Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania asema nchi yake inafuata masharti ya kimataifa katika kusafirisha dola

Dola ya marekani Haki miliki ya picha SOPA Images

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amekanusha kuwa Tanzania ina masharti magumu ya kusafirisha dola na kusema nchi hiyo inafuata vigezo vya kimataifa.

Gavana huyo amebainisha kuwa masharti hayo yapo kisheria toka mwaka 1992.

Profesa Luoga na Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dk Philip Mpango leo Jumatatu Aprili Mosi, 2019 wameongea na waandishi wa habari juu ya ukaguzi wa maduka ya kubadilishia fedha za kigeni nchini humo.

"Kwa mfano unaposafirisha dola kutoka Tanzania inategemea unazipeleka wapi. Marekani huruhusiwi kuingiza zaidi ya dola 10,000 na ukipeleka Uingereza nacho kuna kiwango hicho hicho, ambacho huwezi kuruhusiwa kwenda nacho," Prof Luoga amenukuliwa akisema na Gazeti la Mwananchi.

Pesa ambayo unaruhusiwa kutoka nayo nchini Tanzaniani ile ambayo unaruhusiwa kuingia nayo katika nchi nyingine.

"Si kweli kwamba masharti ya Tanzania ni magumu bali masharti ya kila nchi unayokwenda ni magumu katika kubeba dola zako kupeleka kwako. Ukikutwa na dola 400, 000 kwa mfano swali ni kwamba utaenda kuingiza vipi kwenye nchi unayokwenda? Ambayo haitakuruhusu kuingiza zaidi ya dola 10,000."

Tokea mwishoni mwa mwaka jana, Tanzania imekuwa katika vita dhidi ya kile mamalaka inachokiita biashara haramu ya kubadili fedha za kigeni.

Awali mamlaka zilianzia katika mkoa wa Arusha ambapo maduka kadhaa ya kubadilishia fedha za kigeni yalifutiwa leseni.

Katika siku za hivi karibuni, maduka yanayofanya biashara hiyo jijini Dar es Salaam yamekumbwa na mpaka sasa mengi yao yamefungwa kwa kutokidhi masharti.

'Watakatisha fedha haramu'

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Serikali ya Tanzania inasema hatua zinazochukuliwa zinalenga kulinda thaman ya sarafu yake.

Katika mkutano huo, Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango amesema kuwa ukaguzi uliofanyika mpaka sasa umegundua kuwa maduka hayo yakitumika kinyume na sheria ikiwemo kutakatisha fedha haramu.

Amesema kutokana na shughuli hizo haramu, maduka hayo yamekuwa yakichangia katika kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola.

Kwa mujibu wa Mpango, maduka mengi yamebainika kutumia kiasi kikubwa cha shilingi ya Tanzania kununulia fedha za kigeni, lakini maduka hayo hayana rekodi shaihi zinazoonesha fedha hizo za kigeni walizitimia ama kuzichenji vipi na wapi.

Kutokana na hali hiyo, serikali ya Tanzania sasa imeandaa kanuni mpya ambazo zitaelekeza jinsi ya kuomba leseni za uendeshaji wa maduka hayo kwa mtu binafsi au taasisi yoyote na masharti yake.

"Kanuni hizo zinalenga kuweka mazingira mazuri ya biashara ambayo hayatatoa athari kwa sekta ya fedha na uchumi na badala yake inakuwa yenye manufaa kwa nchi," amesema.

Jijini Dar es Salaam pekee, takribani maduka 80 yamefungwa, na ili kuondoa usumbufu, serikali sasa inawataka wale wanaohitaji huduma hizo kwenda katika benki zote pamoja na Shirika la Posta.

Mada zinazohusiana