Waandishi habari wa BBC na VOA hawaruhusiwi tena kutoa habari Burundi

BBC Haki miliki ya picha Carl Court

Mamlaka nchini Burundi imewapiga marufuku waandishi wa BBC na wale wa shirika la sauti ya Marekani VOA kutofanya kazi nchini humo.

Baraza la kitaifa la mawasiliano nchini humo lilisema kuwa halimruhusu mwandishi yeyote , akiwa raia wa Burundi ama yule wa kigeni kutoa habari yoyote kwa mashirika hayo ya habari.

Baraza hilo limeelezea kuwa uongo makala ya BBC mwaka uliopita kuhusu mauaji yaliotekelezwa na vikosi vya usalama katika nyumba ya siri ndani ya mji mkuu wa Bujumbura.

Mamalaka nchini Burundi imesema kuwa makala hayo yalikiuka sheria za habari nchini humo.

BBC imesisitiza kuwa inawaunga mkono waandishi wake.

Imeshutumu marufuku hiyo ikiitaja kuwa pigo kubwa dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.

''Tunaamini kwamba ni muhimu kwa watu duniani kuweza kupata habari zisizopendelea upande wowote , ikiwemo raia milioni 1.3 wa Burundi ambao hutegemea habari za BBC'', ilisema katika taarifa yake.

Matangazo ya BBC tayari yamesitishwa nchini Burundi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Lakini ikijibu uamuzi huo wa serikali ya Burundi, naibu mkiurugenzi wa shirika la Amnesty International tawi la Afrika mashariki, maziwa makuu na upembe wa Afrika Sarah Jackson amesema kuwa hatua hiyo ni hatua ya serikali ya Burundi kunyamazisha vyombo vya habari.

Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kukandamiza uhuru wa kujieleza ambao umedorora tangu kuanza kwa mzozo wa kisiasa mnamo mwezi Aprili 2015.

Amesema kuwa mamlaka ya Burundi inafaa kukoma kukandamiza vyombo vya habari na kurudisha matangazo ya BBC na VOA mara moja .

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii