Kampuni ya Boeing yashtakiwa kwa ajali ya Shirika la Ndege la Ethiopia

Ethiopia Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mabaki ya ndege ya Ethiopia katika eneo la ajali.

Kampuni ya utengenezaji ndege ya Boeing imefunguliwa mashtaka nchini Marekani na familia ya moja ya abiria waliofariki kwenye ajali ya Shirika la Ndege la Ethiopia.

Watu wote 157 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walifariki katika ajali hiyo iliyotokea mapaema mwezi huu.

Ndugu wa Jackson Musoni, ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa na raia pekee wa Rwanda aliyekuwemo kwenye ajali hiyo, wanadai kuwa ndege sampuli ya Boeing 737 Max zinamapungufu ya kiusanifu katika mifumo yake ya kujiendesha.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ndege aina ya Boeing 737 Max za shirika la Southwest zikiwa zimeegeshwa uwanja wa ndege jimboni California baada ya kutolewa katazo la kupaa.

Ndege zote 371 zinazomiikiwa na mashirika mbalimbali za aina ya 737 Max zimepigwa marufuku kuruka toka ilipotokea ajali hiyo, ambayo ilikuwa ni ya pili kwa sampuli hiyo ndani ya miezi mitano. Ajali ya kwanza ilitokea mwezi Oktoba 2018 nchini Indonesia na kuua watu wote 181 waliokuwamo ndani.

Kampuni ya Boeing bado haijatoa tamko lolote kuhusu kesi hiyo.

Wachunguzi pia bado hawajatoa ripoti kamili juu ya sababu hasa ya ajali hiyo kutokea.

Boeing yatangaza maboresho

Juzi Jumatano, Boeing walitangaza kuwa wamefanyia marekebisho mfumo wa udhibiti (MCA) ambao unahusishwa na ajali zote mbili.

Kama sehemu ya kuboresha ndege hizo, Boeing itaweka mfumo wa onyo kulingana na viwango ,ambao awali ulikua si wa lazima.

Ndege zilizopata ajali za makampuni ya Lion Air ya Indonesia na Ethiopian Airlines, hazikuwa na mfumo wowote wa kuashiria ajali, ambao lengo lake ni kuwaonya marubani wakati mtambo wa uongozaji wa safari ya ndege unapotoa taarifa kinyume na matarajio.

Boeing imesema makampuni hayatakuwa yakitozwa pesa za ziada kwa ajili ya kuweka mfumo huo wa usalama wa ndege.

Lakini bado haijajulikana ni lini ndege hizo zilizozuwiwa kusafiri kote duniani mwezi huu zitaruhusiwa kupaa.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Boeing kukubali kuwa kulikuwa na mapungufu ya kiufundi kwenye ndege hizo. Awali mamlaka za Marekani zilitetea kampuni hiyo zikidai sampuli 737 Max ni salama.

Shinikizo kubwa la kimataifa dhidi ya ndege hizo lilianza mara tu baada ya ajali ya Ethiopia kutokea.

Shirika la Ethiopia lilifuta safari zake zote za ndege aina hiyo mara tu baada ya ajali.

Nchi kadhaa, ikiwamo za Jumuiya ya Ulaya, Canada, Uchina na Rwanda zilipiga marufuku ndege hizo kupaa kwenye anga za mataifa hayo.

Mikasa mibaya zaidi ya Ndege Afrika

Uraia wa waliofariki kwenye ajali ya Ndege Ethiopia

 • Kenya 32
 • Canada 18
 • Ethiopia 9
 • Italia 8
 • Uchina 8
 • Marekani 8
 • Uingere 7
 • Ufaransa 7
 • Misri 6
 • Ujerumani 5
 • India 4
 • Slovakia 4
 • Australia 3
 • Uswizi 3
 • Urusi 3
 • Wakomoro 2
 • Uhispania 2
 • Poland 2
 • Israeli 2
 • Ubelgiji 1
 • Indonesia 1
 • Somalia 1
 • Norway 1
 • Serbia 1
 • Togo 1
 • Msumbiji 1
 • Rwanda 1
 • Sudan 1
 • Uganda 1
 • Yemen 1

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii