CAG Prof Mussa Assad aonya mzozo wake na Bunge kuzaa mgogoro wa kikatiba

Profesa Mussa Assad Haki miliki ya picha NAOT
Image caption Profesa Mussa Assad ametiwa hatiani na Bunge katika tuhuma za kuwa ameudharau mhimili huo.

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad leo amezungumzia mgogoro baina yake na Bunge na kusema unaweza kuzaa mgogoro wa kikatiba.

Jana Bunge la Tanzania lilipitisha azimio la kutokufanya kazi na CAG baada ya kumtia hatiani kwa tuhuma za kudharau chombo hicho.

Wabunge wamefikia uamuzi huo baada ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutaka waridhie mapendekezo yao dhidi ya CAG.

Kamati hiyo ilimhoji CAG Januari 21 baada ya kufanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York mwezi Disemba 2018 ambapo alisema kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.

Akizungumza na shirika la habari la TBC asubuhi leo amesema suala hilo linaweza kuwa kubwa kuliko lilivyo sasa. Prof Assad ametoa rai kuwa busara itumike zaidi ili kupata ufumbuzi.

"Tunaweza kuwa na mgogoro wa kikatiba, kwamba ripoti (za ukaguzi wa mwaka 2017-18) zimeshawasilishwa kwa Raisi na mimi siwakilishi ripoti Bungeni, basi raisi atazipeleka ndani ya siku sita zijazona kama Bunge likikataa kuzipokea hiyo ni tatizo kubwa zaidi. Ni dharau (kwa katiba)wasiwasi wangu ni huo. Zikiwasilishwa bungeni zinakuwa mali ya umma na mimi napata nafasi ya kuzungumza, na hilo pia linaweza kuwa tatizo. Tafsiri ya kuwa (Bunge) hatuwezi kufanya kazi na CAG ni tafsiri pana sana na inatakiwa tuijue vizuri," amesema Prof Assad.

Alioulizwa endapo anaweza kuchukua 'uamuzi mgumu' , Prof Assad amesema, "hana maamuzi ya kufanya zaidi ya kuomba dua watu waongoze vizuri na wafanye maamuzi yenye faida na nchi hii, basi."

Prof Assad amesema pia ataendelea kutekeleza majukumu yake kama ilivyoainishwa kwenye katiba.

Haki miliki ya picha BUNGE
Image caption Spika Job Ndugai aliagiza CAG ahojiwe mwezi Januari akidai kuwa amelidharau Bunge

Mgororo uliopo ulianza Disemba 2018 baada ya CAG kuiambia Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.

"…Kama tunatoa ripoti na inaonekana kuna ubadhilifu halafu hatua hazichukuliwi huo kwangu mimi ni udhaifu kwa Bunge. Bunge linatakiwa liisimamie (serikali) na kuhakikisha kuwa pahali penye matatizo basi hatua zinachukuliwa...Sie kazi yetu ni kutoa ripoti tu na huo udhaifu nafikiri ni jambo la kusikitisha lakini ni jambo tunaamini muda si mrefu huenda likarekebishika. Lakini tatizo kubwa tunahisi kwamba bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa," Profesa Assad aliiambia radio ya UN.

Spika Job Ndugai alilieleza Bunge mwezi Januari kuwa maelezo ya Assad yalioonesha dharau kubwa dhidi ya mhimili huo na kumtaka aende mbele ya kamati kwa hiyari yake, ama apelekwe kwa pingu.

'Nasimama na CAG'

Watumiaji wengi wa mitandao nchini Tanzania wameonekana kumuunga mkono Profesa Assad kwa kauli miu ya Nasimama na CAG ama kwa kimombo I stand with CAG.

Kambi ya upinzani bungeni pia imeweka wazi kuwa inaungana na CAG.

Kiongozi wa Upinzani Bungeni Freeman Mbowe jana Bunge kuwa hatua hiyo dhidi ya CAG ni kuminya mawazo ya watu.

"Mnataka kuwanyima watu haki na uhuru wa mawazo ilhali Katiba imeruhusu kila mtu, akiwamo CAG ana uhuru wa kutoa mawazo na kueleza fikra zake, kufanya mawasiliano na kutoingiliwa kuhusu taarifa yake...Kamati hii ya maadili haiwezi kutenda haki dhidi ya watu wanaoibua hoja zinazoonekana kutoifurahisha serikali," amesema Mbowe.

Kumwondoa kazini CAG

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, CAG huondoka madarakani baada ya kufikisha umri wa kustaafu ama kujiuzulu wadhifa wake.

Ibara 144 ya katiba pia inasema CAG anaweza kuondolewa katika madaraka ya kazi yake kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake (ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote) au kwa sababu ya tabia mbaya, au kwa kuvunja masharti ya sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo, kuna utaratibu maalumu wa kumwondoa ambapo ibara ya 144 (3) inabainisha kuwa iwapo rais ataona kwamba suala la kumwondoa kazini CAG lahitaji kuchunguzwa, basi atateua Tume Maalum ambayo itakuwa na Mwenyekiti na Wajumbe wengine wasiopungua wawili.

Mwenyekiti na angalau nusu ya wajumbe wengine wa tume hiyo itabidi wawe watu ambao ni Majaji au watu waliopata kuwa Majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote iliyomo kwenye Jumuiya ya Madola.

Iwapo Tume itamshauri rais kwamba huyo CAG aondolewe kazini kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya tabia mbaya, basi rais atamwondoa kazini.

Wakati wa uchunguzi, rais anaweza kumsimamisha kazi CAG. Lakini uamuzi huo utabatilika ikiwa Tume itamshauri rais kwamba huyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu asiondolewe kazini.

Mada zinazohusiana