Namanga: Maandamano yakumba mpaka wa Kenya na Tanzania, kunani?

Mji wa Namanga uliopo kati ya mpaka wa kenya na Tanzania wakumbwa na vurugu

Maandamano yamekumba mji wa mpakani wa Namanga uliopo kati ya kenya na Tanzania.

Kulingana na maafisa wa polisi maandamano hayo yalizuka kufuatia kutekwa nyara kwa mfanyibishara mmoja wa Kenya ambaye waandamanji hao wanasema alipelekwa nchini Tanzania.

Mfanyikazi wa ofisi ya serikali katika mji huo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa waandamanaji hao waliojawa na ghadhabu walifunga barabara inayoelekea Tanzania na hivyobasi kukatiza uchukuzi kutoka na kuelekea nchini humo.

Anasema hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi wakati maafisa wa polisi wa Tanzania walipowasili karibu na ukuta unaogawanya Kenya na Tanzania ambapo waandamanaji waliingiwa na mori na kuanza kukabiliana na maafisa hao ambapo walirusha vitoa machozi .

Anasema kuwa Wakenya walitumia fursa ya upepo mkali uliokuwa ukielekea upande wa Tanzania ambapo waliokota na kurudisha vitoa machozi hivyo .

Wakati hali hiyo iliposhindwa kudhibitika , anasema, maafisa wa polisi walipiga risasi hewani kwa lengo la kuwatawanya waandamanaji hao kutoka Kenya.

Kulingana na afisa huyo maafisa wa Polisi wa Kenya wamekuwa wakipiga doria katika eneo hilo huku wakiwaomba waandamanaji hao kuwa watulivu.

Wakaazi waombwa kuwa watulivu

Mfanyibiashara huyo anayejulikana kwa jina Moha alidaiwa kuchukuliwa kutoka eneo analofanya kazi na gari lenya sajili za Tanzania.

''Tangu alipochukuliwa usiku uliopita hajaonekana'', alisema mmoja wa wakaazi wa eneo hilo Odinga Nguduu.

Akizungumzia kuhusu ufungaji wa barabara mkuu wa wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe alisema kuwa ni makosa kwa kundi lolote kusimamisha magari yanayovuka mpaka.

''Hiyo ni kinyume na sheria hivyobasi tutalazimika kutumia uwezo wa serikali kusitisha wazimu huu'', alisema.

Mwaisumbe aliwashauri wakaazi wa namanga kuwa watulivu huku serikali ikichunguza swala hilo.

''Hakuna haja ya vurugu kwa kuwa sasa tunachunguza swala hili tujue ni akina nani waliotekeleza kitendo hicho kwa lengo la kuweza kuwachukulia hatua kali za kisheria'', aliongezea.

Gazeti la The Citizen nchini Tanzania limeelezwa kwamba kamishna wa jimbo la Arusha Jonathan Shanni alizuru mji wa Namanga ili kuchunguza hali ilivyo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii