Kituo cha kurekebisha tabia ya wapenzi wa jinsia moja Zanzibar

Wapenzi wa jinsia moja wakishikana mikono

Mahusiano ya wapenzi wa jinsia moja katika nchi nyingi barani Afrika ni makosa kisheria na ukijulikana unaweza kufungwa jela hadi miaka 30.

Lakini ni watu ambao wapo katika jamii nyingi mbali na kuwa si suala linalojadiliwa sana.

Huko visiwani Zanzibar shirika moja lisilo la kiserikali linashugulika katika kuwabadilisha tabia na kuwapa msaada wa kiafya wanaume wanaojihusisha na mahusiano ya jinsia moja.

Shirika la IYAHIZA linahusika na mapambano ya virusi vya ukimwi kwa vijana visiwani Zanzibar na miongoni mwa miradi wanayoshugulikia ni kuwasaidi makundi maalum, ikiwemo wanaume wanaojihusisha na Mapenzi ya Jinsia Moja, ambapo shirika hili hujikita katika kuwapa msaada wa kiafya na Mabadiliko ya Tabia.

Mbinu mbalimbali hutumiwa, kwanza hufuatwa kisha kupewa ushauri na kupimwa ikiwa wana maambukizi ya magonjwa yoyote ikiwemo virusi vya Ukimwi.

Ingawa kundi hili limekua likijificha kutokana na kuwa hawaruhisiwa kisheria na wanaweza kufungwa hadi miaka 30 jela, imekua vigumu kwa Shirika la IYAHIZA kuwapata hivyo wamekua wakitumia mbinu ya kutumia wale walioacha ili kuwatambua ambao bado wanajihusisha na vitendo hivyo.

''Huwa tunawapata mara nyingi kwa kuwatumia wale EX ambao wao wameacha kabisa, kisha tunawapatia ushauri wa namna ya kuacha mana wao wapo katika hatari zaidi ya kupata magonjwa, kwanza wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja lakini pia wanaweza kuwa wanajihusisha na jinsia nyingine kwa wakati mmoja kwa hivyo hatari inakua kubwa zaidi'' anasema Sabra Mosi Afisa Mradi wa shirika hilo.

Baadhi ya vijana wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja wanasema kuwa shirika hili limewasaidia sana kubadilisha mwenendo wa maisha yao.

''kwana zamani sikua najua masuala ya kupima afya yangu, sikua naona umuhimu wowote, lakini sasa naona nimebadilika na nataka pia kuacha niwe kijana wa kawaida, mana nilikua nadharaulika sana'' anasema kijana mmoja ambae jina lake tumelihifadhi kutokana na usalama wake.

Kijana mwingine ambae ameacha kabisa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, anasema kuwa yupo tayari kuanzisha familia.

''ilinichukua muda kiasi hadi kuacha kabisa, sasa nimeacha kabisa , siwezi tena kurudia vitendo hivi, ni utoto ndio ulisababisha, na nilikua nikidharauliwa hata mtoto mdogo ana thamani, sasa nataka nitafute mke nioe, nianzishe familia yangu''.

Haki miliki ya picha DEA / G. COZZI

Lakini vijana hawa ilikuaje hadi wakaingia katika mapenzi ya jinsia moja?

Vijana ambao wapo katika mradi huo, wengi wanasema kuwa waliingia katika tabia hiyo kutokana na ushawishi wa vijana wenzao.

Lakini kijana mmoja ambae jina lake limehifadhiwa anasema kuwa shemeji yake ndiye aliyekua akimfanyia vitendo hivyo.

''Nilikua naishi na dada yangu, aliyeolewa huko mkoani mwanza, sasa shemeji alikua akinifanyia vitendo hivi mara kwa mara, alikua akiniingilia kinyume na maumbile, na ananiambia nisiseme kwa mtu yoyote, mimi nilikua naogopa, sasa ikaendelea hadi nikazoea, nilikuja kusema nyumbani nikafukuzwa''

Mbali na kuwa shirika hili linataoa msaada wa kiafya na mabadiliko ya tabia, wamesisitiza kuwa hawashawishi kwa namna yoyote watu kujihusisha na vitendo hivyo.

Mapenzi ya jinsia moja miongoni mwa wanaume ni kosa la jinai nchini Tanzania na hatia yake inaadhibiwa kwa kifungo cha kati ya miaka 30 au maisha jela.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii