Siasa Tanzania: Mahakama yaridhia mbunge wa Chadema Joshua Nassari kuvuliwa wadhifa wake ubunge

Joshua Nassari
Image caption Joshua Nassari

Mahakama Kuu kanda ya Dodoma nchini Tanzania 'imebariki' kuvuliwa ubunge kwa Joshua Nassari ambaye alikuwa mbunge wa Arumeru Mashariki kupitia chama cha upinzani Chadema.

Jaji wa mahakama hiyo, Latifa Mansour amekubaliana na uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kuwa Nassari amepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na utoro. (Arumeru Mashariki).

Wiki mbili zilizopita Machi 14, 2019 Ndugai aliiandikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) barua akiieleza kuwa Nassari amepoteza sifa ya kuwa mbunge baada ya kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo bila taarifa. Viakao alivyovikosa Nassari vilifanyika baina ya Septemba 2018 na Januari 2019.

Katika utetezi wake kabla ya kwenda mahakamani, Nassari alidai kuwa alikuwa nje ya nchi akimuuguza mkewe na kuwa aliwasiliana na Ofisi ya Spika kwa kuongea kwa simu na msaidizi wake pamoja na kutuma ujumbe kupitia barua pepe.

Baada ya hukumu ya leo, sasa NEC inatarajiwa hivi karibuni kulitangaza jimbo hilo kuwa wazi na kuandaa uchaguzi mdogo kujaza nafasi hiyo.

Swali miongoni mwa waangalizi wa siasa nchini Tanzania ni kuwa je upinzani utaweza kulitetea jimbo la Arumeru kwenye uchaguzi mdogo?

Ikumbukwe mpaka sasa upinzani tayari wameshapoteza majimbo 11 toka ulipofanyika uchaguzi mkuu wa 2015. Kati ya majimbo hayo, 11 yamepotea baada ya wabunge wake kuhamia chama tawala cha CCM wakisema wanaenda kumuunga mkono rais John Magufuli katika harakati za maendeleo.

Jimbo moja la Buyungu mkoani Kigoma liliondoka mikononi mwa upinzani kwenda CCM baada ya mbunge wa Chadema Mwalimu Kasuku Bilago kufariki dunia Mei 2018.

Katika uchaguzi mdogo wa kuziba pengo lake Agosti 2018, mgombea wa CCM Christopher Chiza aliibuka na ushindi.

Wabunge wa upinzani 'waliounga mkono juhudi'

Image caption Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania, John Magufuli akimkaribisha Edward Lowassa CCM mwezi uliopita

Mbunge wa kwanza wa upinzani kuhama upinzani kwa kigezo cha kuunga mkono juhudi za rais John Magufuli ni Maulid Mtulia wa Kinondoni.

Mtulia alitangaza kujiuzulu ubunge na kukicha chama chake cha CUF mwezi Disemba 2017. Wiki mbili baadae, Dkt Goodluck Mollel akajiuzulu ubunge wa Siha kupitia Chadema na kutangaza kujiunga na CCM.

Wawili hao waliteuliwa na CCM kutetea nafasi zao za ubunge mwezi Februari 2018 na kushinda. Huo ukawa ni mwanzo wa safari ya wabunge wa upinzani kujiuzulu na kurudi tena bungeni kupitia CCM.

Wabunge wengine waliokuwa upinzani na wakahama na majimbo yao ni James Ole Milya (Simanjiro-Chadema), Julius Laizer (Monduli-Chadema), Marwa Ryoba Chacha (Serengeti-Chadema), Zuberi Kuchauka (Liwale-CUF), Abdallah Mtolea (Temeke-CUF), Pauline Gekul (Babati Mjini-Chadema), Mwita Witara (Ukonga-Chadema) na Joseph Mkundi (Ukerewe-Chadema).

Hata hivyo, mbunge wa kwanza kuhama alikuwa wa Singida Kaskazini kupitia CCM Lazaro Nyalandu, lakini CCM waliweza kulitetea jimbo lao kwenye uchaguzi wa marudio.

Ubunge wa Zitto mashakani?

Image caption Endapo ACT-Wazalendo wanafutiwa usajili, Zitto Kabwe, atapoteza ubunge wake.

Jumatatu wiki hii, Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa nchini Tanzania iliiadikia barua ya notisi ya siku 14 ikitishia kuifutia usajili chama cha ACT-Wazalendo.

ACT inatuhumiwa kutowasilisha taarifa ya hesabu za maapato na matumizi kwa mwaka 2013/14 pamoja na kuvunja sheria ya vyama vya siasa kwa mujibu wa msajili ambapo watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa chama hicho kuchoma bendera za chama kingine cha upinzani CUF na kutoa matamshi ya kidini.

Japo ACT wanapinga madai hayo, kama msajili atakifutia usajili, mbunge pekee wa chama hicho Zitto Kabwe.

Mada zinazohusiana