mwananchi: "Kwa kuwa sisi hatukuwa na zuio, tukaona hatuna sababu ya kuacha watu wakavurugana na kuumizana. Kuna sintofahamu tukaona si kipindi sahihi za kuacha huu mkutano ufanyike kwa sasa."

Mada zinazohusiana