Spika Job Ndugai 'afafanua' sakata la CAG nchini Tanzania

Spika Ndugai Haki miliki ya picha BUNGE
Image caption Spika Ndugai asema hatafanya kazi na Prof Assad na si ofisi ya CAG.

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ametoa ufafanuzi kuwa azimio lilopitishwa na Bunge ni kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na si ofisi yake.

Ndugai ametoa kauli hiyo Alhamisi mchana Aprili 4, 2019 Bungeni baada ya suala hilo kuzua mjadala mkubwa nchini.

"Hakuna wakati wowote ambao Bunge limekataa kufanya kazi na taasisi ambayo ni ofisi ya CAG. Bunge hili limekataa kufanya kazi na mtu anayeitwa Profesa Assad basi. Tusiripoti tofauti tukauchonganisha umma na kuuchanganya," amesema Ndugai.

Jumanne Bunge lilipitisha azimio la kutofanya kazi na Profesa Assad kwa sababu ya kauli yake aliyoitoa wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Bunge ni dhaifu.

Mgororo uliopo ulianza Disemba 2018 baada ya CAG kuiambia Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.

"…Kama tunatoa ripoti na inaonekana kuna ubadhilifu halafu hatua hazichukuliwi huo kwangu mimi ni udhaifu kwa Bunge. Bunge linatakiwa liisimamie (serikali) na kuhakikisha kuwa pahali penye matatizo basi hatua zinachukuliwa...Sie kazi yetu ni kutoa ripoti tu na huo udhaifu nafikiri ni jambo la kusikitisha lakini ni jambo tunaamini muda si mrefu huenda likarekebishika. Lakini tatizo kubwa tunahisi kwamba bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa," Profesa Assad aliiambia radio ya UN.

Haki miliki ya picha NAOT
Image caption CAG Prof Mussa Assad amesema ataendelea kutekeleza majukumu yake kikatiba.

Spika Ndugai alilieleza Bunge mwezi Januari kuwa maelezo ya Assad yalioonesha dharau kubwa dhidi ya mhimili huo na kumtaka aende mbele ya kamati Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa hiyari yake, ama apelekwe kwa pingu.

Hata hivyo, alipohojiwa na kamati hiyo, Assad aliendeleza msimamo wake.

Jana, Prof Assad alitahadharisha kuwa mzozo guo baina yake na Bunge unaweza kuzaa mgogoro wa kikatiba.

"Tunaweza kuwa na mgogoro wa kikatiba, kwamba ripoti (za ukaguzi wa mwaka 2017-18) zimeshawasilishwa kwa Raisi na mimi siwakilishi ripoti Bungeni, basi raisi atazipeleka ndani ya siku sita zijazona kama Bunge likikataa kuzipokea hiyo ni tatizo kubwa zaidi. Ni dharau (kwa katiba) wasiwasi wangu ni huo. Zikiwasilishwa bungeni zinakuwa mali ya umma na mimi napata nafasi ya kuzungumza, na hilo pia linaweza kuwa tatizo. Tafsiri ya kuwa (Bunge) hatuwezi kufanya kazi na CAG ni pana sana na inatakiwa tuijue vizuri," Prof Assad aliliambia shirika la utangazaji la umma TBC.

Pia alidai ni ngumu kumtofautisha yeye na ofisi yake.

Marufuku kwa wanahabari

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai amepiga marufuku waandishi wa habari waliopo Bungeni kuhoji wabunge waliosusia kikao.

Ndugai ameonya kuwa mwanahabari yeyote atakayekaidi katazo lake ataondolewa bungeni.

Amri hiyo ya Ndugai imekuja baada ya baadhi ya wabunge wa upinzani kutoka nje ya ukumbi wakionesha ghadhabu zao baada ya mbunge Godbless Lema (Chadema-Arusha Mjini) kupewa adhabu ya kutohudhuria viakao vitatu vya bunge kuanzia leo.

Adhabu hiyo imetolewa baada ya Lema jana kuunga mkono kauli ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali Prof Mussa Assad kuwa "bunge ni dhaifu".

Mbunge mwengine wa Chadema Bi Halima Mdee ambaye pia amefungiwa kuhudhuria vikao viwili vya Bunge kwa kuunga mkono kauli hiyo.

Kwa upande wa CAG bunge hilo limeazimia kutokufanya kazi naye kabisa.

Kwa mujibu wa mtandao wa twita wa gazeti la Nipashe la nchini Tanzania,

Mada zinazohusiana