Karibu katika ulimwengu wa BBC Swahili mpya

Waandishi wa BBC

Kwa miongo sita sasa Idhaa ya Kiswahili ya BBC imekuwa ikikuhabarisha, kukuelimisha na kukuburidisha kwa namna mbali mbali kupitia vipindi vyake maridhawa.

Katika kipindi chote hicho tangu Juni 27, 1957 BBC Swahili imeenda sawia na mabadiliko mbali mbali katika tasnia ya habari kwa ujumla wake. Tokea enzi za matangazo ya redio tu, mpaka sasa kukufikia kwa njia ya runinga, tovuti na mitandao ya kijamii.

Na sasa umewadia muda mwengine wa kufanya mabadiliko, ili kukufikia msomaji, msikilizaji na mtazamaji wetu kwa wepesi zaidi.

Mabadiliko yamefanyika kwa kiasi kikubwa kwenye maudhui na nama ya kuyawasilisha kwenye jamii.

Kwa nini mabadiliko?

"Dunia ya leo si sawa na ile ya ya mwaka 1957. Hivyo basi, msikilizaji wa leo na kesho si swa na yule wa jana na juzi," anaeleza Mhariri wa BBC Swahili, Odhiambo Joseph (OJ).

Kichocheo cha kwanza cha maboresho haya ni kukua kwa teknolojia, ambapo kumeleta mtazamo mpya na aina mpya ya 'walaji' wa habari.

"Sasa tunaenda kuiunganisha jamii ya mtandao na redio. Tuna wafuasi wengi kwenye mitandao yetu ya kijamii...tayari tumeshaanza kupeperusha matangazo mbashara kupitia mitandao ya kijamii (Facebook na Insta Live). Sasa tutaboresha zaidi kwenye eneo hilo ili tuwanase watumiaji wa mitandao hiyo, husasani vijana,"ameeleza OJ.

Kichocheo kingine ni kuongeza ubora wa habari zinazopeperushwa na kuangalia zaidi matokeo chanya. Mfano katika kuripoti habari za biashara, haitakuwa tu kuhusu soko la hisa ama faida na hasara katika mabenki - bali kwa kiasi kikubwa itakuwa namna gani ya kumhamasisha mtu katika namna ya kufikia malengo. Namna gani ya kusaka mitaji na kufanya biashara zenye tija.

Image caption Mhariri wa BBC Swahili Odhiambo Joseph

Pia sasa wasikilizaji wa vipindi vya Amka na BBC na Dira ya Dunia wanaenda kupata wasaa mkubwa wa kuwawajibisha viongozi wao. Juhudi za makusudi zimewekezwa katika kuongeza muda wa mijadala kwenye vipindi hivyo ambapo wananchi watapata wasaa wa kuwauliza maswali viongozi wao.

"Kwenye Amka na BBC kutakuwa na dakika 10 za mjadala. Hapo wananchi watapata muda wa kutosaha wa kuwawajibisha viongozi... mfano kumetokea mauaji Mbeya, tutaalika viongozi studio ama kupitia simu na wasikilizaji wa redio ama mtandaoni watauliza maswali yao na viongozi watawajibu," anafafanua OJ.

Kwa kuzingatia uhalisia wa kijana wa leo, BBC Swahili na redio washirika wanaboresha zaidi uwasilishaji wa habari kupitia kipindi cha Global News Beat (GNB).

"Kijana wa leo ni nadra kumpata kwa nusu saa nzima ama saa moja nzima, ndio maana kwa kupitia GNB tunapeperusha matangazo ya habari kwa lugha yao na kutumia dakika chache tena bila kupotosha maana."

Usipitwe na msafara wa BBC

Kwa wiki yote hii (Jumatatu mpaka Ijumaa 1-5 Aprili) watangazaji wako mahiri wa idhaa ya BBC Swahili watakuwa njiani kukutana na wewe uliyepo nchini Tanzania na Kenya.

Misafara ya waandishi hao itaanzia Dodoma, kupitia Morogoro, Kibaha na kuishia Dar es Salaam kwa upande wa Tanzania. Mombasa, Diani, Voi, Machakos mpaka Nairobi kwa Upande wa Kenya.

Njiani, utapata kushuhudia jinsi matangazo ya BBC Swahili yanavyopeperushwa, utawaona na kuongea na watangazaji pia kuna zawadi kemkem.

Usikubali kupitwa, kuwa sehemu ya mabadiliko.

Mada zinazohusiana